Virusi vya Corona: Tanzania yaondosha zuio la usafiri wa ndege

Serikali ya Tanzania imeondoa zuio la ndege za kimataifa za abiria kuingia na kutoka nchini humo ili kuruhusu shughuli za usafiri wa anga na utalii kuendelea kama kawaida.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kujiridhisha kuwa mwenendo wa maambukizi ya virusi vya Covid-19 umepungua kwa kiasi kikubwa nchini humo, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana jioni na Serikali hiyo.
Taarifa hiyo ya muongozo wa usafiri, iliyotiwa saini na Waziri wa Afya wa Tanzania Bi Ummy Mwalimu pia imebainisha kuwa serikali imeondoa pia sharti la karantini ya siku 14 kwa abiria wote wanaowasili nchini, wageni au wenyeji.
"...badala yake kipimo cha kawaida kitafanyika na ukaguzi wa taarifa za kiafya wanakotoka ili kujiridhisha kuwa wanaowasili hawana maambukizi ya corona," ameeleza Msemaji Mkuu wa Serikai ya Tanzania Dkt Hassan Abbas kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Muongozo huo unasisitiza kuwa hatua kadhaa za kujikinga na Covid-19 zitaendelea kuzingatiwa, ikiwemo kwa wasafiri kujaza fomu maalumu ya maelezo kuhusu historia ya safari zao na kuzikabidhi kwa maafisa afya mipakai ama katika viwanja vya ndege.
Wasafiri pia watatakiwa kujilinda kwa kuvaa barakoa na kuhakikisha kuwa wanaacha nafasi ya kutosha baina yao ili kujiepusha na maambukizi.
Tanzania ilipiga marufuku ndege za abiria kuingia nchini humo Aprili 11 kama njia moja ya kujilinda dhidi ya virusi vya corona. Wakati huo Tnanzania ilikuwa imedhibitisha wagonjwa 32 wa corona, vifo vitatu na wagonjwa watano kupona
Mpaka sasa taifa hilo limesharipoti wagonjwa 509, vifo 21 na wagonjwa 183 kupona. Hata hivyo kuna mashaka kuwa takwimu zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa kuwa mara ya mwisho kutolewa kwa upande wa Tanzania Bara ilikuwa Aprili 29 na Zanzibar Mei 7.
Madereva wa malori ya mizigo
Aidha muongozo huo pia umewalenga maderva wa malori ya mizigo ambao wanaingia Tanzania kutoka nchi jirani.
Maderva wa malori wamekuwa katika kipindi kigumu mipakani kote Afrika Mashariki kutokana na idadi kubwa hususani kutoka Tanzania na Kenya kukutwa na maambukizi ya corona.
Kwa mujibu wa muongozo wa serikali ya Tanzania, kila gari inabidi liwe na wafanyakazi 2-3 ili kuhakikisha kuwa utaratibu wa kuvuka mpaka kuelekea nchi jirani unakuwa rahisi.
Wafanyakazi watapimwa katika vituo vya kuingilia na ikiwa watashukiwa kuwa na virusi vya corona watatengwa au kuwekwa karantini katika maeneo yaliyotengwa.
"Ikiwa wafanyakazi wa magari hayo watatengwa au kuwekwa karantini katika vituo vilivyotengwa maalum kwa kazi hiyo, wamiliki au wasimamizi wa magari hayo watatakiwa kufanya mipango kuhakikisha kuwa mizigo yao inafikishwa katika eneo walilokusudia,"inaeleza sehemu ya muongozo huo.
Wafanyakazi wa magari ya mizigo watawekwa karantini katika hoteli ambazo zitatengwa na serikali au ndani ya magari yao katika kipindi chote watakachoendelea kuwa katika eneo hilo.
Hata hivyo, wakati Wizara ya Afya ya Tanzania ikitoa muongozo huo, baadhi ya wakuu wa mikoa ya Tanzania iliyopo mpakani na Kenya wanachukua hatua ya kuzuia magari ya mizigo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira alitangaza kuzuia mgari ya Kenya kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Holili na jana Jumatatu Mkuu wa Mkoa wa Tanga alitangaza kuzuia magari ya mizigo kutoka Kenya kuingia mkoani humo kupitia mpaka wa Horohoro/Lungalunga.
Kwa nini Tanzania imefikia hatua hii?
Rais John Magufuli alieleza kuridhishwa na mwenendo wa ugonjwa wa Covid -19 nchini Tanzania.
Akieleza idadi ya wagonjwa waliopona na kuruhusiwa katika hospitali na vituo mbalimbali nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema Mungu 'amejibu maombi' na kusisitiza kuwa tahadhari ziendelee kuchukuliwa.
Aliahidi kuwa ikiwa mambo yataendelea 'hivi hivi' kuanzia amepanga kufungua vyuo ili wanafunzi waendelee na masomo na michezo iendelee.
Lakini pia aliamuru Wizara ya Mali asili na Wizara ya Uchukuzi kuziruhusu ndege zinazobeba watalii ziingie nchini Tanzania.














