Uchaguzi Tanzania 2020:Tundu Lissu kupeperusha bendera ya Chadema

Tundu Lissu

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Iliyochapishwa

Baraza Kuu la chama cha upinzani Chadema limemchagua Tundu Lissu kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa Tanzania Oktoba 28.

Lissu amejinyakulia kura 405 sawa na asilimia 91 akifuatiwa kwa mbali na Lazaro Nyalandu aliyepata kura 36 sawa na asilimia 8 na Maryrose Majige aliyepata kura 1 sawa na asilimia 0.23.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika amesema wajumbe 442 wamepiga kura katika kikao hicho na hakuna kura hata moja iliyoharibika,

Jina la Lissu sasa kupelekwa kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika kesho ili kupitishwa rasmi.

Wakati huohuo Baraza Kuu la Chadema limempitisha Salum Mwalimu kuwa Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.

Bwana Said Issa Mohammed pia amepitishwa na baraza hilo kuwa mgombea wa urais wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar.

Baada ya matokeo kutangazwa ukumbi ulilipuka kwa shangwe kutoka kwa wajumbe ambao ndio waliopiga kura.

Aliyeshika nafasi ya tatu katika kinyang'anyiro hicho, Maryrose Majige amewashukuru wajumbe wote kwa kumpa ushirikiano.

Lazaro Nyalandu (Kushoto) amepata kura 36 sawa na asilimia 8 na Maryrose Majige kura 1 sawa na asilimia 0.23

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Maelezo ya picha, Lazaro Nyalandu (Kushoto) amepata kura 36 sawa na asilimia 8 na Maryrose Majige amepata kura 1 sawa na asilimia 0.23

''Mimi kama mwanachadema nipo tayari kushirikiana kwa dhati na mgombea wetu atakayepeperusha bendera ya chama kuingia Ikulu''.

Mgombea aliyeshika nafasi ya pili Lazaro Nyalandu, amesema ''nimeyapokea matokeo hayo kwa mapenzi makubwa na kuwa ulikuwa ni wakati wa Tundu Lissu''.

Lissu amesema nini?

Akizungumza na baada ya kuchaguliwa, Lissu amesema ushindi wake ni wa chama na kazi mbele yao bado ni ngumu.

''Dada Rose sio mshindwa wala ndugu yangu Nyalandu sio mshindwa, mimi sio mshindi, ushindi ni wa chama chetu.''

''Hatua zinazofuata ndio ngumu zaidi...tujiandae kupiga kazi zaidi, tukatengeneze kimbunga kuelekea Oktoba''.

Sera za Lissu

Lissu amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa serikali ya Rais John Pombe Magufuli kwa miaka mitano iliyopita.

akizungumza kwa njia ya mtandao akiwa ughaibuni alisema: ''Nina wajibu wa kutaja kile kilichonisukuma kutaka kugombea nafasi hii ya juu kabisa kiungozi katika mfumo wa kikatiba wa nchi yetu yaani Rais wa Jamuhuri ya Muungano .''

Wajumbe 442 wamepiga kura katika kikao hicho na hakuna kura hata moja iliyoharibika

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Maelezo ya picha, Wajumbe 442 wamepiga kura katika kikao hicho na hakuna kura hata moja iliyoharibika

''Kwa kipindi cha miaka mitano itakayoishia Oktoba mwaka huu nchi yetu imetawaliwa na serikali ya Rais John Pombe Magufuli na Chama cha Mapinduzi , CCM kwa namna ambayo imeiweka nchi yetu katika

mtihani mkubwa kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia.Kwa mtihani huu nchi yetu iko njia panda, na kwa vyovyote vile itakavyokuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na umuhimu mkubwa katika historia ya nchi yetu''.

Lissu ameahidi kuendesha serikali yake kwa misingi ya katiba na kuheshimu uhuru wa mihimili mingine.

Amesema serikali yake itaandaa sera thabiti za kiuchumi zitazohakikisha kwamba serikali inabaki kama mwangalizi wa shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na sekta binafsi.

''Serikali yangu itakuwa msimamizi wa maslahi ya jumla ya wananchi ili kuhakikisha usalama wa bidhaa na udhibiti wa bei za bidhaa na huduma muhimu kwa ustawi wa wananchi''.

Lissu amesema serikali yake itafanya mageuzi makubwa katika mfumo wa utozaji kodi ili kuondoa utitiri wa kodi tofauti na hali ilivyo sasa.

Tundu Lissu alirejea Tanzania na kulakiwa na mamia ya wafuasi wake katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, Jumatatu Juma lililopita, karibu miaka mitatu tangu anusurike na jaribio la mauaji.