Afisa wa anga wa shirika la anga za mbali la Urusi akamatwa kwa uhaini

Chanzo cha picha, Image copyrightFACEBOOK.COM/ISAFRONOV
Shirika la anga za mbali la Urusi Roskosmos limesema katika taarifa yake iliyoandikwa kwa Kirusi kwamba kukamatwa kwa mwandishi wa zamani wa habari, Ivan Safranov hakuhusiani na kazi anayoifanya kwa sasa katika shirika hilo.
Huduma za usalama za Urusi FSB zimesema kuwa anashukiwa kufanyia upelelezi nchi mwanachama wa muungano wa Nato, limesema shirika la habari la Urusi- Ria.
Safronov aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa masuala ya kijeshi katika magazeti ya kila siku ya taarifa za biashara ya Kommersant na Vedomosti.
Hatahivyo, msemaji wa serikali ya Urusi mjini Kremlin Dmitry Peskov ameiambia BBC kuwa: "Kulingana na taarifa tunazozifahamu kukamatwa kwake hakuhusiani na shughuli zake za awali kama mwandishi wa habari kwa namna yoyote ."
Safronov alijiunga na Shirika la Urusi la anga za mbali Roskosmos kama mshauri wa masuala ya habari wa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Dmitry Rogozin katikati ya mwezi Mei.
Shirika la anga za mbali limesema linawasaidia wachunguzi kupata majibu ya maswali yao.
Mwandishi huyo wa zamani wa habari anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela iwapo atapatikana na hatia.
Ria ilinukuu taarifa ya huduma za usalama FSB ikisema Safronov anaaminiwa kuwa aliwahi kufanyia kazi huduma za usalama za nchi mwanachama wa Nato ambayo haikutajwa .
"Alikusanya na kutuma kwa wawakilishi wake taarifa kuhusu ushirikiano wa kiufundi wa jeshi, ulinzi na usalama wa Shirikisho la Urusi ," ilisema.
Shirika la habari la Interfax lilinukuu vyanzo vya FSB vikisema Bwana Safronov aliitwa kuhojiwa na maafisa wa FSB mwaka mmoja uliopita lakini hakukua na ushahidi wa mashitaka ya uhalifu wakati huo.
Hatahivyo, mwezi Juni 2019, vikao vya mahakama vilifanyika juu ya madai ya kufichuliwa kwa taarifa za siri za taifa na gazeti la kila siku la Kommersant .
Taarifa hizo ziliripotiwa kuwa zilitokana na taarifa aliyoandikwa kwa ushirikiano wa Safronov kuhusu namna Urusi ilivyotoa ndege ya kivita ya jet - Su-35 kwa nchi za Misri na Iran. Ripoti hiyo baadae iliondolewa kutoka kwenye tovuti wa gazeti la Kommersant..
Wakati kesi ilipokuwa ikiendeshwa mahakamani, Safronov alikuwa amefutwa kazi na gazeti kutokana na taarifa aliyokua ameiandika iliyosema kuwa Spika wa Bunge la seneti la Urusi Valentina Matviyenko alikua karibu kuondoka madarakani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kitengo chote cha siasa cha Gazeti hilo kilijiuzulu kupinga kufutwa kazi kwa Safronov.
Baba yake Safronov, anayeitwa Ivan, pia alifahamika sana kama mwandishi wa taarifa za maoni juu ya jeshi katika gazeti la Kommersant.
Alifariki baada ya kuanguka kutoka kwenye makazi yake yaliyokua katika ghorofa ya tano mwaka 2007.
Ivan Safronov alikua akichunguza madai ya mauzo yaliyopangwa ya silaha za Urusi kwa Syria na Iran wakati alipokufa, lilisema gazeti la ,Kommersant.
Roskosmos ni nini?
Roskosmos ni Shirika la shughuli za anga la taifa la Urusi- (State Corporation for Space Activities), na lilipata hadhi hiyo mwaka 2015 kama shirika linalohusika na safari mbalimbali na mipango ya anga.
Bwana Rogozin, mwanasiasa mwenye utata, alichukua uongozi wa shirika hilo mwezi Mei 2018.
Lakini limekua likikumbwa na matatizo. Ajali iliyotokea baadae mwaka 2018 ilisababisha kusitishwa kwa safari ya roketi ya Soyuz iliyokuwa imepangwa kuelekea Kituo cha kimkataifa cha anga za mbali.
Kabla tu ya tukio hilo, mhudumu wa ISS alikuwa amegundua shimo la ajabu.
Mwaka uliofuata, mradi wa anga za mbali wa Rais Vladimir , ulitiwa doa kwa kashfa wakati maafisa wa ngazi ya juu walipofungwa kwa makosa ya wizi na ufisadi.












