Idadi ya waliothibitishwa kuwa na corona Kenya yafikia 2,862 , wagonjwa wapya 95 wakiripotiwa kuambukizwa

Waziri wa Afya Kenya Mutahi Kagwe

Chanzo cha picha, PICHA MINISTRY OF HEALTH KENYA/

Iliyochapishwa

Katibu wa Wizara ya Afya Kenya Rashid Aman amethibitisha kuwa wagonjwa wapya 95 wameambukizwa corona huku 92 wakiwa raia wa Kenya na 3 raia wa kigeni.

Hadi kufikia leo hii idadi ya watu 98,439 wamepimwa corona Kenya na waliothibitishwa kuambukizwa kufikia sasa wakiwa ni 2,862, Aman amesema.

Mombasa imekuwa na wagonjwa 56, Nairobi 13, Busia 10, Kajiado 6, Kilifi 3, Kitui, Kwale na Marsabit zikiwa na mgonjwa mmoja mmoja kila moja.

Aidha wagonjwa 97 wameruhusiwa kwenda nyumbani na kufanya idadi ya waliopona kuwa 849.

Aman amesema kwamba wanaohudumia wagonjwa wa corona wanastahili kuvaa barakoa za N95 ili kujikinga na maambukizi.

Hii ni baada ya Bwana Aman kusisitiza kwamba serikali itawaruhusu wagonjwa wa Covid-19 wasio kwenye hatari kuendelea kupata nafuu wakiwa nyumbani.

Wakati huohuo, ameongeza kwamba wahudumu wa afya watatu kutoka eneo la Nyeri wameambukizwa virusi vya corona.

Aidha Aman amesisitizia mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwamba wenye umri wa zaidi ya miaka 60 pia nao wavae barakoa za aina ya N95.

Akijibu maswali kutoka kwa wanahabari, Wizara hiyo ya Afya imesema kwamba inafikiria kuanzisha vituo ambapo wale walioambukizwa virusi vya corona lakini hawaoneshi dalili wanaweza kukaa na kufuatiliwa maendeleo yao.

Coronavirus