Virusi vya corona: sababu za kuwepo kwa mlipuko wa virusi kwenye viwanda vya nyama

Nyama zikiwa zimetundikwa

Chanzo cha picha, Toennies

Iliyochapishwa

Mamia ya wafanyakazi wamepatikana na virusi vya corona katika makapuni ya kutengeneza nyama na machinjioni.

Makampuni hayo ni pamoja na mengine yenye wafanyakazi 150 ambao wameambukizwa virusi vya corona.

Kumekuwa na milipuko mikubwa Ujerumani, Ufaransa, Uhispania na Marekani.

Bev Clarkson kutoka chama cha wafanyakazi, anasema: "Chama hiki kimekuwa kikionya kila wakati kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa mlipuko wa virusi vya corona Uingereza hasa katika makampuni ya kutengeneza nyama".

Kwanini wafanyakazi wa makampuni ya nyama wanapata virusi vya corona?

Watu wanapata virusi vya corona kutokana na matone ya mate yanayoruka kutoka mdomoni ambayo yanaweza kusababisha kukohoa, kuchemua au hata aliyeambukizwa akasambaza virusi hivyo.

Maambukizi hayo huenda yakatokea baada ya kukaribiana na aliyeambukizwa au kugusa sehemu iliyopata maambukizi.

"Hususan, viwandani, maeneo ya ndani ambayo huwa ni baridi sana na yenye unyevunyevu, yana mazingira yanayopendwa na virusi vya corona na hupelekea virusi hivyo kukaa kwa muda mrefu na kusambaa," kulingana na Lawrence Young, Profesa wa masuala ya molekyuli chuo kikuu cha Warwick.

"Virusi vinavyosambazwa kwa matone yanayoruka kutoka kwa watu walioambukizwa huenda vikaendelea kusambaa kwa muda mrefu."

Jambo jingine la kuzingatiwa katika maeneo ya kazi yenye majokofu, ni mashine zinazonguruma kwa sauti ya juu, ambapo wafanyakazi wanahitajika kuzungumza kwa sauti ya juu na hilo pia huenda likaongeza usambaaji wa matone ya mate ya watu waliopata maambukizi.

Wafanyakazi katika kiwanda cha nyama ya Kuku

Chanzo cha picha, Getty Images

Vipi kuhusu mazingira ya kufanyia kazi?

Ni muhimu sana kwa wafanyakazi kuwa umbali wa mita 2 baina yao wakati wanafanya kazi katika viwanda vyenye shughuli nyingi na pia ukosefu wa jua kunaweza kusaidia virusi kuendelea kuwa hai kwa muda mrefu zaidi.

"Wakati watu wanakaribiana wakiwa wanafanya kazi kwasababu bila shaka hii ni kazi ngumu, huku wakiwa wanahema kwa nguvu, kuna uwezekano mkubwa wa kusambaa kwa virusi kutoka kwa mtu mmoja aliyeambukizwa hadi kwa wengi walio karibu nae," amesema Tara Smith, Profesa wa masuala ya kuambukizwa chuo kikuu cha Kent, Ohio.

Hata hivyo hakuna ushahidi unaoonesha kwamba bidhaa za nyama zinaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 viwandani.

Shirika la kudumisha viwango vya chakula limesema kuna uwezekano mdogo wa kupata virusi vya corona kutoka kwa vyakula kwasababu ugonjwa huo hausambazwi kwa njia hiyo.

Kiwanda cha nyama

Chanzo cha picha, Toennies

Sio tu hali ilivyo ndani ya viwanda ambayo inaweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya corona.

"Baadhi ya viwanda hivi vina makazi karibu na wakati mwengine chumba kimoja ni makazi kwa wafanyakazi kadhaa. Pia inawezekana wafanyakazi wanasafirishwa kwa basi hadi maeneo ya kufanyakazi, na watakuwa pamoja kwa siku nzima," amesema Michael Head, mtafiti mwandamizi wa masuala ya afya katika chuo cha Southampton.

Chama cha wafanyakazi kinasema kwamba ingawa kinawakilisha wengi katika makampuni ya kutengeneza nyama, mara nyingi wafanyakazi wa viwanda hivyo ni raia wa kigeni ambao huenda hawana likizo mtu anapokuwa mgonjwa, hivyobasi kuna uwezekano akakosa pesa zinazomwezesha kujikimu wakati anajitenga nyumbani baada ya kuugua.

Chama hicho kinasema mara nyingi huwa hawazungumzi Kiingereza kama lugha yao rasmi na wana wasiwasi wa kupoteza ajira zao, na hilo linawafanya kunyamaza hata wanapokuwa wagonjwa.

Kipi kinafanywa kulinda wafanyakazi?

Serikali imetoa mwongozo wa kuwa na mazingira salama ya kufanya kazi katika makampuni ya kutengeneza vyakula ikiwemo kutokaribiana kwa angalau umbali wa mita mbili.

Lakini pia kuna miongozo ya usafi viwandani wa mara kwa mara tofauti na hali ya kawaida, kutenga wafanyakazi wanaoonesha dalili na uwepo wa muda wa kuanza na kupumzika vilevile.

Pia kuna mapendekezo ya uvaaji wa mavazi ya kujikinga na virusi - na wafanyakazi wa makampuni ya kuuza nyama huvaa nguo hizo ingawa mara nyingi hawana barakoa.

Dkt. Yvonne Doyle, mkurugenzi wa wizara ya afya, amethibitisha kuwa wamearifiwa milipuko ya corona katika viwanda kadhaa vingine vikiwa ni vya kutengeneza nyama.

"Milipuko inapotokea, tunafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Afya kupima na kufuatilia waliopata maambukizi pamoja na kuhakikisha tunapata waliokaribiana nao, ndani na nje ya kampuni."

Nchini Ujerumani, serikali imepiga marufuku wafanyakazi kutoka nje - badala yake wanaoruhusiwa ni wafanyakazi walioajiriwa na kampuni pekee.

Aidha, ripoti kutoka Kituo cha Kudhibiti Magonjwa Marekani kimependekeza kupunguza kiwango cha uzalishaji, kuweka vizuizi vya kutenganisha watu, ni lazima kwa kila mmoja kuvaa mavazi ya kumkinga uso na kuhakikisha kwamba hakuna atakayekosa kulipwa kwasababu ya kujitenga.