Virusi vya corona: Brazil ni nchi ya pili iliyopitisha vifo 50,000

Raia wa Brazil wakisubiri kupata huduma katika hospitali ya Atalia do Norte, Brazil, 20 June 2020

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Raia wa Brazil wakisubiri kupata huduma katika hospitali ya Atalia do Norte
Iliyochapishwa

Brazil imekuwa nchi ya pili, baada ya Marekani, kuandikisha zaidi ya vifo 50,000 kutokana na virusi vya Corona.

Wizara ya Afya nchini humo inasema jana pekee, wagonjwa 641 walifariki, huku viwango vya maambukizi ya ugonjwa huo vikiongezeka hadi milioni moja kufikia wikendi.

Wataalamu wameonya kuwa kilele cha maambukizi nchini Brazil bado hakijafikiwa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limerekodi ongezeko kubwa zaidi la maambukizi ya ugonjwa huo kwa siku, huku Amerika kusini ikiwa na idadi ya juu zaidi ya maambukizi mapya.

Kati ya visa vipya 183,000 vya maambukizi yaliyoripotiwa katika kipindi cha saa 24, zaidi ya asilimia 60 ni kutokea Kaskazini na Kusini mwa America, shirika hilo lilisema.

Licha ya kuongezeko kwa mlipuko wa virusi, maelfu ya wafuasi wa rais wa Brazil Jair Bolsonaro wameshiriki maandamano sambamba na mahasimu wao siku ya Jumapili

Maandamano dhidi ya serikali yanashinikiza Bwana Bolsonaro aondolewe madarakani.

Wafuasi wake wanasema Bunge la Congress na mahakama ya juu zaidi inajaribu kudhibiti uwezo wake .

Waandamanaji wanaopinga serikali walikusanyika katika miji tofauti kikiwemo São Paulo

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Waandamanaji wanaopinga serikali walikusanyika katika miji tofauti kikiwemo São Paulo

Rais Bolsonaro amekosolewa vikali kutokana na jinsi anavyoshughulikia mlipuko wa virusi vya corona nchini humo.

Amepinga hatua ya kuweka amri ya kutotoka nje na kutofautiana hadharani na ushauri wa wizara yake ya afya.

Siku ya Jumapili, wizara hiyo ilitangaza vifo zaidi ya 641 vilivyorekodiwa katika kipindi cha saa 24, na kufikisha 50,617.

Pia nchi hiyo ilithibitisha maambukizi mapya zaidi ya 17,000 katika kipindi sawia na hicho.

Ni Marekani pekee iliyo na idadi ya juu zaidi ya maambukizi, ikiwa na jumla ya watu milioni 2.2 walioambukizwa huku watu 120,000 wakifariki.

Bw. Bolsonaro anadai kuwa athari za kiuchumi itakuwa mbaya zaidi kuliko maambukizi ya virusi vyenyewe, hoja ambayo inaungwa mkono na wengi. Lakini hatua yake imesababisha mawaziri wawili wa Afya kujiuzulu.

Wafuasi wa rais Jair Bolsonaro pia waliandamana katika barabara za mji wa São Paulo

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wafuasi wa rais Jair Bolsonaro pia waliandamana katika barabara za mji wa São Paulo

Brazil kwa sasa ina jumla ya wagonjwa milioni moja wa corona huku watu 50,000 wakifariki kutokana na ugonjwa huo.

Licha ya hayo rais hajatilia maanani haja ya kuchukua usukani katika kudhibiti maambukizi huku baadhi ya raia wake wakihisi kuwa hakuna uongozi dhabiti.

Wizara ya afya haina waziri baada ya mmoja kati ya wawili waliokuwepo kufutwa kazi na mwenginekujiuzulu mwenyewe chini ya mwezi mmoja.

Je ni nani atakaye tatua shida iliyopo Brazil - huku wengi wakiwa hawana matumaini na utawala wa Bosonaro?

Coronavirus
Banner