Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ajali ya ndege Iran: 'Kosa la kibinadamu' lilisababisha kudunguliwa kwa ndege ya Ukraine
Iran imesema kuwa makosa ya kibinadamu iyaliyofanywa na maafisa wake wa ulinzi yalisababisha kudunguliwa kimakosa kwa ndege ya abiria ya Ukraine mwezi Januari.
Katika ripoti iliyotolewa siku ya Jumamosi, Shirika linalosimamia usafiri wa anga nchini Iran (CAOI) lililaumu "makosa ya kibinadamu" na mawasiliano mabaya ya kijeshi.
Watu wote 176 waliokuwa wameabiri ndege hiyo walifariki ndege hiyo ilipolipuliwa kwa makombora mawili muda mfupi baada ya kuanza safari kutoka mjini Tehran.
Iran awali ilikana kuhusika na ajali hiyo.
Lakini baada ya maafisa wa intelijensia wa Ulaya kusema kwamba wana ushahidi wa kuthibitisha Iran ilihusika, nchi hiyo ilikiri makosa, ikisema kuwa ilidhani ndege hiyo ni kombora la kulipua meli.
Rais Iran Hassan Rouhani alielezea tukio hilo kuwa "kosa ambalo haliwezi kusamehewa".
Ndege hiyo ya shirika la ndege la kimataifa la Ukraine ilidunguliwa Januari 8, wakati kulikuwa na taharuki kubwa kati ya Iran na Marekani.
Vikosi vya ulinzi wa anga nchini Iran vilikuwa katika hali ya tahadhari wakati huo.
Saa kadhaa kabla ya tukio hilo, nchi hiyo ilikuwa imeshambulia kwa makombora ya masafa ya mbali kambi mbili za wanajeshi wa Marekani nchini Iraq katika hatua ya kulipiza kisasi kuuawa kwa jenerali wake wa ngazi ya jeshini Qasem Soleimani, katika shambolio lililofanywa na Marekani kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani mjini Baghdad.
Ripoti hiyo inasema nini?
Maelezo kamili ya ripoti CAOI haijatolewa kwa umma, lakini baadhi ya maelezo yake yamechapishwa na shirika la habari la Fars.
Katika matokeo ya uchunguzi wake, ripoti ya CAOI imesema ndege hiyo ya abiria ilikuwa ikisafiri katika njia ya kawaida ya ndege, lakini kitengo cha ulinzi wa angani cha majeshi ya Iran kilielekeza vifaa vyake upande huo bila kuzingatia kama vipo sawa au la. Kutokana na dosari hiyo walishindwa kutambua ndege hiyo ya abiria wakidhani ni silaha hatari.
Ripoti hiyo pia imesema kuwa maafisa wanaosimamia kitengo cha makombora hawakuweza kuwasiliana na kituo kikuu kupata idhini, hatua ambayo iliwafanya kulipua ndege hiyo.
"Laiti mawasiliano yangelikuwa sawa, ndege hiyo haingelilengwa," iliamua ripoti ya CAOI.
Mwezi uliopita mamlaka nchini Iran ilisema kuwa maafisa sita wamekamtwa kutokana na tukio hilo.
Iran mara kadhaa imechelewa kutoa kifaa kinachonakili safari ya ndege "black box", ambayo ina data muhimu na mawasiliano ya marubani. Inatarajiwa kutuma kifaa hicho nchini Ufaransa kwa uchunguzi zaidi Julai 20, kwa mujibu wa shirika la habari la Iran IRNA.
Kumekuwa na maswali kadha wa kadha kwa nini Iran haikufunga anga zake wakati wa shambulio hilo.
Kanda ya rekodi ya sauti iliopatikana na kituo cha habari cha Canada CBC, inaashiria kuwa anga ya Iran iliachwa wazi ili kuzuia shambulio la Marekani dhidi ya nchi hiyo na pia isifichue njama ya Iran kushambulia kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq.
Rekodi hiyo inadai kuwa na mawasiliano kati ya familia ya mmoja wa wahasiriwa wa ajali hiyo na Hassan Rezaeifar, ambaye wakayi huo alikuwa anaongoza uchunguzi wa Iran kuhusiana na ajali hiyo.
Naibu wa Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Mohsen Baharvand amepuuzilia mbali rekodi hiyo, akisema haiwezi kutumiwa kama ushahidi