Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Je ni habari gani hizi zinazotoa matumaini kuhusu tiba ya corona?
Ni miezi mitatu tangu shirika la afya duniani WHO kutangaza kwamba kusambaa kwa virusi vya Covid-19 kumesababisha janga.
Ilikuwa tarehe 11 mwezi Machi na tangu wakati huo tafiti chungu nzima zimezinduliwa kuhusu tiba ya ugonjwa huo.
Ukweli ni kwamba tayari hatua kubwa zimeafikiwa katika utafutaji wa tiba ya maradhi hayo.
Maabara zilizopo katika mataifa tofauti duniani zimeanza kuchunguza takriban tiba 150.
Baadhi yake tayari zilikua zikiuzwa katika maduka ya dawa na sasa zinafanyiwa vipimo iwapo zinaweza kutibu ugonjwa huo.
WHO imekuwa ikizifanyia majaribio dawa zinazoleta matumaini kwa mgonjwa.
- Uingereza inasema kwamba majaribio yake kwa jina Recovery ndio makubwa zaidi duniani. Zaidi ya wagonjwa 11,000 wameshiriki katika utafiti huo.
- Mojawapo ya dawa zinazofanyiwa utafiti dexamethasone , imeonesha kusaidia maisha ya wagonjwa wa corona walio katika hali mahututi .
- Vituo kadhaa vya utafiti vinajaribu kutumia damu ya wagonjwa waliopona virusi hivyo vya corona kutafuta dawa..
Hatua tatu zinazochunguzwa:
- Dawa za kukabiliana na HIV ambazo huathiri uwezo wa Covid-19 kuzaana mwilini.
- Dawa zinazoweza kudhibiti utendakazi wa kinga ya mwili. Wagonjwa huwa katika hali mahututi wakati kinga yao inapoanza kutumia nguvu zaidi hatua inayofanya uharibifu mwilini.
- Mfumo wa kinga ya mwili kutoka kwa damu ya mtu aliyepona corona ama katika maabara ili kuweza kushambulia virusi vya corona.
Je ni dawa gani zinazoleta matumaini?
Dexamethasone, dawa ya kwanza ambayo imeonekana kuokoa maisha ya watu walio na Covid-19 imebainika kuwa hatua kubwa katika vita dhidi ya corona.
Vipimo vya mapema vimeonesha kwamba dawa hiyo ya bei nafuu hupunguza hatari ya kifo kwa thuluthi moja miongoni mwa wagonjwa ambao wanahitaji mashine za kuwasaidia kupumua na moja kwa tano miongoni mwa wagonjwa ambao wanalazimika kutumia oksijeni.
Maambukizi ya virusi vya corona husababisha uvimbe mwilini wakati kinga inapojaribu kukabiliana navyo.
Hali hiyo inaweza kusababisha mfumo wa kinga mwilini ulio dhabiti na ni utendaji huo ambao unaweza kusababisha madhara makubwa kwa mgonjwa.
Dawa ya Dexamethasone hukabiliana na tatizo hilo.
Remdesivir
Majaribio ya dawa ya remdesivir, inayotumika kutibu virusi vya ukimwi, pia yameonesha matumaini .
Dawa hiyo ilitengenezwa kwa lengo la kutibu Ebola. Majaribio yaliofanywa nchini Marekani miongoni mwa zaidi ya watu 1,000 duniani yamebaini kwamba remdesvir ilipunguza muda wa dalili kujitokeza kutoka siku 15 hadi siku 11.
Katika utafiti huo, baadhi ya wagonjwa walipewa tiba hiyo huku wengine wakipokea dawa kama hiyo lakini bandia.
Ni mojawapo ya dawa nne katika majaribo hayo ya WHO na mtengenezaji wake Gilead pia anafanya majaribio.
Hatahivyo huku remdesvir ikiwa inaweza kusaidia mtu kupona na hata kuzuia watu kutibiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, tafiti kufikia sasa hazijatoa ishara zozote kwamba inaweza kutibu virusi vya corona.
Dawa za kukabiliana na virusi vya HIV zinadaiwa kuwa na uwezo mkubwa katika awamu za kwanza za ugonjwa na kuzuia utendakazi wa dawa hizo wakati ugonjwa huo upo katika awamu za mwisho.
Je dawa za HIV zinaweza kukabiliana na coronavirus?
Japokuwa mengi yamesemwa kuihusu, kuna ushahidi mchache kwamba baadhi ya dawa za HIV kama vile Lopinavir na ritonavir, huenda zikawa na uwezo wa kutibu virusi vya corona.
Matokeo yake yanaonesha kwamba zinaweza kufanyakazi katika maabara lakini majaribio dhidi ya wanadamu yamekuwa na matokeo mabaya.
Mchanganyiko huo haukuimarisha hali ya mtu kuweza kupona, kupunguza idadi ya vifo ama hata kupunguza viwango vya virusi hivyo miongoni mwa wagonjwa wa corona walio katika hali mbaya.
Hatahivyo tangu majaribio hayo yafanyiwe wagonjwa walio katika hali mahututi { robo ya wagonjwa hao walifariki} Huenda maambukizi yalikuwa katika awamu ambayo dawa hizo zilishindwa kuyadhibiti.
Je dawa ya kutibu malaria inaweza kutibu virusi vya corona?
Dawa za malaria ni miongoni mwa dawa zinazofanyiwa majaribio na shirika la Afya duniani .
Chloroquine na , hydroxychloroquine zinaweza kuwa na nguvu za kukabiliana na virusi mbali na kutuliza mfumo wa kinga mwilini.
Baadhi ya watu wanaamini kwamba dawa hizo zinaweza kufanya kazi kama tiba mbadala ya corona , kutokana na madai yaliotolewa na rais wa Marekani Donald Trump , lakini kuna ushahidi mchache kuhusu uwezo wake.
Hydroxychloroquine pia hutumika kama tiba ya kutibu baridi yabisi kwasababu inasaidia kudhibiti kinga.
Majaribio ya mapema yaliofanyika katika maabara yameonesha zinaweza kukabiliana na virusi hivyo lakini kuna wasiwasi mwingi kuhusu matumizi yake dhidi ya ugonjwa huo.
Matokeo ya utafiti mwengine kutoka katika majaribio hayo ya Recovery yanayofanywa na Uingereza umebaini kwamba hydroxychloroquine haifanyi kazi kama tiba ya Covid-19 hivyobasi imeondolewa katika utafiti huo.
WHO awali ilikuwa imefutilia mbali majribio dhidi ya dawa hiyo baada ya utafiti mkubwa katika jarida la Lancet kubaini kwamba matumizi ya dawa hiyo yanaweza kusababisha matatizo ya moyo na hata kuongeza uwezekano wa mtu kufariki.
WHO inasema kwamba hakuna maelezo sahihi ya ushahidi kuhusu uwezo wake.
Je damu ya watu waliopona corona inaweza kutibu virusi hivyo?
Watu wanaopona maambukizi hupata antibodies katika damu yao, kufautia makabiliano dhidi ya virusi hivyo.
Wazo ni kuchukua eneo la damu lililo na antibodies na kumpatia mgonjwa.
Marekani tayari imefanikiwa kuwatibu wagonjwa 500 na kile kinachojulikana kama plasma na mataifa mengine pia yameanza kutumia njia hiyo.
Je itachukua muda gani kabla ya kupata tiba?
Ni mapema mno kujua ni lini tutapata tiba itakayotibu corona.
Hatahivyo katika kipindi cha miezi ijayo ni muhimu kuanza kupata matokeo ya majaribio hayo.
Ni mapema sana kujua iwapo tutapata chanjo ambayo itazuia maambukizi badala ya kuyatibu.
Hii ni kwasababu madaktari wanafanyia utafiti dawa ambazo tayari zimetengenezwa na zinajulikana kuwa salama kwa matumizi ya binadamu, huku utafiti wa kutafuta chanjo ukianza kuanzia mwanzo.
Dawa nyengine mpya za kutibu corona zinafanyiwa majaribio katika maabara, lakini haziko tayari kujaribiwa katika wanadamu.
Kwanini tunahitaji tiba?
Mojawapo ya sababu za wazi ni kwamba itaokoa maisha, lakini pia inaweza kuruhusu kuondolewa kwa amri za kutotoka nje iliowekwa katika mataifa mengi.
Uwepo wa tiba madhubuti utafanya virusi vya corona kutokuwa na athari mbaya.
Iwapo watu katika hospitali watazuiwa kufikia wakati ambapo watahitaji mashine za kupumua, kutakuwa na hatari chache za ukosefu wa vyumba vya wagonjwa mahututi kwa kuwa kutakuwa na udhibiti wa idadi ya watu watakaotumia vyumba hivyo.