Trump, Biden washutumiana kuhusu vurugu zinazotokea nchini humo

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Rais wa Marekani Donald Trump na mpinzani wake wa Democratic Joe Biden wameshutumiana kutokana na vurugu zilizotokea huko Portland, Oregon.

Bwana Trump amemlaumu meya wa Democrat huko Portland, Ted Wheeler, kwa kuruhusu kutokea kwa kifo na uharibifu mjini humo.

Lakini Bwana Biden amesema rais alikuwa anachochea vurugu hizo.

Mwanaume mmoja alipigwa risasi huko Portland Jumamosi huku kwingineko mjini humo wanaopendelea Trump walikabiliana na waandamanaji wa Black Lives Matter.

Portland imekuwa kitovu cha maandamano dhidi ya ukatili unaotekelezwa na polisi na ubaguzi wa rangi tangu kutokea kwa mauaji ya George Floyd, Mmarekani mweusi huko Minneapolis, Mei 25 na kusababisha ghadhabu nchini na hata kimataifa.

'Hii ni Marekani ya Trump'

Katika msururu wa ujumbe wa Twitter Jumapili, Bwana Trump alisema kwamba "Portland haiwezi kujikwamua kutokana na hali hiyo kwa kuwa na meya mpumbavu", na kupendekeza kwamba atapeleka majeshi ya serikali mjini humo. Pia amemshutumu Bwana Biden kwa "kutokuwa na ari ya uongozi ".

Katika taarifa, Bwana Biden amesema: "[Trump] anaweza kufikiria kwamba kuandika kuhusu sheria na utaratibu kwenye mtandao wa Twitter kunafanya aonekane imara - lakini kushindwa kwake kushawishi wafuasi wake wasizue vurugu kunaonesha udhaifu wake."

Sheria na utaratibu ndio imekuwa maudhui makubwa ya Rais Trump anapotafuta kuchaguliwa tena, na kufanya wafuasi wa Democtrats na mgombea wao Joe Biden kuonekana kama wasio na msimamo thabiti kuhusu uhalifu.

Awali, kaimu waziri wa mambo ya ndani Chad Wolf alisema maafisa wa Democrats huko Portland waliruhusu uvunjaji wa sheria na kutokea kwa ghasia na kuongeza kwamba machaguo yote ya kutatua ghasia zilizotokea yalikuwa wazi.

Kwa upande wake, Democrats wamejibu kwa kusema ghasia hizo zinatokea chini ya uongozi wa Trump na kumshutumu kwa kufanya hali kuwa mbaya zaidi kwa kejeli zake.

Meya Wheeler amesema Trump ndio "aliyesababisha chuki na mgawanyiko.

"Ningeshukuru ikiwa rais angetuunga mkono au kujitenga na sisi," amesema.

Waathirka 'waliunga mkono mrengo wa kulia'

Polisi inachunguza ufyatuaji wa risasi mjini humo ambako kumesababisha maandamano ya miezi kadhaa.

"Maafisa wa polisi Portland walisikia milio ya risasi ikitokea barabara ya Alder. Walichukua hatua na kubaini mwathirika aliyekuwa amepigwa risasi na kujeruhiwa kifuani," Polisi huko Portland imesema kwenye taarifa.

Picha nyingine inaonesha polisi wakijaribu kumshika mtu aliyekuwa na yule aliyepigwa risasi.

Polisi bado haijatambua mwanaume aliyefariki au kuthibitisha kwamba ufyatuaji wa risasi una uhusiano na makabiliano yaliyozuka moja kwa moja katika mji huo.

Bila kumtaja jina lake, mwasisi wa kundi la mrengo wa kulia Patriot Prayer, amesema mwathirika alikuwa "mfuasi na rafiki mzuri", shirika la habari la Associated Press limesema.

Mauaji hayo yametokea huku kukiwa na mapigano kati ya wafuasi wa Trump na waandamanaji wa Black Lives Matter katikati ya mji.

Wasiwasi uliongezeka pale msafara wa magari 600 uliokuwa unapeperusha bendera na kubeba takribani wafuasi 1,000 wa Trump waliokuwa wamekusanyika katika duka kubwa kaunti ya Clackmas viungani mwa mji kuingia mji wa Portland.

Watu kumi wamekamatwa kwasababu ya makabiliano hayo, polisi imesema.

Wiki muhimu sana kwa Trump

Peter Bowes, mwanahabari wa BBC Amerika Kaskazini.

Ghasia zinazoendelea Marekani zinasababisha kuangazia kampeni ya kuchaguliwa tena kwa Donald Trump - kushutumu miji ambayo ni ngome kwa Democtrats, ambapo migogoro mingi imetokea na kuonesha twasira ya kuwa ni rais anayependelea utekelezaji wa sheria.

Portland imekuwa kitovu cha maandamano ya Black Lives Matter tangu mauaji ya George Floyd lakini kukutana kwa wafuasi wanaopendelea Trump na maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi kumefanya hali kuwa mbaya zaidi.

Akiandika ujumbe kweye mtandao wa Twitter" Sheria na Utaratibu!!!" saa kadhaa baada ya kutokea kwa maandamano, Bwana Trump ameweka wazi kwamba suala hilo ndio litakalotawala wito wake wa kutaka kuchaguliwa tena madarakani kwa muhula wa pili.

Hii huenda ikawa wiki muhimu kwake. Jumanne, rais atakuwa anaelekea Kenosha jimbo la Wisconsin, eneo ambalo linapitia msukosuko wa kisiasa kwenye maandamano ya ghasia yalisababishwa na tukio la Jacob Blake kufyatuliwa risasi.

Lengo la ziara hiyo limeelezewa kuwa Bwana Trump atakutana na polisi wa eneo na kutathinimi uharibifu uliotokana na maandamano ya hivi karibuni.

Wamarekani wengi watakuwa wanafuatilia kuona ikiwa rais pia atazungumza na Bwana Blake na familia yake na ikiwa ataonesha hisia ya kuwa pamoja na wenye kukasirishwa na unyama unaotekelezwa na polisi.