Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wadukuzi wa mtandao wa Urusi, China na Iran walenga taarifa za Trump na Biden, Microsoft imesema
Wadukuzi wenye uhusiano na Urusi China na Iran wanajaribu kuingilia taarifa za watu na makundi yanayohusika na uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2020 , Microsoft imesema.
Wadukuzi wa Urusi ambao waliweza kuingilia kampeni za mwaka 2016 za chama cha Democratic kwa mara nyingine tena wamehusika katika udukuzi wa sasa, imesema kampuni hiyo ya teknolojia.
Microsoft imesema ilikuwa "wazi kwamba shughuli za makundi ya kigeni yalifanya juhudi zao " kuulenga uchaguzi.
Kampeni ya Donald Trump na hasimu wake upande wa Democratic Joe Biden zinalengwa katika tovuti za mashambulio ya kimtandao .
Wadukuzi kutoka kikundi cha Strotium wamelenga zaidi ya makampuni 200 ambayo mengi kati yake yana uhusiano na vyama vya kisiasa vya Marekani-vyote cha Warepublicans na Wademocrats, imesema taarifa ya Microsoft.
Washambuliaji wa kimtandao pia walilenga vyama vya kisiasa vya Uingereza, imesema Microsoft, bila kuvitaja ni vipi.
Strontium pia kinafahamika kama Fancy Bear, kitengo cha mashambulio ya kimtandao kinachodaiwa kuwa na uhusiano na idara ya ujasusi ya jeshi la Urusi, GRU.
Microsoft imesema nini kingine?
"Sawa na kile kilikchoshuhudiwa mwaka 2016, Strontium imeanza harakati za kuvuna taarifa za watu za kuingia kwenye mtandao au kuharibu akaunti zao za mtandao jambo ambalo linaaminiwa kuwa linalenga kukusanya taarifa za kijasusi au kuvuruga utendaji ," alisema Tom Burt, makamu rais wa Microsoft anayehusika na usalama na uaminifu.
Kampuni hiyo imesema kuwa wadukuzi wa China walikuwa wameanza kuwalenga watu binafsi wenye uhusiano na kampeni ya Bwana Biden, huku wadukuzi wa Iran wakiendelea na juhusi za kuwalenga watu wenye uhusiano na kampeni ya Trump.
Mengi kati ya mashambulio ya kimtandao hayakuweza kufanikiwa, kwa mujibu wa Microsoft. Mashambulio hayo pia hayakuwa yamefanywa kwa makundi ambayo yanashuhghulikia mifumo ya upigaji kura yenyewe.
"Kile tulichokiona ni kuendelea kwa aina ya mashambulio ya awali ambayo hayawalengi wagombea pekee na wafanyakazi wa kampeni lakini pia wale ambao wanawaomba ushauri juu ya masuala muhimu ," Bwana Burt alisema.
"Shughuli hizi zinaonesha haja kwa watu na makampuni yanayohusika katika mchakato wa kisiasa kutumia fursa ya usaidizi wa kimtandao unaotolewa bure na wa garama nafuu kujilinda wenyewe dhidi ya mashambulio wakati tunakaribia siku ya uchaguzi ."
Microsoft iliripoti kuwa makundi ya kichina yalikuwa yameanza mashambulio dhidi ya akaunti za barua pepe za watu binafsi na za watu wenye uhusiano na kampeni ya Biden, na " takriban mmoja wa watu maarufu ambaye zamani alikuwa na ushirika na utawala wa Trump ".
"Watu binafisi maarufu" katika jamii ya masuala ya kimataifa , taasisi za masomo na makampuni ya sera pia yalilengwa na kundi la wadukuzi wa China , linalofahamika kama Zirconium.
Kikundi cha Iran kinachofahamika kama Phosphorus hakikufanikiwa kuzifikia akaunti za maafisa wa Ikulu ya Marekani -White House na wafanyakazi wa kampeni za Bwana Trump kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu kilipojaribu kushambulia.
Microsoft haikuweza kubaini lengo la wadukuzi wa Urusi, China na Iran lilikuwa ni lipi. Google ilisema kuwa mwezi Juni kwamba iligundua majaribio sawa na hayo ya udukuzi wa kimtandao ya China na Iran.
Naibu waziri wa masuala ya habari za kampeni ya kitaifa ya Bwana Trump Thea McDonald amesema: "Sisi ni walengwa wakubwa, kwa hiyo haishangazi kuona shughuli zenye nia mbaya zilizoelekezwa katika kampeni na wafanyanyazi wetu ."
Afisa wa kampeni ya Biden alisema: "Tulifahamu kuanzia mwanzo wa kampeni kwamba tutalengwa na mashambulio na tumejiandaa kwa ajili yao."
Ripoti hiyo imekuja siku moja baada ya mfichuzi katika wizara ya usalama wa ndani nchini Marekani kudai kuwa alishinikizwa kusema uongo juu ya uingiliaji wa Urusi kwasababu ulimfanya rais ''aonekane vibaya ".
Utawala wa Trump umejibu vipi ?
Afisa w angazi ya juu wa wizara ya usalama wa ndani ya nchi , Christopher Krebs, amesema kuwa onyo la Microsoft linathibitisha kile ambacho tayari kilikuwa kimesemwa na majasusi wa Marekani
" Ni muhimu kusema kwamba hakuna mashambulio yoyote yaliyohusika katika shughuli za utendaji wa miundombinu ya upigaji kura na hakuna athari iliyobainika kwenye mifumo ya uchaguzi ," Bwana Krebs alisema.
Mapema Alhamisi, utawala wa Trump ulishitaki kampuni ya taifa ya Urusi kwa njama za kuingilia mchakato wa kisiasa wa Marekani.
Wizara ya fedha ya Marekani pia ilimuwekea vikwazo mbunge wa Moscow - mwenye uhusiano na Ukraine, Andrii Derkach, ambaye anashutumiwa kwa uingiliaji sawa na huo.
Bwana Derkach anadaiwa kutoa sauti iliyohaririwa ambayo ililenga kumchafulia sifa mgombea wa Democrat Joe Biden. Sauti hiyo iliyorekodiwa imekuwa ikitumiwa Rais Donald Trump.
Rais huyo wa Ukraine alikutana na wakili binafsi wa Trump, Rudy Giuliani, mwezi Disemba mwaka jana.
Je Ujasusi wa Marekani umesemaje?
Idara za ujasusi za Marekani zilisema kuwa mwezi Agosti kwamba China,Urusi na Iran walikuwa wanafanya juhudi za kuvuruga uchaguzi ujao.
Tathmini yao ilibaini kuwa Urusi ilikuwa inataka "kumdhalilisha" Bwana Biden Pia walibaini kuwa China na Iran walitaka Bwana Trump apoteze kura.
Ujasisi wa Marekani ulionya Iran, inaweza kujaribu "kuvuruga" taasisi za demokrasia za Marekani na rais kupitia maudhui ya mtandaoni.
Ni nini kilichotokea mwaka 2016?
Mashirika ya ujasusi ya Marekani yalisema kwamba mwaka 2016 Urusi ilikuwa nyuma ya juhudi za kuvuruga kampeni za uchaguzi za Hillary Clinton, huku taifa likiidhinisha harakati za mashambulio ya kimtandao na taarifa gushi zilipandikizwa kwenye mitandao ya kijamii.
Uchunguzi wa mshauri maalumu Robert Mueller ulibaini kuwa wadukuzi wa Urusi waliweza kufikia mifumo ya kamati ya taifa ya chama cha Democratic pamoja na barua pepe za mwenyekiti wa kampeni wa Bi Clinton John Podesta.
Walifichua maelfu ya barua pepe kutoka kwenye kampeni.
Baadaye Facebook ilitoa ushahidi kwamba maudhui yaliyoungwa mkono na Urusi yaliyotumwa wakati wa uchaguzi yaliwafikia Wamarekani milioni 126 kwenye mtandao huo.
Bwana Mueller hakubaini kwamba kampeni ya Trump ilishirikiana na na Urusi katika madai ya kuvuruga uchaguzi.