Rais Magufuli kuwania muhula wa pili wa uongozi, yapi mafanikio, changamoto?

John Magufuli, CCM party's presidential candidate in Tanzania - July 2015

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, John Magufuli amejitengenezea jina la kuwa mchapa kazi
Iliyochapishwa

Rais wa Tanzania, John Magufuli amechukua fomu ya kugombea muhula wa pili wa nafasi ya urais wanchi hiyo kupitia chama chake , Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Magufuli amechukua fomu hizo katika ofisi ya CCM mkoani Dodoma, siku moja baada ya kulivunja bunge lililomaliza muda wake kikatiba.

Tanzania sasa rasmi imeingia katika mchakato wa uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba, huku CCM pamoja na vyama vingine vya siasa nchini humo vikitoa ratiba ya ndani ya ugombeaji nafasi zote kuanzia urais mpaka madiwani.

Siku ya Jumanne alipokuwa akihutubia shughuli za kuvunja mkutano wa 11 wa bunge amesifu namna serikali yake ilivyotekeleza ahadi zake ilizotoa wakati alipokuwa anawania kiti hicho mwaka 2015.

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Tanzania, John Magufuli

Mafanikio na changamoto katika muhula wa kwanza wa uongozi wake

Magufuli amefanikiwa kwa kuweka rekodi nzuri katika kupanua na kuboresha miundombinu kama barabara, umeme na kufanya mabadiliko kadha wa kadha katika sekta ya madini.

Rais Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015 aliahidi kupanua barabara, reli na miundombinu ya umeme.

Serikali yake ilipitisha sheria mpya ya madini iliyolenga kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa kati faida kati ya Makampuni makubwa ya madini na serikali.

''Mabadiliko makubwa yamefanyika ikiwemo kuzuia utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi kwa kufungua masoko ya madini katika kila mkoa, ili kuongeza ushirikishwaji wachimbaji wadogo,'' alisema alipokuwa akilihutubia bunge.

Pamoja na kufanya mengi katika kipindi cha muhula wa kwanza, Rais Magufuli amekosolewa pia ndani na nje ya nchi akionekana kuwa kiongozi anayetoa maamuzi ya haraka kwa kutoa marufuku ya jambo au kuwaachisha kazi watendaji wa chini yake.

"Ametumbuliwa" ni neno ambalo limekuwa maarufu katika vinywa vya wengi baada ya kiongozi huyo kuwafukuza kazi watendaji pale ambapo anaona mambo hayaendi sawa.

Katika utawala wa rais Magufuli, viongozi kadhaa serikalini kuanzia mawaziri, wakurugenzi na watendaji wengine wameachishwa kazi na wengine kubadilishiwa mjukukumu.

Licha ya watendaji kuwa na hofu katika utendaji wao kumekuwa na madadiliko chanya katika utoaji wa huduma za jamii kama afya na ukuaji wa mtandao wa maji.

Ilikuwa ni jambo la kawaida wagonjwa na kina mama wajawazito kulala chini. Lakini baada ya ziara yake ya kushtukiza katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili na kufanya mabadiliko na maboresho katika vifaa.

Elimu bure kwa shule za msingi za serikali ni jambo ambalo aliweza kulifanikisha.

Rais Magufuli amekosolewa kwa kutofanya safari za nje kwenda kwenye mikutano mikubwa ya kimataifa hasa nchi za Magharibi kuliwakilisha taifa lake tangu aingie madarakani na badala yake amekuwa akituma wawakilishi wake.

Magufuli amekuwa akisisitiza msimamo wake wa kutokuwepo safari zisizo na lazima kwa watumishi wa Umma isipokuwa kwa idhini maalum.

Mara kadhaa maamuzi ya rais Magufuli yamesababisha kuitwa dikteta na upinzani na wanaharakati.

Vyama vya upinzani vilisitishwa kufanya mikutano ya hadhara na wanasiasa wengi wa upinzani wamedai kunyimwa haki zao za msingi.

Viongozi wakuu wa upinzani wamepandishwa mahakamani kwa kesi za uchochezi.

Utendaji wa vyombo vya habari na wanahabari nchini humo, umekuwa mgumu kutokana hofu na kuminywa kwa uhuru wao.

Baadhi ya watu wameshtakiwa kwa madai ya kumtusi rais kwenye mitandao ya kijamii.