Shirika la kutetea haki za wanyama Thailand lalalama kuhusu utumizi mbaya wa tumbili

Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya maduka ya jumla yameondoa maji ya nazi pamoja na mafuta yake madukani baada ya kubainika kwamba bidhaa hizo zimekuwa zikitengenezwa kutokana na nazi zinazotundwa na tumbili.
Tumbili hao huchukuliwa msituni na kufunzwa jinsi ya kutunda zaidi ya nazi 1,000 kwa siku, maafisa wanaohusika na kuzuia unyanyasaji wa wanyama wamesema.
Kundi hilo linalotetea haki za wanyama limesema kwamba tumbili hao hutumika kama mashine za kutunda nazi nchini Thailand.
Zikijibu kampuni za Waitrose, Ocado, Co-op na Boots zimeapa kusitisha uuzaji wa bidhaa hizo.
Wakati huohuo, Duka la jumla la Morissons limesema kwamba tayari limeondoa bidhaa zinazotengenezwa kutokana na nazi zilizotundwa na tumbili.
Katika taarifa yake, Waitrose imesema kwamba : kama sera yetu ya kuwalinda wanyama tumeapa kutouza bidhaa yoyote inayotokana na unyanyasaji wa tumbili. Co-op ilisema: Kama muuzaji anayefuata maadili, haturuhusu utumizi wa tumbili kuwa chanzo cha bidhaa tunazouza.
Katika ujumbe wa twitter mapema siku ya Ijumaa , mchumba wa waziri mkuu Carrie Symonds muhafidhina, alitoa wito kwa maduka yote ya jumla kutonunua bidhaa hizo.
Duka la jumla la Sinsubury liliambia BBC kwamba: tunafikiria viwango vyetu na kuchunguza tatizo hili na wanaotuuzia bidhaa.
Nazi 1000 kwa siku
Shirika hilo la kutetea maslahi ya wanyama Peta lilisema kwamba limefanikiwa kupata kampuni nane nchini Thailand ambazo hutumia tumbili kutunda nazi kwa uuzaji wa kigeni kote duniani.
Tumbili wanaume huweza kutunda hadi nazi 1000 kwa siku , Peta imesema huku ikidaiwa kwamba mwanadamu anaweza kutunda nazi 80 pekee kwa siku.
Pia shirika hilo liligundua shule za tumbili ambapo wanyama hao hufunzwa kutunda nazi mbali na kupeleka baiskeli ama hata kucheza mpira wa vikapu ili kuwafurahisha watalii.
''Wanyama katika vituo hivyo - wengi wao wakiwa wamechukuliwa msituni kinyume na sheria wamekuwa wakionyesha tabia tofauti inayoashiria kwamba wanateseka'', ilisema Peta

Chanzo cha picha, Getty Images
"Tumbili walifungwa katika matairi yaliochakaa ama hata kuwekwa ndani ya ngome ili kuwazuia kutotoroka huku tumbili mmoja aliyekuwa akipiga kelele akijaribu kumtoroka aliyekuwa anatembea naye''.
Katika kisa kimoja , shirika hilo liliambiwa kwamba baadhi ya meno ya wanyama hao yatatolewa iwapo watajaribu kuwauma wamiliki wao.
''Wanyama hawa walio na akili nyingi wananyimwa vitu vinavyowachochea kunoa bongo zao, uhuru, na kila kitu ambacho kitafanya maisha yao kuwa bora, lakini kwa lengo la kuwatumia kutunda nazi'', alisema mkurugenzi wa Peta Elisa Allen.
Peta inawataka watu walio na maadili mema kuzuia utumiaji mbaya wa tumbili kwa kukana bidhaa zinazotokana na kutundwa kwa nazi kutoka Thailand












