Uchaguzi wa Tanzania 2020: Mahakama ya Afrika yataka Tanzania kuruhusu kupingwa kwa matokeo ya urais mahakamani

Iliyochapishwa

Mahakama ya Afrika imeamuru Tanzania kuviruhusu vyama vya siasa kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani

Katiba ya Tanzania hairuhusu mahakama kuhoji wala kupinga matokeo ya urais mara mshindi wa uchaguzi atakapokuwa ametangazwa na tume ya uchaguzi

Lakini jana, Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, yenye makao yake makuu jijini Arusha, Kaskazini mwa Tanzania, imeitaka Tanzania kuchukua hatua "za muhimu za kikatiba na za kisheria, ndani ya muda mwafaka" kubadilisha sheria hiyo inayozuia kupingwa kwa matokeo ya urais

Kesi hii ilipelekwa mahakamani hapo na Mtanzania na mwanasheria nguli wa haki za binadamu Jebra Kambole ambaye alihoji kwamba kifungu hicho cha sheria kinachozuia kupingwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais kinakiuka haki zake za msingi

Uamuzi huu wa mahakama ya Afrika unakuja wakati ambao matokeo ya uchaguzi wa urais ya nchi za jirani za Kenya na Malawi yalipingwa mahakamani na mahakama kuamuru marudio ya chaguzi hizo

Wakati marudio ya uchaguzi wa nchini Kenya yalisusiwa na vyama vya upinzani nchini humo, kurudiwa kwa uchaguzi nchini Malawi kulipelekea muungano wa vyama vya upinzani kushinda

Hata hivyo kutokana na siku chache kubakia hadi uchaguzi mkuu kufanyika, kuna uwezekano mdogo wa mabadiliko hayo kufanyika juu ya uchaguzi wa mwaka huu

Hii ina maana gani kwa raia wa Tanzania?

Mwanasheria Jebra Kambole ambaye ndiye aliyepeleka shauri hilo mahajamani amesema;

''Uamuzi huu una maana kubwa sana kwa Watanzania, kwanza kabisa lilikua suala la muda mrefu kwamba matokeo ya urais yanaweza kupingwa mahakamani au la.

Ni jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu sana kwa hiyo ina maanisha kuwa watu wataweza kuyapinga matokeo ya urais mahakamani ambapo kabla ya uamuzi huu mahakama ilikuwa haiwezi kusikiliza jambo lolote ambalo linahusiana na uchaguzi wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

''Hivyo ina maana kuwa haki za msingi za Watanzania zinaanza kuonesha mwanga na zinaweza kupatikana sasa''.Alisema

Jebra Kambole amesema nini?

Amesema kuwa alichochewa na namna ambavyo alikuwa akiona nchi nyingine zilizokuwa zimepiga hatua kwenye jambo hili, lakini Watanzania wameonekana kuwa nyuma sana kwenye masuala ya ulinzi wa haki za binaadamu Tanzania.

''Nilikuwa ninanung'unika na kusikitika sana kuona kwa nini sisi tunakuwa nyuma kwenye masuala ya ulinzi wa haki za binadamu? Hivyo hiki ndicho kilichokuwa kikinipa moyo sana kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha kuwa haya mambo yanakaa sawa Tanzania''. Alisema Bwana Kambole.

''Nchi kama Malawi, Kenya, Burundi, watu wanaweza kwenda mahakamani na kupinga matokeo ya urais. Tanzania nchi kubwa ambayo imejinasibu ina heshima kwa kufuata misingi ya haki za binadamu na utawala bora inakuwaje jambo hili tunaendelea kulikumbatia katika sheria zetu''? Alihoji kambole.

Mahakama imesema nini?

Imetamka wazi kwamba kifungu cha 41 kifungu kidogo cha 7 cha katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, kinakiuka mkataba wa Afrika Mashariki.

''Uamuzi huu una maana kwa kuwa sasa unatoa mwanya kwa kwa raia kuchukua hatua ya kupinga vipengele vingine vya katiba kuchukua hatua ya kwenda mahakamani''. Alisema Kambole.

Ndani ya miezi 12 Serikali ya Tanzania imetakiwa kupeleka ripoti katika mahakama ya Afrika kuonesha ni kwa kiasi gani imetekeleza uamuzi huo.

Jebra kambole amesema utekelezaji wa maamuzi hayo ni changamoto kubwa lakini wanalitazama suala hili kwa karibu na kuwa hatua hii ya Mahakama ya Afrika ni kubwa sana katika ukuaji wa demokrasia nchini Tanzania.