Serikali ya Tanzania imepiga marufuku kuratibu, kupanga maandamano mtandaoni

Kampeni za mtandaoni za kuunga mkono maandamano zimepigwa marufuku Tanzania. Kwa mujibu wa kanuni mpya za mitandao, ambazo zimeanza kufanya kazi mwezi uliopita, zinataka watoaji wa maudhui ya burudani, elimu na dini kupata leseni kutoka kwa mamlaka.
Katika orodha ya maudhui yaliyopigwa marufuku, kanuni hizo mpya pia zimeharamisha kutoa taarifa kuhusu milipuko ya maradhi ya kuambukiza bila idhini ya mamlaka.
Kanuni hizo ni mbadala wa kanuni ya maudhui ya mtandaoni ya mwaka 2018, ambayo wanaharakati waliikosoa wakisema ni kuingilia uhuru wa kujieleza.
Lakini kama ilivyokuwa kwa kanuni za mwaka 2018, kanuni za sasa zinaweza kutafsiriwa kwa namna ambayo itagusa pia makundi ya WhatsApp.
Ukiukaji wa kanuni ni jinai ambayo adhabu yake ni faini ambayo si chini ya shilingi milioni tano (takribani dola 2145) au kifungo cha miezi kumi na miwili au vyote kwa pamoja.
Kanuni hizo zinagusa maudhui kama ya mapenzi ya jinsia moja, maudhui yasiyo na staha, faragha, maudhui ya udhalilishaji, maudhui dhidi ya usalama wa Umma, maudhui yanayosababisha vurugu na kutishia usalama wa taifa.
Pia maudhui yanayogusa masuala ya dini, imani ya mtu binafsi, haki ya umiliki na masuala ya afya.
Taarifa kwa Umma ambayo inaweza kusababisha hali ya vurugu, matumizi ya lugha chafu, pia utoaji wa taarifa za uongo na taarifa za maudhui ya kupotosha.
Athari zitakazojitokeza
Wanaharakati wanasema kuwa kanuni hizi ni muendelezo tu wa kuminya watu kujieleza na kuminya uhuru wa watu kutoa taarifa
''Mfano katika kifungu cha nane kinachotoa adhabu kali ya kufutiwa leseni au kusimamishwa kwa wale watakaothubutu kukiuka''. Alisema Anna Henga Mkurugenzi mtendaji kituo sheria na haki za binadamu, LHRC
Bi Henga ameiambia BBC : ''Kuna vifungu viwili ambavyo ni vigumu sana kwa mfano kuhusu utoaji wa leseni kwa kanda, kwamba unatakakiwa kutoa taarifa za kanda husika na si vinginevyo''
Leseni zimegawanywa kutokana na maudhui, kama dini, habari za papohapo, hivyo itawawia vigumu watoa habari kutoa taarifa kuhusu maudhui ya namna nyingine.
Biashara haramu
Kanuni hizi mpya zinawagusa pia wale wafanyabiashara za mitandaoni ambao huweka maudhui ya kuwashawishi watu kwenye mitandao ya kijamii yanayohamasisha michezo ya kamari na bahati na sibu na biashara nyingine ya kufanana na hizo
Kanuni zinapiga marufuku kuweka mtandaoni maudhui ya kuhamasisha ''wito wa kuchochea uvunjaji wa kanuni na sheria'' kwa kuhimiza 'maandamano ' mtandaoni. ''Maudhui yanayojihusisha na upangaji, uratibu , na kuhamasisha maandamano.
Biashara mitandaoni
Kutangaza bidhaa mitandaoni hasa zile zisizo na leseni kumepigwa marufuku na kwamba adhabu itatolewa dhidi wafanya biashara hao.
Hii itawagusa wale wanaofanya biashara ya dawa (Suplements), za kupunguza uzito, vidonge vya urembo na krimu.
Kanuni hizi zimezua gumzo mtandaoni huku wanaharakati mbalimbali wakihoji kuhusu makali ya kanuni hizi na utekelezaji wake.












