Watu 97 waokolewa bahari ya Mediterania nchini Libya baada ya chombo kupoteza uelekeo

Iliyochapishwa

Watu 97, wameokolewa, wakiwemo watoto 28 kutoka kwenye boti iliyotengenezwa kwa mpira iliyokuwa imepoteza uelekeo na kusombwa na maji katika bahari ya Mediterania umbali wa maili 30 kutoka pwani ya Libya, waangalizi wa kimataifa wa bahari wameeleza.

Inaaminika kuwa boti hiyo ilitokea nchini Libya.

Kikosi cha uokoaji na meli ya shirika la Sea- Watch waligundua chombo hicho siku ya Jumapili asubuhi, msemaji Oliver Kulikowski ameiambia BBC.

Watu waliookolewa walikuwa wamechoka na walikuwa wamepungukiwa maji mwilini, aliongeza.

Bado watu hao hawajajulikana kuwa raia wa nchi gani, kwa kuwa wakati huu wanaimarika afya zao kabla ya tathimini, alisema bwana Kulikowski.

Haijulikani mahali watakapopelekwa.

Tukio hilo limetokea siku nne baada ya takribani wahamiaji 45 na wakimbizi, wakiwemo watoto watano, kufa baada ya meli kuvunjika mwaka huu, Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR limeeleza.

UNHCR na shirika la uhamiaji (IOM) limetaka jitihada za utafutaji na uokoaji kuongezwa.

Mashirika yamesema bila jitihada za makusudi kufanyika katika operesheni hizo, maisha ya watu wengi zaidi yatapotea kwenye bahari ya Mediterania.

Shirika la Sea- Watch 4 inaendeshwa na muungano wa mashirika kadhaa, ikiwemo madaktari wasio na mipaka (MSF) chini ya mwamvuli wa United4Rescue.

Zaidi ya watu 300 wanaripotiwa kupoteza maisha wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kutokea Libya kuelekea Ulaya mwaka huu, huku takwimu zikiaminika kuwa kubwa zaidi.

Tangu kuangushwa kwa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi, Libya imekuwa njia muhimu ya wahamiaji kupita.

Lakini mazingira kwa wahamiaji ni hatari, huku Shirika la wakimbizi duniani UNHCR na IOM wakitahadharisha kuwa ''wako hatarini kutokana na mgogoro unaoendelea, na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ukamataji watu kiholela.''