Polisi mbaroni kwa kumburuza mwanamke umbali wa mita 200 kwa tuhuma za wizi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Viongozi na wanaharakati wa haki za binaadamu kutoka kaunti ya Nakuru nchini Kenya wamepaza sauti zao kukemea vitendo vya ukatili unaofanywa na polisi mjini humo.

Sasa wanamtaka Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai kuingilia kati suala hilo.

Wakiongozwa na gavana Lee Kinyanjui, wabunge Joseph Tonui (mbunge wa Kureoi Kusini), Kuria Kimani (Molo), Charity Kithambi (Njoro) na mwakilishi wa wanawake Liza Chelule, walionya kuhusu ongezeko la vitendo vya kikatili katika sehemu mbalimbali za nchi.

Katika kipindi cha miezi miwili, Gazeti la Daily Nation la Kenya limeripoti kuwa karibu watu wanane wamenyanyaswa na polisi kwa kipigo mjini Nakuru na kuwaacha wakiuguza majeraha makubwa, hali iliyozua ghadhabu miongoni mwa raia.

Video ilisambaa mitandaoni

Katika tukio la hivi karibuni, Naibu mkuu wa kituo cha polisi cha Olenguruone, OCS David Kiprotich alinaswa kwa picha ya video, ambayo imesambaa mitandaoni, akimshambulia mwanamke mmoja mwenye miaka 21 aliyekuwa akimtuhumu kuwa mnyang'anyi.

Video hiyo inamuonesha mwanamke huyo, Bi Mercy Cherono, akiwa amefungwa na kamba kwenye pikipiki na kisha kuburuzwa na polisi huyo, huku tukio hilo likishuhudiwa hadharani.

Tukio hilo limeibua hasira kwa Umma, huku viongozi na makundi ya haki za binaadamu yakikemea kitendo hicho na kutaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya afisa wa polisi aliyetenda kitendo hicho.

Kukamatwa kwa washukiwa

Gazeti la Standard la Kenya limeripoti kuwa polisi watatu wanaohusishwa na shambulio dhidi ya Mercy Cherono wamekamatwa.

Kukamatwa kwao kumekuja baada ya kufanyika uchunguzi na taasisi inayosimamia mwenendo wa polisi (IPOA) na kubaini kilichotokea wakati polisi wakidai kuwa mwanamke huyo alishambuliwa na kundi la watu.

Senata wa Nakuru Susan Kihika amesema ni vigumu kufikiria maumivu na athari za kisaikolojia alizozipata mwanamama huyo mikononi mwa polisi aliyemfunga mikono na kumburuza na pikipiki.

''Kitendo hiki cha kinyama kinapaswa kukemewa, na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya polisi aliyetenda kitendo hicho. Hatutanyamaza wakati tukiona wale wanaoaminika kulinda usalama wetu wanageuka kuwa wahalifu dhidi ya ubinaadamu,''alisema.

Wizi

Afisa wa polisi alimshutumu Bi Cherono kwa kuba mtungi wa gesi, televisheni , kompyuta mpakato na nguo nyumbani kwake.

Kwa mujibu wa mashuhuda, polisi alimchukua bi Cherono na kumtoa nje ya nyumba yake alimopanga eneo la Olenguruone kabla ya tukio.

Polisi huyo amedai kuwa bi Cherono, akiwa na washirika wake wawili, walivunja nyumba yake tarehe 6 mwezi Juni na kuiba vitu hivyo, miongoni mwa vitu hivyo ni pamoja na sare za polisi, Gazeti la Daily Nation limeripoti.

Alisema kuwa washirika wenzake kwenye tukio hilo walikimbia na baadhi ya vitu.

Katika video iliyosambaa mitandaoni, Bi Cherono, alionekana akigugumia kwa maumivu na kuomba msamaha kwa ofisa aliyekuwa akimburuta kwa pikipiki kwenye njia mbovu, huku mwanaume mwingine akimchapa.

Mwanamke huyo aliburutwa umbali wa mita 200 kabla ya kuokolewa na watu kabla ya kukimbizwa hospitali anakopatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa muuguzi aliyemhudumia katika hospitali hiyo, mwanamke huyo amevunjika mguu na kupata majeraha ya tishu kwenye mkono wake wa kulia.

Mama yake, Catherine Cherotich ametaka haki itendeke kwa binti yake.