Tundu Lissu asema atarejea Tanzania Julai 28

Iliyochapishwa

Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu amesema anatarajia kurudi nchini humo Julai 28.

Lissu ametangaza nia ya kugombea urais kupitia chama chake cha CHADEMA Oktoba mwaka huu. Mwanasiasa huyo kwa sasa yuko ughaibuni ambapo alienda kupata matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017.

Akizungumza leo katika mkutano unaoendelea kwa njia ya mtandao ulioandaliwa na taasisi ya The Resistance Bureau, Lissu amesema ameshakata tiketi ya ndege na watanzania watarajie kumpokea Julai 28.

Mjadala huo umewahusisha viongozi kadhaa wa upinzani na wanaharakati mbalimbali wa Afrika, washiriki wa Afrika Mashariki wakiwa Bobi Wine mpinzani kutoka nchini Uganda na Tundu Lissu wa Tanzania

Akijibu swali kuhusu kama anahofu kuwa anaweza kuzuiwa kuingia nchini mwake, Lisu amesema: ''Sina sababu ya kuamini kuwa nitazuiwa kurudi nyumbani, mimi si mhalifu niliondoka nje ya Tanzania nikiwa sina fahamu, nilishambuliwa kwa risasi mara 16 na watu ambao mpaka sasa hawajakamatwa.''

''Hivyo ninarejea nyumbani kuikabili serikali iliyosema kuwa haina hatia katika tukio hilo la jaribio la kuniua, kunizuia kutadhihirishia dunia kuwa ilihusika na shambulio la mwaka 2017 kama nilivyosema sina sababu ya kuamini kuwa nitazuiwa kurejea nyumbani''. Alieleza Lissu kwenye mkutano huo.

Juma lililopita Lissu aliwakilishwa na Wakala wake David Djumbe kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama cha CHADEMA kuwania nafasi ya urais.

Akizungumza kwa njia ya mitandao akiwa ughaibuni, Lissu alitangaza nia ya kuwania urais nchini Tanzania, uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2020.

Lissu alitangaza nia hiyo akiwa ughaibuni ambako alipelekwa miaka takribani mitatu iliyopita baada ya kushambuliwa vibaya kwa risasi na watu wasiojulikana.

''Sasa ninapenda kuwataarifu rasmi kwamba nimetangaza rasmi nia yangu ya kugombea nafasi ya urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.Tayari nimeshawasilisha taarifa rasmi ya kutangaza nia hiyo kwa katibu mkuu wa chama chetu kama iliyoelekezwa kwenye maelekezo yake kwa wanachama wa chama chetu.'' Alisema