Virusi vya corona: Tanzania yatoa muongozo wa ufunguzi wa shule

Chanzo cha picha, Anthony Asael/Art in All of Us
Serikali ya Tanzania imetoa mwongozo mpya wa ufunguzi wa shule, vyuo na taasisi nyengine za elimu wakati ambapo taasisi zote za elimu zimefunguliwa tena kuanzia Jumatatu Juni 29,2020.
Muongozo huo umetolewa wakati shule kuanzia za chekechea hadi sekondari zimefunguliwa na mamlaka ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutangaza kwamba ugonjwa wa Covid-19 umepungua kwa kiasi kikubwa.
Miongoni mwa miongozo ni kwamba wanafunzi chini ya umri wa miaka minane na wale wenye magonjwa ya matatizo ya kupumua kama pumu, ugonjwa wa moyo na selimundu wasivae barakoa.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema ikiwa mwanafunzi ataumwa au ana matatizo ya kupumua anastahili kuepuka maeneo yenye msongomano wa watu na kuvua barakoa ili apate hewa safi na kutafuta usaidizi.
Aliwaambia wasimamizi wa shule kuhakikisha kwamba wanafunzi hawavai barakoa wakati wanafanya mazoezi kama vile kukimbia na michezo mingine.
Waziri amesema kuwa shule zinahitajika kuwa safi pamoja na kutengwa kwa maeneo ya kunawa mikono katika maeneo ya kimkakati na wanafunzi hawastahili kubeba vitakasa mikono shuleni.
Hatua ya kufunguliwa tena kwa shule imepokelewa kwa hisia mseto, msisimko na mashaka vilevile.

Maryam Zavalla, mzazi wa mwanafunzi wa miaka mitatu, ameiambia BBC kwamba ameamua kufuatilia hali ilivyo kwanza kabla ya kumrejesha mtoto wake shuleni.
"Shule zimefunguliwa leo lakini nimewaambia wasije kumchukua leo, ana miaka mitatu tu, naona ataendelea kuwa nyumbani kwanza nikifuatilia hali inavyoendelea, pengine ataenda wiki ijayo," Bi. Zavalla amesema.
Mzazi mwengine Shafia Twahir amesema kuwa yeye ameridhika na hatu zilizochukuliwa na hivyo basi amemruhusu kijana wake wa miaka minne kurejea shuleni.
"Tumekuwa na mawasialiano ya mara kwa mara na uongozi wa shule. Leo watoto wametekeleza hatua ya kutokaribiana shuleni na hata kwenye mabasi na pia ndani ya madarasa, wanaosha mikono yao kila mara na vitakasa mikono vimewekwa kila sehemu ... lakini tutaendelea kufuatiia hali hiyo."

Chanzo cha picha, @umwalimu
Aidha, Waziri wa afya Ummy mwalimu amewataka wazazi kuwapa watoto wao barakoa za uso na kutoa taarifa ya dalili zozote za ugonjwa wa virusi vya corona kwa mamlaka ili vipimo vifanywe haraka iwezekanavyo.
Wamiliki wa mabasi ya watoto wa shule wametakiwa kutoa vitakasa mikono kwa wanafunzi kabla ya kuingia ndani ya basi huku wasimamizi wa usafiri wa umma wakitakiwa kufuata miongozi iliyotolewa.

Chanzo cha picha, BBC-Eagan Salla
Waziri aliwaambia wataalamu wa afya kufanya ukaguzi wa kila mara katika maeneo yao kuhakikisha kwamba hatua za kuzuia usambaaji wa ugonjwa wa Covid-19 unafuatwa wakati madarasa yanaendelea.
Tofauti na nchi jirani, Tanzania iliamua kutochukua hatua kali za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19. Hakuna hatua ya kutotoka nje iliyochukuliwa ingawa shule, mikusanyiko ya watu kama vile kwenye matamasha ya muziki na shughuli za michezo xilipigwa marufuku wakati nchi hiyo iliporekodi mgonjwa wa kwanza aliyepata maambukizi ya virusi vya corona katikati ya Machi.

Tofauti na nchi jirani, Tanzania iliamua kutochukua hatua kali za kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.
Hakuna hatua ya kutotoka nje iliyochukuliwa ingawa shule, mikusanyiko ya watu kama vile kwenye matamasha ya muziki na shughuli za michezo xilipigwa marufuku wakati nchi hiyo iliporekodi mgonjwa wa kwanza aliyepata maambukizi ya virusi vya corona katikati ya Machi.












