Maadhimisho ya miaka 10 ya mashambilio ya kigaidi Kampala

Miaka 10 ya mashambilio ya kigaidi Kampala
Maelezo ya picha, Miaka 10 ya mashambilio ya kigaidi Kampala
    • Author, Issaac Mumena
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Imetimu miaka kumi tangu kufanyika kwa mashambulizi ya mabomu mji wa Kampala ambapo mashabiki waliokuwa wakitazama fainali za kombe la dunia walinaswa katika tanzia hiyo.

Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 70 na kuwacha wengine wengi na majeraha.

Manusura hao hadi mpaka sasa wanakumbuka kisa hicho kama ambacho kilitokea jana.

Na baadhi yao hawataki tena kuangalia michezo kwenye mikusanyiko, amesema mwandishi wa BBC Issaac Mumena.

Miaka 10 ya mashambilio ya kigaidi kampala
Maelezo ya picha, Baadhi ya walionusurika shambulio hawataki hata kuangalia tena michezo kwenye mikusanyiko

Ilikuwa siku kama ya leo tarehe 11 mwezi wa Julai wakati mamia ya mashabiki wa soka nchini Uganda walifurika kwenye uwanja wa raga wa Kyadondo mjini Kampala kutazama mechi ya fainali ya kombe la dunia iliyochezwa uwanja wa Soccer City mjini Johnnesburg, kati ya Uhispania dhidi ya Uholanzi.

Mechi hiyo ilimazika Uhispania ikitwaa taji hilo baada ya kuifunga Uholanzi goli moja kwa 0.

Ilikuwa furaha kwa Wahispania lakini majonzi kwa Waganda baada ya wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab kushambulia uwanja wa Kyandondo kwa mabomu ya kujitoa muhanga pamoja na eneo la mkahama lenye raia wengi wa Ethiopia sehemu ya Kabalagala kitongoji cha jiji la Kampala, ambapo watu 70 walipoteza maisha na zaidi ya wengine 70 kujeruhiwa.

Aidadi Athumani ni mmoja wa manusura wa siku hiyo:

''Nakumbuka wakati huo tulikuwa tukiangalia fainali ya kombe la dunia kati ya Uhispania dhidi ya uholanzi, mimi nikishabikia Uholanzi ndipo yakotea mashambulizi ya mabomu na mimi nikiwa mmoja wapo waliopata madhara na raia wengine wa Uganda.''

Aidadi ni mwalimu wa shule moja ya upili ya wilaya ya Mukono kilomita 30 kutoka mjini Kampala anasema tangu tukio hilo maisha yake yamebadilika hata utendaji kazi wake.

Aidha, Aidadi ni shabiki mkubwa wa soka na ni shabiki wa timu ya Arsenal, lakini shambulio la mwaka 2010 limepunguza ushabiki wake.

''Majeraha ya mabomu bado yananisumbuwa, wakati wa baridi nasikia maumivu kwenye makovu, changamoto nyingine ni maumivu ya kichwa na wakati nafundisha watoto darasani inabidi niketi badala ya kusimama kama ilivyokuwa zamani, na siwezi kuchukuwa muda mwingi kufundisha,'' Aidadi amesema.

Licha ya Aidadi kuogopa mikusanyiko ya watu, uongozi wa uwanja wa raga wa Kyadondo ulipata fundisho kubwa kutokana na shambulio la mwaka 2010, na kuongeza ulinzi zaidi katika uwanja huo.

''Kabla ya janga la Covid-19 mashabiki waliendelea kutazama michezo mbali mbali nyakati za usiku na walikuwa wanajitokeza kwa wingi bila kuogopa. Watu walikuwa wamerudi katika uwanja wa Kyadondo, wamesahau yaliyotokea miaka 10 iliyopita. Na pia tumeongeza ulinzi hapa Kyadondo, tuna kituo cha polisi ambao wanafanya kazi saa 24, na tumekuwa tukiandaa michezo ya usiku ya raga na watu wanajaa, kwa hiyo maisha yamerudi kama ilivyolkuwa zamani kabla ya shambulio la mwaka 2010'', amesema Tolbert Onyango mwenyekiti wa klabu hiyo.

Shambulio la kigaidi la mwaka 2010 lilileta fundisho kubwa kwa vikosi vya ulinzi nchini Uganda ambapo kikosi maalum cha kupambana na ugaidi kilianzishwa.

Na licha ya kuwepo vitisho vingi vya magaidi kushambulia Uganda jeshi la UPDF limeweza kudhibiti vyema na magaidi kushindwa kufanya mashambulizi waliokusudia.