Sababu ya muswada wa kumkinga rais na mashtaka ya kikatiba kukosolewa Tanzania

Chanzo cha picha, BUNGE TANZANIA
Bunge la Tanzania limepitisha muswada wa mabadiliko mbalimbali ya sheria ikiwemo kuwapa kinga viongozi wakuu akiwemo rais kushtakiwa kwa madai ya kuvunja katiba na sheria.
Muswada huo kwa sasa unasubiri kusainiwa na rais John Magufuli ili kuwa sheria.
Kati ya mabadiliko hayo yaliyopitishwa, maeneo mawili yamezua mjadala na kupingwa vikali na wanaharakati wa haki za binaadamu na vyama vya upinzani.
Eneo la kwanza ni la viongozi wakuu wa mihimili ya dola, ambao ni Rais, Makamu wa Rais, Jaji Mkuu, Spika na Naibu Spika kwa kuvunja sheria kutoshtakiwa kwa kuvunja sheria wakiwa madarakani.
Kwa mujibu wa muswada huo, sasa atakayeshtakiwa kwa niaba ya viongozi wote hao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kambi rasmi ya upinzania na wana harakati wamekuwa wakipendekeza mabadiliko hayo yafutwe, na badala yake viongozi hao waendelee kushtakiwa moja kwa moja.
Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Fulgence Masawe ameiambia BBC kuwa kwa mabadiliko hayo, dhana ya uwajibikaji kwa viongozi hao wakuu inaondolewa.
"…shida yetu ni kuwa unaondoa dhana ya uwajibikaji. Anayeapa kuilinda katiba ni kiongozi kwa nafasi yake, sasa unaposema anapoivunja katiba uende kumshtaki mwanasheria mkuu ina maana unaishtaki serikali kwa makosa aliyoyafanya mtu mwengine."
Hata kabla ya mabadiliko haya, tayari rais analindwa kwa kinga dhidi ya mashtaka lakini ni ya jinai na si utendaji.
"Kwenye utendaji alikuwa hana kinga hiyo, kwa mfano akifanya maamuzi ambayo yanakiuka sheria na katiba unaweza kumshtaki. Sasa shida yetu tunasema hivi, kwa kawaida sheria zinaishi miaka na miaka. Rais tuliyenaye sasa anaweza kuwa mzuri, anayekuja huko mbele tunaweza kumdhibiti vipi? Kwa hiyo tunatengeneza sheria ambayo huwezi kudhibiti viongozi huko tunakokwenda," ameeleza Massawe.
Kufungua kesi za kikatiba
Kwa sasa, kwa mujibu wa sheria za Tanzania mtu yeyote anaweza kwenda mahakamani na kufungua kesi ya kikatiba pale anapoona jambo fulani hususani la ukiukwaji wa haki za binaadamu linafanyika kwa mujibu wa sheria.
Kwa muswada uliopitishwa na bunge, itahitajika mtu kuwa na maslahi ya moja kwa moja ama kuathirika moja kwa moja na sheria husika kabla ya kufungua kesi.
Wanaopinga mapendekezo hayo wanadai kuwa hiyo itaminya wigo unaotolewa na katiba wa watu kulinda misingi ya haki za binaadamu.
Wakili na mtetezi wa haki za binaadamu Jebra Kambole ameieleza BBC kuwa mabadiliko hayo yatafanya ugumu wa kufungua kesi za maslahi ya Umma.
"Kama mabadiliko haya yangefanyika miaka ya nyuma hata kesi dhidi ya ndoa za utotoni isingefunguliwa. Hii ina maana kuwa sheria ya ndoa za utotoni ingeendelea kuwepo," ameeleza Kambole.
Kwa mujibu wa wakili huyo, muswada huo utakaposainiwa na kuwa sheria watapinga kwa kufungua kesi katika mahakama za ndani na nje ya Tanzania.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Hoja za serikali ni zipi?
Akitetea mabadiliko yaliyomo kwenye muswada huo bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Profesa Adelardus Kilangi, alisema mabadiliko hayo hayataondoa dhana ya kupata suluhu.
"Lengo la kufungua kesi hizi ni kupata suluhu, hivyo hata akishtakiwa mwanasheria mkuu bado suluhu itapatikana mahakamani kisheria."
Kwa mujibu wa Profesa Kilangi, hata sasa kwenye kesi zote ambazo serikali inashtakiwa ama hata kesi za ubunge bado mwanasheria mkuu anasimama mahakamani.
"Lengo la marekebisho haya pia ni kuwa na maudhui ya dhana ya kinga dhidi ya Rais ambayo ni kulinda hadhi ya Rais na nafasi yake," amesema pia Profesa Kilangi.
Kuhusu haki ya mtu yoyote kufungua mashtaka ya haki za ukiukwaji wa haki za binadamu, amesema kuwa Katiba inaelekeza kuwa kutakuwa na utaratibu wa kufuatwa utakaowekwa kisheria.
"Hapa hatukiuki katiba, tunaweka utaratibu wa kisheria…hili suala la nani ahusike katika kufungua mashtaka haya (locus standi) ni mjadala mpana. Tunasema yule ambaye mwenye maslahi ya moja kwa moja ndiyo afungue mashtaka. Hata Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya imeweka wazi msimamo wake kuwa lazima uwe umeathirika moja kwa moja ndiyo ufungue mashtaka katika mahakama hiyo."












