Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni furaha kwa Zinedine Zidane baada ya Real Madrid kushinda taji la La liga Uhispania
Zinedine Zidane anasema kwamba ushindi wa taji la kwanza na Real Madrid baada ya kipindi cha miaka mitatu umemfurahisha zaidi ya kushinda kombe la klabu bingwa Ulaya.
Real ilikamilisha ushindi huo huku ikiwa imesalia na mechi moja kucheza baada ya kuishinda Villareal katika uwanja wa Alfredo Di Stefano uliokuwa hauna mashabiki.
Karim Benzema alifunga kupitia shambulio lililopita katikati ya miguu ya kipa Sergio Asenjo na kuongeza bao la pili kupitia mkwaju wa penalti.
Katika tukio la kushangaza Sergio Amos alisaidia katika jaribio la kwanza ambapo Benzema alifunga lakini juhudi hiyo ikakataliwa.
Vicente Iborra aliipatia timu yake bao la kufutia machozi ambalo halikubadili ushindi wa Real Madrid wa 34 wa taji la Uhispania.
Timu hiyo ya Zidane imeshinda mechi zote 10 ilizocheza tangu ligi ya Uhispania kuanza upya mwezi Juni.
Wanaingia katika mechi yao ya mwisho wakiwa na uongozi wa pointi saba mbele ya Bareclona waliopo katika nafasi ya pili.
''Hii ni bora zaidi ya chochote kile. Inachukua juhudi kubwa kushinda La Liga'', alisema mkufunzi huyo wa Real Madrid.
''Baada ya dakika 38 una pointi nyingi zaidi ya timu nyengine yoyote . Baada ya masharti ya kutotoka nje na kila kitu, ni kitu cha kufurahisha kwa kweli''.
''Hii leo ni mojawapo ya siku bora zaidi kwangu mimi kama mtaalamu'', alisema Zidane.
''Baada ya kila kilichotokea, likizo ya miezi mitatu, ni vyema tulichofanikiwa''.
Mataji ya La Liga yamekuwa machache ukilinganisha na yale ya klabu bingwa Ulaya muongo huu hili likiwa taji lao la tatu katika kipindi cha misimu yao tisa.
Walishinda mataji matatu mfululizo katika makombe ya Ulaya katika kipindi cha kwanza cha Zidane lakini walikuwa wakimaliza katika nafasi ya tatu tangu waliposhinda taji hilo kwa mara ya mwisho, ambapo Bareclona wamekuwa wakitawazwa kuwa mabingwa.
Zidane alikuwa mkufunzi wa klabu hiyo mara ya mwisho waliposhinda taji la ligi na kuliweka kama lango lake.
Ilionekana kana kwamba kikosi hicho cha raia huyo wa Ufaransa kitashindwa kuafikia lengo hilo wakati kandanda nchini Uhispania ilipoahirishwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona mwezi Machi huku Barcelona ikiwa juu ya jedwali.