Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Virusi vya corona: Habari za kupotosha dhidi ya Rais Magufuli, Ummy Mwalimu na 'tiba' ya Madagascar
Huku idadi ya wagonjwa wa corona ikizidi kuongezeka katika mataifa ya Afrika, habari za kupotosha zinaendelea kusambazwa katika mitandao ya kijamii .
Hizi hapa baadhi ya habari ambazo zimesambazwa sana.
1. Rais Magufuli hakupiga marufuku uvaaji wa barakoa katika maeneo ya Umma
Ujumbe wa kupotosha umekuwa ukienea katika mitandao ya kijamii ikidai kwamba rais Magufuli amepiga marufuku uvaaji wa barakoa katika maeneo ya umma.
Machapisho hayo yanadai kwamba rais huyo alisema kwamba uvaaji wa barakoa utasababisha hofu na kutoa ujumbe mbaya kwa wageni na watalii wakati usafiri wa kimataifa utakaporea hali yake ya kawaida, lakini ni ujumbe wa kughushi.
Pia kuna taarifa bandia zinazosambaa ambazo zilitiwa saini nyumbani kwake huko Chato.
Hatahivyo kufuatia uchunguzi wetu , tulibaini kwamba rais Magufuli alikuwa katika mji wa Dodoma wakati huo. Msemaji wa rais ametoa wito kwa Umma kupuuzilia mbali taarifa hizo.
Serikali ya Tanzania inaendelea kuwasisitizia raia wake kuvaa barakoa katika maeneo ya Umma na kutokaribiana.
2.Waziri wa afya Ummy Mwalimu hakupatikana na corona
Habari iliyochapishwa katika mtandao wa kijamii iliyodai kwamba waziri wa Afya Ummy Mwalimu alikutwa na corona, ilisambazwa sana katika mtandao wa Twitter.
Lakini habari hiyo sio ya kweli. Chanzo cha habari hiyo ni picha ya chapisho la Twitter ambayo mwanzilishi wake anasema kwamba ilichapishwa na waziri huyo.
Tafsiri ya lugha ya kiswahili ilisoma: inasikitisha kwamba nimekutwa na corona , Lakini nitaendelea kuhudumia taifa langu kama ambaye niko katika mstari wa mbele hadi hali itapokuwa shwari.
lakini ujumbe huo haukuwa katika ukurasa wa waziri huyo . Waziri huyo pamoja na wizara yake wamepuuzilia mbali ripoti hiyo kuwa ni ghushi.
3. Njama ya kuizuia Afrika kutengeneza tiba
Tutaanza na nadharia inayomzunguka rais wa Madagascar Andry Rajoelina na tiba ambayo haijathibitishwa ya miti shamba kwa jina Covid Organic ambayo anasema ina uwezo wa kutibu corona.
Mitandao ya kijamii imekuwa ikisambaza madai kwamba anajaribiwa kuhongwa na shirika la Afya duniani ili kuitia sumu kwa siri dawa hiyo.
Nadharia hizo zisizo na msingi zinasema kwamba WHO inataka kuyathibitishia mataifa ya Afrika hayawezi kujitegemea kwa kupata tiba yao yenyewe.
Nadharia hiyo kwa mara ya kwanza ilidaiwa kuonekana katika anuani moja ya Facebook ambayo ilikuwa ikifanya operesheni zake kutoka Angola na DR Congo tarehe 23 Aprili. Madai hayo baadaye yalichapishwa na magazeti mawili nchini Tanzania tarehe 14 Mei.
Mojawapo ya ripoti hizo inadai kwamba rais Rajoelina alikiri katika mahojiano na chombo cha habari cha France24- kwamba alipatiwa fedha ili kufanya hivyo.
Habari hiyo imesambazwa sana katika vyombo vya habari barani Afrika. Bwana Rajoelina ni kweli alihojiwa na chombo cha habari cha France24 tarehe 11 Mei, lakini hakuna hata mara moja anasema kwamba alipatiwa fedha na WHO.
WHO iliiambia BBC kwamba habari hiyo ni ya uongo , na kwamba serikali ya Madagascar imekana madai hayo.
Tangu uzinduzi wa tiba hiyo , kumekuwa na matamshi ambayo yamedaiwa kutolewa na Andry Rajoelina, kulingana na msemaji wa serikali yake Lova Ranoramoro.
Kinywaji hicho cha mitishamba kinaendelea kutengenezwa nchini Madagascar na kimepelekwa katika mataifa mengine ya Afrika , lakini hakuna ushahidi kwamba kinafanya kazi dhidi ya virusi hivyo.
Shirika la Afya Duniani linasema kwamba linaunga mkono uvumbuzi kama huo unaotokana na dawa za miti shamba lakini likaweka tahadhari kuhusu dawa ambazo hazijafanyiwa vipimo.
4. Beji feki dhidi ya corona
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na maafisa wengine waandamaizi wametumia beji za kujilinda ambazo zinadaiwa kuzui corona , lakini ambazo hazifanyi kazi.
Picha zilizochapishwa katika Facebook na kitengo cha habari cha rais huyo zinamuonesha yeye na maafisa wengine wakivalia kile kinachoonekana kuwa kinafanana na aina mbili ya beji ambazo zinaweza kununuliwa mtandaoni kwa jina Air Doctor na Virus Shut Out.
Lakini hakuna ushahidi kwamba beji hizo zinaweza kuzuia virusi na bakteria.
Alipowasiliana na BBC , msemaji wa serikali ya Sudan Kusini alisema kwamba beji hizo walizipata kutoka kwa watu waliosema kwamba wanafanya kazi kwa niaba ya serikali Japan.
lakini waliongezea kwamba waliacha kuvaa beji hizo kwasababu hazijaidhinishwa na WHO.
Ubalozi wa Japan nchini Sudan Kusini umekataa kuhusishwa na beji hizo. Vifaa kama hivyo vinauzwa duniani na vimeonekana kutumiwa na wanachama wa bunge la Urusi.
Kemikali inayotolewa na beji hizo - inayoweza kutoa rangi -Chlorine dioxide- ni hatari, hatua iliofanya shirika moja la kudhibiti dawa nchini Marekani FDA kutoa onyo.