Asteria Mabirika, mwanamke aliyeachika kutokana na ''kunuka mkojo''

Chanzo cha picha, AMref health
Asteria alitengana na baadhi ya ndugu na familia kwasababu ya tatizo lake la Fistula ya uzazi na kuachika kwenye ndoa zaidi ya nne kutokana na ''kunuka mikojo''.
''Nilipata ugonjwa huu baada ya mimba yangu ya pili, mkunga aliyenizalisha hakuwa hata na mpira wa kujikinga mkononi, na mtoto aligoma kutoka, akalazimika kumvuta na kumtoa na mikono''
Asteria Mabirika kutoka moja ya kijiji mkoa wa Mwanza, anasema kuwa amelazimika kuishi na ugonjwa huu kwa muda mrefu kutokana na kukosa uelewa wa kujua kuwa anaweza kupona kwa kwenda kushughulikia tatizo lake kwenye kituo cha afya.
''Nilikaa siku chache baada ya kujifungua mtoto ambaye alifariki, kisha nikaanza kuona mkojo unatoka bila kujiuzuia, nikashangaa nini hiki? Mama na baba wakasema nipelekwe kwa mganga nikaaguliwe''
Kuolewa na waganga wa jadi.
Kutokana na tatizo lake Asteria alikua akienda kwa waganga wa vijiji mbalimbali ili waweze kumsaidia, Mganga wa kwanza baada ya kushindwa kumtibu akaamua kumuoa, na kuishi nae.
''Alinioa baada ya kuona kuwa siponi, akanipatia ujauzito, nikazaa vizuri tu lakini baada ya muda akaanza kuwa anaondoka nyumbani kwa muda kisha anarudi, baadae akaniambia hawezi kuendelea na mimi kwakua nanuka na siponi'' anasema Asteria.
Alikutana na mganga mwingine ambae pia ilikua hivyo hivyo, kisha akakutana na wanaume wengine ambao pia walimuacha kwakua ananuka.
''Kuna mwingine alikuja nyumbani kwetu, akanioa na tukaishi nae hapa nyumbani kwa zaidi ya miaka minne, lakini baadae nae akaanza kuwa na wanawake wengine, na kuniambia kuwa siponi, nikamwambia nenda'' anasema Asteria.

Chanzo cha picha, AMref health
Kufunga biashara yake
Asteria kabla ya kupata Fistula ya uzazi anasema kuwa alikua na biashara ya duka pamoja na hoteli akiuza chakula, lakini baada ya kupata ugonjwa huu, mambo yakabadilika.
''Nilikua na duka, nauza sabuni, sukari, na pia na hoteli napika pika, lakini baadae sasa wakaanza kusema kuwa nanuka, ikabibidi nifunge duka nikaacha sasa kufanya shughuli yoyote nikawa hapa nyumbani.'' anasema Asteria.
Baada ya kuona anatengwa kutokana na hali yake akaamua kufanya shughuli nyingine ambayo ni kuimba na kucheza kwenye mikusanyiko.
Asteria anasema baadhi ya watu kijijini kwao walikua wakifurahia jinsi anavyocheza na kuimba lakini wengine walikua wakitema mate na kusema ananuka.
''Wengine hawakua na shida wanajua jinsi nilivyohangaika na hii hali, hivyo walikua wakifurahi, lakini baadhi walikua hadi wanatema mate eti nanuka!''
Ugonjwa huu ni wa aina gani?
Ugonjwa wa Fistula ya uzazi huwapata wanawake wengi wakati wa kujifungua hasa wale wanaozaa wakiwa na umri mdogo pamoja na kukosa msaada stahiki wakati wa kujifungua.
Ugonjwa huu husababisha mwanamke ashindwe kujizuia haja ndogo ama kubwa.

Chanzo cha picha, AMref health
''Fistula ya uzazi inatokea pale mwanamke anapopata uchungu kwa muda mrefu au mtoto anapokwama kwenye nyonga za uzazi na kusababisha sehemu laini za nyonga kukandamizwa na hatimaye kukosa damu, na sehemu hizo zinakufa na kuacha tundu ambalo ndio fistula.'' anasema Daktari Venance Wilfred.
Aidha Dakatri Venance anaongeza pia kutokana na tundu sehemu ya kibofu na uke ama tundu lisilo la kawaida kati ya uke na sehemu ya haja kubwa husababisha mwanamke atoe mkojo au haja kubwa bila kujizuia .
Kwa Mujibu wa Hospitali ya CCBRT Nchini Tanzania wanawake zaidi ya elfu tatu hupata ugonjwa huu lakini wengi hawapati matibabu stahiki kutokana na uelewa kuwa mdogo.
Huduma za afya za kutibu ugonjwa huu ni bure katika baadhi ya hospitali nchini Tanzania ikiwemo CCBRT.
Lakini kukosa elimu kwa wanawake husababisha matibabu kutokuwafikia wa wakatii,
Dr Florence temu, mkuregenzi wa shirika la AMref health Africa Tanzania, anasema kuwa kupitia mradi wao wamekua wakiwasaidia kisaikolojia wanawake hawa kutokana na kutengwa na jamii na unyanyapaa wanaokumbana nao.
''Wengi wa wanawake hawa baada ya kupata fistula ya uzazi, huwa wanakumbwa sana na unyanyapaa na kutengwa na familia zao, sisi tumeweza kuwafikia katika vijiji mbalimbali na kuwapa msaada wa kisaikolojia, lakini pia tumekua tukitoa mafunzo kwa watumishi wa afya wakiwemo Madkatari wanawasadia wanawake hawa.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani inakadiriwa kuwa wanawake zaidi ya milioni mbili kutoka Afrika na asia wanaishi na ugonjwa huu, bila kupatiwa matibabu yoyote,
Kwa upande wa Tanzania wengi wamekua wakitafuta msaada kwa waganga wa jadi.













