Lampedusa: Muhamiaji mwanamke mwenye virusi vya corona ajifungua ndani ya helikopta

Chanzo cha picha, EPA
Muhamiaji mwanamke ambaye alipatikana na virusi vya corona baada ya kupimwa amejifungua mtoto ndani ya helikoptawa wakati alipokuwa alisafirishwa kwenda hospitali kutoka kwenye kituo cha wahamiaji nchini Italia kilichopo katika kisiwa cha Lampedusa.
Italia inasema kuwa imeshuhudia ongezeko la wahamiaji wanaowasili mwaka huu.
Meli ya uokozi ilipewa ruhusa Jumanne kuwasafirisha wahamiaji 353 waliookolewa kwenye kisiwa cha Sicily baada ya kupigiwa simu na Umoja wa Mataifa ulioitaka iwaokoe.
Wakati huo huo, meli ya mafuta iliyokuwa na wahamiaji 27 ndani yake imeomba upya isaidiwe kuwafikisha wahamiaji kwenye mwambao wa Italia.
Meli ya hiyo ya kibiashara , Maersk Etienne, inasema iliwaokoa wahamiaji hao kufuatia ombi la Malta mapema mwezi Agosti lakini tangu wakati huo imeachwa baharini. Wafanyakazi wake wanasema watu waliomo "wana hali mbaya".
Nini kilichotokea Lampedusa?
Mwanamke alikuwa amepatikana na virusi vya corona wakati alipopata uchungu wa uzazi.
Alikuwa anaishi katika kituo kinachowashikilia wahamiaji ambacho kilikuwa kimejaa wahamiaji mara kumi ya uwezo wake wa kawaida, kulingana taarifa za shirika la habari la Reuters.
Maafisa wanasema waliamua kumuhamishia katika hospitali ya mji mkuu wa Sicily Palermo -ambayo ilikuwa umbali wa mwendo wa saa moja kwakwa ndege - ili aweze kujifungua kwa usalama. Lakini akajifungua safarini ndani ya ndege.
Mwanamke huyo ambaye bado hajatambuliwa-kwa sasa yuko katika hospitali ya Palermo pamoja na mtoto wake mchanga.
Tukio hilo limetokea huku kukiwa na mzozo baina ya watawala wa kisiwa cha Sicily na serikali ya taifa, huku Gavana wa Sicily Nello Musumeci akiishutumu serikali kuu ya Roma kwa kutompatia msaada wa kutosha wa kushughulikia wahamiaji wanaowasili kutoka Afrika.
Wahamiaji wapatao 19,400 wamewasili kwenye maeneo ya mwambao wa Italia hadi sasa mwaka huu, ikilinganishwa na wahamiaji wapatao 5,200 waliowasili katika kipindi sawa na hicho mwaka jana, kwa mujibu wa taarifa zilizoangaliwa na shirika la habari la Reuters.
Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya 40,000 wamewasili Ulaya kupitia baharini katika 2020 na watu 443 wamekufa au wamepotea walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterranean wakitokea Afrika magharibi.
Vipi kuhusu waliokwama katika bahari?
Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi Jumamosi lilitoa wito wa kuruhusiwa kwa mamia ya wahamiaji na wakimbizi waliokwama kwenye meli katika bahari ya Mediterranean waruhusiwe kuondoka salama.
Katika pamoja na Shirika la Umoja wa mataifa la wahamiaji, lilisema kuwa ni "muhimu kunusuru maisha ".
Walinzi wa mwambao wa Italia waliwaokoa watu 49 kutoka katika chombo kilichokua kimejaa kupita uwezo kilichodhaminiwa na msanii wa Uingereza Banksy mwishoni mwa juma.
Shirika lisilo la kiserikali lililoikoa meli ya Sea Watch 4 lilisema wahamiaji 353 walipanda meli hiyo baada ya kupewa ruhusa Jumanne ya kutia nanga katika eneo la Palermo. Kwanza watahamishiwa katika meli kwa ajili ya kukaa karantini, lilisema.
Meli ya kibiashara ya mafuta yenye wahamiaji 27, akiwemo mwanamke mjamzito na mtoto mdogo mmoja, bado imesalia ndani ya bahari na wahudumu wake wanatoa wito wa "msaada wa dharura wa kibinadamu na kuondoka salama ."

Chanzo cha picha, Maersk Tankers
Wahudumu wa meli yenye bendera ya Denmark- Maersk Etienne ilisema kuwa iliwaokoa wahamiaji tarehe 5 Agosti Tkwa ombi la mamlaka za Malta, lakini tangu wakati huo imetelekezwa ndani ya bahari.
"Umekuwa ni muda mrefu sasa, siku 27 tangu tulipoitwa na maafisa wa Malta kuwachukua wahamiaji 27," Tommy Thomassen, afisa mkuu wa masuala ya kiufundi wa meli ya mafuta ya Maersk aliiambia BBC.
"Tuna hali mbaya na tunalilia jamii ya kimataifa itusaidie ," alisema.
Bwana Thomassen alisema kuwa meli hiyo "haina muundo wala vifaa'' vya kuwabeba wahamiaji, ambao wamekuwa wakilala kwenye madawati.
"Wahudumu wamefanya kila wawezalo kuwasaidia wahamiaji waishi maisha yanayokubalika, lakini sio hali ambayo ungependa mtu yeyote aiishi kwa kipindi kirefu ," alisema.












