Jacob Blake: Afisa wa polisi aliyempiga risasi mtu mweusi huko Kenosha Marekani atajwa

Jacob Blake alipigwa risasi mara saba mgongoni na polisi

Chanzo cha picha, BENCRUMP.COM

Maelezo ya picha, Jacob Blake alipigwa risasi mara saba mgongoni na polisi
Iliyochapishwa

Mwanasheria mkuu wa Wisconsin amemtaja afisa wa polisi aliyempiga risasi Mmarekani mweusi siku ya Jumapili, katika tukio ambalo limesabbaisha maandamano ya siku kadhaa.

Josh Kaul aliwambia wanahabari siku ya Jumatano kwamba Rusten Sheskey alimpiga risasi saba Jacob Blake mgongoni alipokuwa akifungua mlango wa gari lake.

Maafisa walipata kisu katika gari la bwana Blake, lakini aliongeza hakukua na silaha zingine.

Tukio la kupigwa risasi kwa Blake katika mazingira ya kutatanisha limesababisha maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa katika siku za hivu karibuni, baadhi zikigeuka kuwa ghasia.

Kijana wa miaka 17 amekamatwa siku ya Jamatano baaada ya watu wawili kuuawa na mwengine kujeruhiwa katika maandamano ya Jumanne usiku

Bwana Blake anaendelea kupokea matibabu japo amepoteza fahamu, lakini mawakili wake wanahofia itakuwa "miujiza" kwake kutembea tena.

Mwanasheria mkuu amtaja afisa wa polisi aliehusika na shambulio dhidi ya Jacob Blake huko Kenosha
Maelezo ya picha, Mwanasheria mkuu amtaja afisa wa polisi aliehusika na shambulio dhidi ya Jacob Blake huko Kenosha

Rais wa Marekani Donald Trump ametuma maafisa wa ulinzi wa taifa kudhibiti usalama mjini Kenosha, na kuandika ujumbe katika Twitter yake kuwa wamepelekwa kukabiliana na "wizi, uteketezaji, ghasia, na uharibifu uliofanywa kwa jumla katika barabara za Marekani".

Idara ya Haki imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa cha kupigwa risasi kwa Bwana Blake. Imetuma zaidii ya maajenti 200 wa shirika la upelelezi la Marekani FBI katika mji huo, kwa mujibu wa msemaji wake.

Muda mfupi baada ya ujumbe wa Twitter wa Bwana Trump, Gavana wa Wisconsin Tony Evers alisema amewaruhusu maafisa wa walinzi wa taifa 500 kusaidia katika juhudi za kudumisha usalama licha ya hofu kwamba ghasia huenda zikaongezeka.

Maandamano pia yamesambaa hadi miji mingine ya Marekani, ikiwa ni pamoja na Portland, Oregon na katika maeneo ya Minneapolis, Minnesota, ambako mauaji ya Mmarekani mweusi aliyekuwa hakujihami George Floyd mwezi Mei yalisababisha maandamano ya Black Lives Matter kote nchini Marekani na kwengineko duniani.

Mwanasheria mkuu alisema nini?

Siku ya Jumatano Bw. Kaul iliwaelezea wanahabari kuhusu uchunguzi unaoendelea kufuatia tukio hilo

Maafisa walikuwa wameitwa katika eneo la tukio siku ya Jumapili baada ya mwanamke kuripoti kuwa "mpenzi wake amefika katika jengo hilo wakati hakutakiwa kufika hapo".

Mawakili wa Bw. Blake wamesema alikuwa akijaribu "kuzuia mzozo wa kinyumbani" polisi walipomshambulia kwa silaha

Walipofika hapo walijaribu kumkamata, kwa kutumia kifaa maalum dhidi yake. Baada ya Bw. Blake kufungua mlango wa gari lake, Afisa Rusten Sheskey - ambaye amehudumu katika idara ya polisi ya Kenosha kwa miaka saba - alimpiga Blake risasi saba mgongoni.

"Hakuna afisa mwengine aliyetumia silaha yake," Bwana Kaul alisema.

Bwana Blake alikuwa amewaambia wachunguzi kwamba alikuwa na kisu, na Bw. Kaul amesema kuwa maaafisa "walipata kisu ndani ya gari upande wa dereva. Na hawakupata silaha nyingine ndani ya gari hilo.

Mwanasheria mkuu wa Wisconsin pia alizungumzia ghasia za hivi karibuni katika mji huo akitaja kuwa ya "kughadhabisha".

Alisema kuna baadhi ya watu "waliojihusisha na visa vya uharibifu na ambao sio wakaazi wa Kenosha au kutoka Jimbo la Wisconsin".

"Kile wanachofanya ni kusababisha vurugu," alisema, akiongeza kuwa watu wa Kenosha "wanastahili kupewa nafasi ya kujieleza, kupitia maandamano ya amani [na] kushinikiza mageuzi wanayotaka yafanyike."

Nini kilifanyika Jumanne?

Kumeshuhudiwa siku kadhaa za maandamano ya ghasia tangu bwana Blake alipopigwa risasi.

Siku ya Jumanne, kundi dogo la watu liliwarushia polisi fataki na chupa za maji mjini Kenosha, lakini polisi hao walijibu kwa kutumia vitoa machozi na risasi za mpira.

Msemaji wa chama cha polisi aliiambia BBC kuwa watu binafsi na makundi kadhaa yanatoa ulinzi kwasababu maafisa wa usalama wamelemewa na waandamanaji..

Kanda za video katika mitandao ya kijamii, zilionesha mtu aliekuwa na bunduki akifukuzwa na kundi la watu kabla ya kuanguka chini na kuonekana kana kwamba anawafyatulia risasi.

Video zingine zilionesha raia waliojihami, baadhi yao wakiwa wamevalia mavazi yanayofanana na ya kijeshi, wakikusanyika nje ya maduka ya kibiashara wakisema wanatoa ulinzi.

Amri ya kutotoka nje hadi siku ya Jumapili imewekwa huku viongozi wa kijamii wakitoa wito kwa wakaazi kuzingatia amri hiyo.