Mambo matatu muhimu ya kukusaidia wakati wa changamoto maishani

Iliyochapishwa

Kuna wakati ambao unazongwa na mitihani ya maisha kiasi cha kuhisi unapanda mlima kila siku, na kila asubuhi unapoamka, mlima ule bado uko pale pale unakukodolea macho.

Je ni changamoto gani maishani ambayo umepitia na kuhisi maisha yako yamefika mwisho?

Inasemekana kwamba ukakamavu ni uwezo wa kwendana na hali inayotatiza au kukabiliana na changamoto.

Lucy Hone ni mkurugenzi wa taasisi inayoangazia ustawi na namna ya kuwa mkakamavu wakati unapitia changamoto maishani huko New Zealand.

Bi. Hone ni mtaalamu na sio tu kwa masomo na taaluma yake lakini pia kwasababu ukakamavu wake ulipitia changamoto kubwa mwaka 2014.

"Abi wangu mdogo, ambaye alikuwa na umri wa miaka 12 wakati huo, alikuwa ameenda kutembea na rafiki yake mpendwa Ella, na mama yake Ella, ambaye pia alikuwa rafiki yangu wa dhati.

Wakati wanarejea nyumbani kutoka matembezi yao, dereva wao aliendesha gari kwa kasi ya juu mno na badala ya kupunguza kasi alipokaribia kulikokuwa na ishara ya kusimama barabarani, alifululiza moja kwa moja na wote watatu wakafariki dunia papo hapo.

''Hii ndio sababu ninasema nina kiwango fulani cha ukakamavu wa kukabiliana na changamoto. Kweli nilikuwa nimesomea nyanja hiyo lakini nililazimika kuangalia tena kitu gani kinachoweza kunisaidia kukabiliana na hali hii'', amesema Bi Hones.

Kwasasa Bi. Hone amekiri yeye ni mwenye bahati kwasababu anaweza kusema wakati anakumbana na changamoto hiyo alikuwa anaufahamu wa namna ya kukabiliana na majaribu, iwapo atapitia hatua ngumu zaidi maishani mwake.

Lakini anasisitiza kwamba, kwa bahati mbaya mara nyingi watu huchukulia ukakamavu kama kitu binafsi licha ya kufahamu fika kuwa ni zaidi ya hilo.

Miujiza wakati kama huo ni kile kinachochukuliwa kuwa kawaida tu

Mikakati ifuatayo Bi. Hone aliitegemea sana wakati anapitia changamoto baada ya jamaa wake watatu kufariki dunia kwa wakati mmoja na bado anaitumia hadi hii leo:

1. Kuelewa kwamba changamoto ni sehemu ya maisha

Haijalishi unapitia nini, ama uwe umepewa talaka, umefutwa kazi, au kumpoteza mpendwa wako, inakuwa vigumu sana kukabiliana na changamoto husika wakati huo.

Unapopitia magumu kama hayo, kufahamu kwamba machungu na changamoto ni kawaida huwa hatua muhimu sana maishani na kunasaidia kuzuia kujiona mpweke kaisi cha hata kuhisi maisha yamekosa maana.

2. Fuatilia mambo yanayokufahirisha

Katika hali kama hizo, sikiliza na fuatilia kile kinachopelekea wewe kuwa na fikra njema.

Mwanadamu ana uzoefu mzuri sana wa kutambua na kupeleka fikra kwa yote ambayo ni mabaya. Lakini sio rahisi kwake kuanza kufikiria vitu au mambo mazuri yanayompa kumbukumbu za kumletea tabasamu na fikra njema.

Kuna umuhimu mkubwa wa kutoa angalizo kwa mambo yanayokuletea faraja na furaha ili kuweza kukabiliana na athari zitokanazo na changamoto unazopitia.

Watu wakakamavu huangalia kwa makini sana kile watakachokipa kipaumbele.

3. "Je hili linakusaidia au kukuumiza zaidi?"

Jiulize, "Je kile ninachofikiria au kutenda kwa wakati huu kinanisaidia au kinazuia juhudi zangu za kukabiliana na changamoto ninayopitia?"

Mara nyingi, watu hufikiria kwamba kuwa imara, wa thamani na mkakamavu kunamaanisha kupitia changamoto kimya kimya, bila kuhusisha wengine vile unavyohisi, lakini huo si ukweli.

Kuwa mkakamavu pia ni uwezo wa kukubali hali, kujua ni lini unastahili kuitisha usaidizi na kuwasiliana.

Utafiti unaonesha kwamba kuwa na uhusiano imara wenye kukusaidia na kukuunga mkono huenda ndio njia ya msingi ya kuimarisha uthabiti wako, kukupa ukakamavu na kukabiliana na changamoto unayopitia.

Bi. Hone aliyepoteza wapendwa wake watatu anasema yeye na mume wake walikuwa na bahati sana binti yao alipofariki dunia.

''Tulikuwa na jamii iliyotusaidia na kuwa na sisi kwa kila namna kipindi kile, jambo ambalo lilitusaidia sana. Na hicho tu ndicho unachohitaji wakati unapokumbana na changamoto, au majanga ya aina hiyo.

Hakuna anayeweza kupitia hilo peke yake.

Katika moja ya utafiti, Chris Peterson, alielezea utafiti wake wa muda mrefu kwa maneno machache tu: "Watu wengine ni muhimu. "

Pia unaweza kutazama: