Virusi vya corona: Kuna tahadhari kwamba maelfu ya watu huenda wakapata matatizo ya mapafu

Chanzo cha picha, ANTHONY MCHUGH
Maelfu ya watu watahitajika kurejea hospitali baada ya janga la ugonjwa wa Covid-19 kuangaliwa ikiwa mapafu yao yameathirika, madaktari wamezungumza na BBC.
Wataalamu wana wasiwasi kuwa kiasi kikubwa cha watu huenda wakapata matatizo ya kufura kwa mapafu.
Tatizo hili halina tiba na dalili zake ni pomoja na matatizo ya kupumua, kukohoa na uchovu.
Uingereza imesema inafungua vituo ambavyo watu wanaweza kupata ushauri wa wataalamu baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Dereva wa taxi aliyestaafu, Anthony McHugh, 68, alilazwa hospitali Machi 6, akiwa na dalili za virusi vya corona. Hali yake iliendelea kuwa mbaya na kuhamishwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ambapo aliwekwa mashine ya kusaidia kupumua kwa siku 13.
"Nilikuwa naishiwa na pumzi, kisha nikakimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi zaidi ya hapo hakuna ninachoweza kukumbuka," anasema.
'Ni mwenye bahati kuwa hai'
Bwana McHugh, kutoka hospitali ya Hertfordshire, alikuwa hospitali kwa wiki nne na wiki zingine mbili akawa kwenye eneo lililotengwa ambapo wagonjwa wanaweza kuendelea kupata usaidizi wakiwa wanapata nafuu.
Alirejea nyumbani katikati ya Aprili lakini miezi miwili baadae bado alikuwa na matatizo ya kupumua.
"Ni kazi ndogo ndogo tu kama kupanda ngazi akiwa anaelekea chumbani na kumwagilia maua maji. Lakini mgongo wangu ukaanza kupinda hadi ikabidi niache," anasema.
Picha zilizopigwa alipokuwa hospitali zilionesha mfano wa ukungu uliotanda kwenye mapafu dalili ya ugonjwa wa virusi vya corona.
Mapafu ya Tony kabla na baada ya kuugua ugonjwa wa Covid-19.

Chanzo cha picha, ANTHONY MCHUGH
Katika visa kadhaa inasemekana kwamba virusi vya corona vinaweza vinakabilina na kinga ya mwili ambayo inaweza kusababisha mtu kuwa na kamasi, majimaji na seli zingine kujaza vifuko vya hewa. Hilo linapotokea, nimonia au homa ya mapafu inaweza kujitokeza na kufanya iwe vigumu mtu kupumua bila usaidizi.
Picha ya eksirei ya mapafu ya Bwana McHugh aliyopigwa wiki sita baada ya kuondoka hospitali ilionesha mistari miembamba meupe, ambayo inaweza kuchukuliwa kama dalili za awali za kufura kwa mapafu.
'Wasiwasi uliopo'
"Kwa hali kama hizi, kwa sasa hakuna tunachoweza kusema kwa uhakika," amesema Dkt. Sam Hare, mtaalamu wa picha za X-ray.
"Lakini kawaida kama utakuwa na virusi au maambukizi kwa wiki sita, matokeo ya eksirei yanatakiwa kuonesha kwamba mgonjwa ameshapona."
Lakini kama wagonjwa wengine wa Covid-19 ambao wameruhusiwa kuondoka hospitalini, Bwana McHugh atahitajika kupigwa picha nyengine ya eksirei baada ya wiki 12 kuangaliwa ikiwa ukungu uliokuwa umejitokeza kwenye mapafu, umepungua.
Uvimbe kwenye mapafu ni nini?
- Huu ni ugonjwa unaotokea wakati sehemu za mapafu zimeathirika na kupata ukungu.
- Tishu nzito zinafanya iwe vigumu kwa vifuko vya hewa kufanya kazi ipasavyo.
- Wakati mwingine, hili linaweza kusababisha matatizo ya kupumua na uchovu, pamoja na mgonjwa kuwa katika hatari ya kupata maambukizi mengine ya mapafu siku zijazo.
- Ni hali ambayo haiwezi kubadilika na wakati mwingine ni yenye kuendelea hivyo basi ni sawa na kusema kwamba hali hii huendelea kuwa mbaya kadiri muda unavyosonga mbele.
Utafiti kuhusu kuathirika kwa mapafu kunakosababishwa na virusi vya corona bado uko hatua za awali.
Inadhaniwa kwamba wenye dalili za wastani za ugonjwa huo hawako katika hatari ya kupata maambukizi. Lakini wale walio hospitali hasa waliolazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi au waliopata maambukizi makali, wako katika hatari ya kuathirika.
Utafiti nchini China, uliochapishwa Machi, wagonjwa 66 kati ya 70 bado walikuwa wanaonesha kwamba mapafu yao yameathirika hata baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali.
Wataalamu wa picha za eksirei wanasema, kulingana na matokeo ya wagonjwa wa awali, kuna wasiwasi kwamba huenda wagonjwa waliopata maambukizi makali wakawa na athari za muda mrefu.
"Kwa picha zilizopigwa wagonjwa baada ya wiki sita, hadi kufikia sasa naweza kusema asilimia 20 hadi 30 ya wagonjwa ambao wamekuwa hospitali zinaonesha dalili za awali za mapafu kuathirika," amesema Dkt. Hare, aliyesaidia kwenye kuanda mwongozo wa namna ya kubaini wagonjwa wa Covid-19.
Utafiti wa kina za ugonjwa wa virusi vya corona uliotokea awali wa Sars na Mers, ulibaini kuwa asilimia 20 hadi 60 ya wagonjwa walikuwa na matatizo ya afya pamoja na kuvimba kwa mapafu.
Wakati ambapo dunia ilifanikiwa kukabili milipuko hiyo ya awali, virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 vimesambaa kote duniani huku hadi kufikia sasa maambukizi zaidi ya milioni 8 yakithibitishwa.
Zaidi ya wagonjwa 100,000 wamelazimika kupata matibabu hospitali kwasababu ya ugonjwa wa Covid-19 nchini Uingereza tangu kuanza kwa janga hilo Februari, kulingana na takwimu za wizara.
"Wasiwasi wangu na ugonjwa wa Covid-19 ni kwasababu idadi kubwa ya watu wamepata maambukizi," amesema Dkt. Hare.
"Nina wasiwasi na idadi kubwa ya watu ambao tutahitajika kuwapa matibabu, kwasababu wengi zaidi wamepata maambukizi ya virusi vya corona."
Uvimbe kwenye mapafu ni ugonjwa ambao hauwezi kutibika kwasababu ukungu uliotanda kwenye mapafu hauondoki. Lakini dawa mpya zimeanza kupunguza kasi ya ugonjwa huo na hata kuusitisha kabisha iwapo utagundulika mapema.
"Tunahitajika kufahamu ukubwa wa tatizo na wakati muafaka wa kuingilia kati ili kuanza kutoa matibabu," amesema Profesa Gisli Jenkins, wa Taasisi ya Afya ya Taifa, anayefuatilia waliopona ugonjwa wa Covid-19 na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Profesa Jenkins, mwenye makao yake Nottingham, amesema: "Wasiwasi wangu katika maisha yangu yote hatujawahi kuwa na watu wengi wenye matatizo ya mapafu kwa wakati mmoja."

Chanzo cha picha, ANTHONY MCHUGH












