Virusi vya corona: Utafiti wa matumizi ya dawa ya hydroxychloroquine wapingwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Makala maalumu iliyobainisha kuwa hydroxychloroquine inaongeza hatari ya kifo kwa wagonjwa wa virusi vya corona imeondolewa kutokana na kuwepo na maswali kuhusu data.
Waandishi wa utafiti huo wamesema kuwa hawawezi tena kuthibitisha ukweli wake kwa kuwa kampuni ya masuala ya afya ta Surgisphere iliyotoa data hizo , haitakubali kupitiwa upya kwa data yake na chombo binafsi.
Matokeo ya utafiti yalisababisha Shirika la Afya duniani kuahirisha utafiti wake kwa dawa hiyo ya kupambana na Malaria.
Lakini viongozi akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump ameendele kusisitiza matumizi yake.
Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya afya ya Surgisphere, Sapan Desai, mmoja kati ya watafiti ameliambia gazeti la Guardian kuwa atatoa ushirikiano na chombo binafsi kitakachofanya ukaguzi lakini alisema kutoa data kunaweza ''kukiuka makubaliano ya wateja na matakwa ya kuwatunzia siri''.
Utafiti ulisema nini?
Utafiti kwenye makala hayo , uluyochapishwa mwezi uliopita kwenye jalada la kitabibu la Lancet , ulihusisha wagonjwa 96,000 wa virusi vya corona katika hospitali 671 duniani. Karibu wagonjwa 15,000 walipatiwa dawa ya Hydroxychloroquine -au dawa ya kufanana na hiyo, chloroquine ikiwa peke yake au sambamba na dawa ya kuua bakteria (antibiotic)
Utafiti huo ulihitimisha kuwa dawa haikuonesha matunda katika kupambana na virusi vya corona isipokuwa iliongeza hatari kwa wagonjwa kupata matatizo ya moyo na kifo.
Mandeep Mehra, Profesa kutoka Chuo cha Havard aliyeongoza utafiti huo, sambamba na Frank Ruschitzka kutoka Chuo cha hospitali ya Zurich na Amit Patel wa Chuo Kikuu cha Utah, alisema kwenye taarifa kuwa wamejaribu kuandaa mchakato kwa ajili ya data zao kupitiwa na mtu wa tatu, lakini taasisi ya Surgisphere ilikataa kutoa ushirikiano.
''Tunaomba radhi kwenu, wahariri na wasomaji kwa usumbufu ambao umejitokeza,'' lilisema jopo hilo.

Taarifa zaidi kuhusu virusi vya corona:

Je kuna ushahidi kuwa dawa inatibu virusi vya corona ?
Kumekuwa na maoni mbalimbali ya jamii ya wanasayansi kuhusu matumizi ya dawa hiyo katika kutibu virusi vya corona.
Hydroxychloroquine ni salama kwa kutibu malaria, na maradhi mengine kama vile lupus na baridi yabisi, lakini mpaka sasa hakuna majaribio yaliyohitimisha kuwa inaweza kutumika kutibu Covid-19.
Matokeo ya majaribio katika Chuo cha Minnesota yalionesha kuwa hydroxychloroquine haina ufanisi wa kuzuia virusi vya corona.
WHO ilisema tarehe 3 Juni kuwa itaanzisha majaribio yake baada ya kuahirishwa mwezi uliopita.
Tafiti nyingine pia zinafanyika katika nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza, Marekani na Senegal.
Mwezi Machi, Shirika la Dawa na Chakula nchini Marekani liliidhinisha ''matumizi ya dharura'' ya dawa hiyo lakini matumizi hayo yaliruhusiwa kwa wagonjwa wachache waliolazwa pekee. Lakini mwezi uliofuata, lilitoa angalizo kuhusu matumizi yake kwa kuwa kulikuwa na ripoti za baadhi ya wagonjwa kupata matatizo ya moyo.
Kwanini imejipatia umaarufu?
Pamoja na kuwepo na tahadhari kuhusu ufanisi na usalama wake, Rais wa Marekani Donald Trump aliweka wazi mwezi Mei kuwa alikuwa akitumia hydroxychloroquine kama njia ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, lakini baadae alisema ameacha.
Trump amerejelea kueleza umuhimu wa dawa hiyo. Katika mkutano na wanahabari mwezi Aprili, alisema '' utapoteza nini? Tumia.''
Kutokana na kauli ya Trumo , kulikuwa na ripoti za ongezeko la matumizi ya dawa hiyo nchini Marekani kwa dawa zote mbili Hydroxychloroquine na Chloroquine.
Pia kumekuwa na idadi kubwa ya mahitaji ya dawa hiyo duniani.
Rais wa Brazil Jair Bolsonari pia amedai kwenye video kuwa ''Hydroxychloroquine inafanya kazi katika maeneo yote'' video hiyo iliondolewa na Facebook kwa kukiuka taratibu za utoaji taarifa kwa kupotosha taarifa.













