Shambulio Pakistan: Uvamizi wa kigaidi katika jengo la hisa Karachi
Wanaume wanne wenye silaha wamevamia jengo la soko la hisa Pakistan, Karachi na kusababisha vifo vya walinzi wawili na afisa wa polisi huku wengine kadhaa wakipata majeraha kabla ya wavamizi hao kuuawa kwa kupigwa risasi.
Washambuliaji hao walivamia eneo hilo la soko la hisa baada ya kurusha gurunedi kwenye lango kuu la jengo lakini maafisa wanasema kuwa walishindwakufika kwenye ghorofa ya biashara ya soko la hisa.
Wafanyakazi waliokuwa ndani ya jengo walijifungia kwenye vyumba na wengi wao wakaokolewa. Vikosi vya usalama vinaendelea kusaka eneo la tukio.
Wanamgambo kutoka kundi la Baloch Liberation Army wamekiri kutekeleza shambulio hilo.
Makundi ya Baloch yamekuwa yakipigana kwa muda mrefu yakidai kujitenga na kutaka kuwa na mgao mkubwa wa raslimali katika jimbo la Balochistan.

Chanzo cha picha, Reuters
Pakistan imekuwa ikivamiwa na wanamgambo hasa makundi ya wanamgambo wa Kiislamu lakini mashambulizi kama haya yamekuwa nadra sana miaka ya hivi karibuni.
'Walifyatulia kila mmoja risasi'
Shambulio la Jumatatu lilianza pale wanamgambo wenye silaha walio na bunduki za rishasha waliporusha gurunedi na kuanza kufyatualia eneo la usalama nje ya jengo la soko la hisa.
"Walikuja kwa kutumia gari la Corolla rangi ya fedha na wakasimamishwa na polisi nje ya lango kuu ambapo ufyatulianaji wa risasi ulianza," Jenerali inspekta wa polisi wa Sindh, Ghulam Nabi Memon amezungumza na BBC Urdu.

Chanzo cha picha, Reuters
Walinzi walijibu shambulio hilo na kuwaua wavamizi wote wanne waliokuwa wamejihami kwa silaha., mamlaka imesema.
Maafisa watatu wa polisi ni miongoni mwa saba waliojeruhia na wanaendelea kupata matibabu hospitalini.
Bwana Memon amesema wavamizi hao hawakufaulu kuingia ndani ya jengo kuu na gurunedi, vilipuzi na silaha zingine zilipatikana kutoka kwao.
Mamlaka ya jengo la soko la hisa la Pakistan imethibitisha kwamba hakuna mwanamgambo yeyote aliyeingia ndani ya jengo hilo.
Mkurugenzi wake, Abid Ali Habib, amesema wanaume hao wenye silaha waliingia kupitia eneo la kuegesha magari na kuanza kufyatulia kila mmoja risasi.
Picha za eneo la tukio zinaonesha miili wanaume wawili ikiwa imelala chini karibu na eneo lenye silaha nyingi. Haikubainika mara moja ikiwa kuna wanamgambo zaidi waliohusika na shambulio hilo na hivyo basi msako wa jengo ukaendelezwa kila sehemu na vikosi vya usalama.
Taarifa zinasema kuwa watu wengi waliokuwepo kwenye jengo la soko la hisa walifaulu kutoroka au kujificha ndani ya vyumba. Wale waliokuwepo ndani ya jengo walihamishwa eneo salama kupitia mlango wa nyuma, Runinga ya Geo imesema.
Wakati huu biashara ya soko la hisa inaendelea kama wakaida.
Jengo hilo lina ofisi nyingi za taasisi za fedha kwenye eneo lenye usalama wa hali ya juu pamoja na ofisi ambazo ni makao makuu kwa benki nyingi na biashara zingine.
Jengo hilo limesema kawaida huwa kunawafanyakazi takriban 8,000 lakini kwasababu ya janga la corona wengi wanafanyakazi kutoka nyumbani.


Kwanini makundi ya Balochi yanapigana?
The Baloch Liberation Army ni moja ya makundi ambayo yamekuwa yakitekeleza mashambulizi Pakistan.
2018, wanachana wa kundi hilo walivamia ubalozi wa China, Karachi na kusababisha vifo vya watu wanne. Wafanyakazi wote waliokuwa ndani walikuwa salama.
Mwaka jana kundi hilo lilivamia hoteli ya nyota tano katika bandari ya Gwadar huko Balochistan. Hoteli hiyo ni kitovu cha miradi ya mabilioni ya madola ya China na ililengwa ili kuvamia raia wa China na wawekezaji wengine.
Wanagambo wanaotaka kujitenga huko Balochistan wanapinga uwekezaji wa China wakidai kwamba manufaa yake kwa raia ni ya chini mno.
Awali kundi hilo lilitaka kujitenga kisiasa lakini taratibu limekuwa likigeuka na vuguvugu linatotumia silaha lenye nia ya kujitenga na kuorodheshwa kama kundila kigaidi na Pakistan, Uingereza na Marekani.













