Amy ana wiki mbili tu kupata mtu atakayempa uboho wa kufanana na yeye

Chanzo cha picha, Bartlett family
Amy Bartlett, 14, kutoka West Bridgford, karibu na Nottingham, alikuwa anakaribia kumaliza matibabu alipoarifiwa kwamba ugonjwa wa saratani anaotibiwa umerejea tena upya na anahitajika kufanyiwa upandikizaji.
Marie Bartlett, mama yake msichana amesema hilo lilimvunja moyo kabisa asijue kitakachomtokea binti yake.
Hospitali ya taifa imesema ni vigumu sana kuendesha zoezi la kupata mtu ambaye uboho wake unafafa na mgonjwa kipindi hiki kwasababu ya virusi vya corona na kufanya iwe vigumu hata zaidi kumpata mwenye uboho sawa na wake.
Amy alibainika kuwa na ugonjwa wa lukemia akiwa na umri wa miaka 12 alipoanza kulalamika kupata maumivu makali kiunoni na kwenye mbavu.
Hali yake ilifanya atambuliwe kama aliye katika hatari zaidi na kuanza kupata matibabu ya hali juu ya tiba ya kemikali inayopewa watoto wenye ugonjwa huo, Hospitali ya chuo kikuu cha Nottingham, imesema.

Chanzo cha picha, Bartlett family
Kupitia matibabu aliyokuwa anapata, alianza kuwa na matatizo ya figo, dawa za muda mrefu zikasababisha ugonjwa wa kisukari na kuanza kuwa na mzio kutoka na matibabu aliyokuwa anapokea.
Matibabu hayo yalitakiwa kumalizika Julai 4 lakini wiki mbili ziizopita familia iliarifiwa kwamba ugonjwa wa Amy umerejea tena.
Bi Bartlett amesema: "Ilinivunja moyo kabisa na kuwa na wakati mgumu kumuelezea na kumshawishi vilevile kuwa ingawa amepata matibabu hayo huenda mchakato huo ukaanza tena."
Baba yake msichana, Leigh, ameongeza: "Anajitahidi kuwa na mtazamo chanya, ni msichana shupavu, lakini sio rahisi hasa ukifikiria kwamba ni mtu wako wa karibu."
Amy ameanza tena kupata matibabu lakini bado hajafanikiwa kupata mtu mwenye uboho kama wake anayeweza kumsaidia ili afanyiwe upandikizaji.

Chanzo cha picha, Bartlett family
Pia unaweza kusoma:
Kaka yake Marcus amepimwa lakini uboho wake haufanini na wa dada yake.
"Tuna wiki mbili hadi tatu tu za kumpata mwenye uboho unaofanana na wa Amy, kwahiyo kufikia sasa muda ni kitu cha msingi sana kwetu," Bi. Bartlett amesema.
Hospitali ya Chuo Kikuu cha Nottingham imesema kwamba mchakato wa kutafuta mtu kama kawaida hauwezi kufanyika kwasababu ya corona ingawa wanaotaka kujitolea bado wanaweza kujisajili.












