Uchaguzi wa Tanzania 2020: Matukio matano ambayo yalitawala bunge la Tanzania 2015-2020

Chanzo cha picha, Bunge
- Author, Na Markus Mpangala
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Bunge la 11 la Tanzania (2015-2020) linatamatishwa leo Jumanne Juni 19, huku likiwa limegawanya mitazamo ya wachambuzi wa masuala ya siasa.
Bunge hilo likiwa chini ya Spika Job Ndugai linatajwa kutofikia viwango vya ubora wa Bunge la 9 na lile 10 chini ya Maspika Anne Makinda (2010-2015) au Samuel Sitta (2005-2010).
Job Ndugai alichaguliwa Spika wa Bunge la Tanzania mnamo Novemba 17 mwaka 2015 baada ya kumshinda mpinzani wake Goodluck Ole Medeye kutoka CHADEMA. Katika uchaguzi huo Ndugai alipata kura 254 dhidi ya 109 za Ole Medeye kati ya kura 363.
Aidha, Ndugai anakuwa Spika wa sita akitanguliwa na Adam Sapi Mkwawa ambaye aliongoza vipindi viwili kati ya mwaka 1964 hadi 1973 na mwaka 1975 hadi 1994. Wengine ni Erasto A.M Mang'enya (1973-1975), Pius Msekwa (1994-2005), Samuel Sitta (2005-2010) na Anne Makinda (2010-2015).
Chombo hicho chenye mamlaka ya kutunga sheria nchini humo kimetajwa kupoteza mvuto, huku kikiendeshwa 'gizani' kutokana na kuzuia kuoneshwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni ama redio, pia uhaba wa demokrasia,upendeleo kwa chama tawala CCM na kukiingia kifua serikali dhidi ya ukosoaji bungeni.
Kwa kipindi cha miaka mitano Bunge la Job Ndugai limerindima kwa mambo mbalimbali ambayo baadhi yamechangia taswira ya kuonekana nyuma kiufanisi kulinganisha na bunge la 9 na 10.
Yafuatayo ni mambo matamo yaliyotikisa Bunge hilo.
Kufutwa 'Bunge Live'
Januari 27, 2016, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye alitangaza umma kusitishwa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya bunge.
Tangazo hilo, kwa mujibu wa wanaharakati na viongozi wa upinzani wanadai lilikiuka katiaba ambayo inatoa haki kwa wananchi kupata habari na taarifa.

Chanzo cha picha, NApe Nauye/Facebook
Licha ya vyombo vya habari binafsi kuwa tayari kutumia gharama zao kurusha matangazo ya Bunge mbashara lakini Bunge la Ndugai lilitupilia.
Chini ya uongozi wa Spika Samuel Sitta, bunge likajizolea umaarufu kwa viwango na kasi. Serikali ya Kikwete ikatikiswa haswa na bunge hususani kwenye kashfa kubwa za rushwa/ufisadi.
Mijadala ya bunge kuhusu kashfa ya Richmond - ambapo uchunguzi wa kamati ya bunge ulibaini makosa kwenye utoaji wa mkataba wa kufua umeme kutoka Marekani - na kupelekea kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Edward Lowassa ilirushwa mbashara kwenye televisheni.
Pia 'sarakasi' za kashfa ya Escrow mwaka 2014 iliyowaondoa madarakani mawaziri wawili waandamizi na Mwanasheria Mkuu pamoja na kuwatia lawamani, wafanyabiashara wakubwa, wanasiasa mpaka majaji.
Sababu kuu ya serikali kusitisha matangazo mubashara ya bunge kupitia runinga ya taifa ilitajwa kama gharama kubwa za uendeshaji.
Hivi karibuni, katika mahojiano na runinga hiyo ya taifa, Spika Ndugai amedai kuwa lugha isiyo ya staha ya baadhi ya wabunge pia ilikuwa ni moja ya sababu ya kuzuia matanagazo hayo ya moja kwa moja.
Kwa wakosoaji, hatua hiyo wanaitaja kama ya serikali kujaribu kuzuia wananchi kushuhudia ukosoaji wa shughuli zake.
Kushambuliwa na kufukuzwa ubunge Tundu Lissu

Shambulizi la Septemba 7 mwaka 2017 dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ni moja ya matukio makubwa kuwahi kutokea katika historia ya siasa za vyama vingi nchini Tanzania.
Namna ambavyo tukio hilo limeshughulikiwa na bunge pia ni moja ya mambo ambayo yanapigiwa mfano wakati wa kukosoa miaka mitano ya bunge la 11.
Hadi Bunge linafikia tamati sakata la kushambuliwa Tundu Lissu halijapatiwa majibu hadi leo, hakuna aliyekamatwa wala kupandishwa mahakamani juu ya tukio hilo.
Akiwa ughaibuni kwa matibabu, Lissu akatumbukia katika mzozo na uongozi wa bunge juu ya kile alichokiita stahiki zake na tuhuma za mhimili huo kushindwa kulifuatilia tukio hilo ipasavyo.
Lissu alifanya ziara katika nchi mbalimbali barani Ulaya kuelezea hali ya kisiasa nchini Tanzania, jambo ambalo halikupokewa vizuri na mamlaka nyumbani Tanzania. Lissu alifanya mahojiano BBC (Uingereza) na DW (Ujerumani), VOA (Marekani).
Aidha, Januari 28, 2019 Tundu Lissu alikumbana na rungu la uongozi wa Bunge la Ndugai baada ya kufukuzwa ubunge kwa madai ya utoro pamoja na kukosa sifa kutokana na kutojaza fomu ya taarifa za mali na madeni yake.
Mvutano wa 'Bunge dhaifu' kati ya Spika na CAG
Mvutano kati ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kuhusu udhaifu wa Bunge ulichanja mbuga na kuibua mjadala mkali dhidi ya uongozi wa Bunge ambao mnamo Januari 7 mwaka 2019 ulitangaza kumwita CAG bungeni kwenda kujieleza.

Chanzo cha picha, NAOT
CAG Assad aliitika wito wa Spika na kujieleza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge uliotolewa kwake mnamo Januari 21 mwaka 2019.
Kiini cha mvutano wa wawili hao kilitokana na CAG kudai kuwa Bunge ni dhaifu kwa kushindwa kuchukua hatua juu ya mambo mbalimbali yanayowasilishwa bungeni na ofisi yake. CAG aliyaeleza hayo alipoulizwa na mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa mwezi Disemba 2018.
Spika Ndugai alidai kuwa kauli ya CAG kuwa inadhalilisha Bunge, pia akatangaza kutofanya kazi na CAG Assad.
Licha ya kushinikizwa na bunge pamoja na spika Ndugai kuomba radhi, Profesa Assad hakufanya hivyo mpaka alipoondoka mamlakani Novemba 2019 baada ya kutoongezewa mkataba na rais John Magufuli.
Hama hama na kufukuzwa wabunge
Bunge la 11 limeshuhudia wabunge 8 wakihama upinzani kwenda kujiunga CCM pamoja na mbunge wa CCM Lazaro Nyalandu kujiunga na upinzani.
Wabunge wa upinzania waliojiunga CCM na kurejea bungeni baada ya kushinda chaguzi ndogo ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Dk. Godwin Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara (Ukonga), Marwa Ryoba(Serenteti), Pauline Gekul (Babati Mjini), Lazaro Nyalandu (Singida kusini). Joshua Nassari (Arumeru mashariki) alipoteza ubunge wake baada ya kutohudhuria vikao vitatu mfululizo.

Bunge limeshuhudia chama cha CUF kikipoteza wabunge 8 wa viti maalumu baada ya kambi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba na Kaimu Katibu Mkuu Magdalena Hamisi Sakaya kumwandikia barua Spika wa Bunge Job Ndugai kuwa wamefukuzwa unachama.
Wabunge hao ni Severina Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed, anbao wanatajwa kuwa kambi ya aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho Maalim Seif Hamad.
Pia katika hatua hizi za mwisho wabunge kadhaa wa Chadema wametangaza kukihama chama hicho kwenda CCM ama vyama vingine vya upinzani pale muda wa ubunge wao utakapokwisha.
Virusi vya Corona
Virusi vya corona havikulitikisa bunge la Tanzania peke yake bali ofisi na sehemu mbalimbali ndani na nje yanchi hiyo.
Kwa Bunge la Tanzania, kama ilivyotokea kwa mabunge mengine ulimwenguni taratibu za kiuendeshaji zilibadilika kabisa.
Hata hivyo, bunge hilo ambalo lilikuwa katika mkutano wake wa mwisho wa bajeti, halikusitisha kabisa vikao vyake kama baadhi ya nchi zilivyofanya.
Hatua hiyo ilipingwa na baadhi ya vyama vya upinzani pamoja na wanaharakati.

Chanzo cha picha, CHADEMA/TWITTER
Bunge la Ndugai liliingia kwenye migogoro ya mara kwa mara na wabunge wa upinzani, na sakata la corona pia lilizua mgogoro mwengine baina ya Spika na wabunge wa Chadema.
Spika Ndugai aliwazuia wabunge wa Chadema kutoingia bunge hadi wahakikishe wamelipa posho walizolipwa kwa madai hawakufanyia kazi. Pia aliwapa sharti kuwa wataruhusiwa kuingia bungeni ikiwa watawasilisha vyeti vya kuthibitisha kuwa hawana maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona.
Uamuzi huo ulikuja baada ya wabunge wa Chadema kutangaza kwenda karantini kwa siku 14 kujikinga na corona baada ya pendekezo lao la kusitishwa shughuli za Bunge kwa siku 21 kugonga mwamba.
Wakati wa mlipuko wa corona bunge hilo limeshuhudia wabunge wake watatu wakifariki kwa kufuatana. Hata hivyo haikuthibitishwa na mamlaka, ikiwemo Bunge kuwa vifo hivyo vimetokana na corona, japo suala hilo limeacha mashaka.












