Shambulio Afghanistan: Vifo katika chumba cha kujifungua kina mama vyafikia 24

watoto 19 wanaangaliwa katkahospitali ya watoto wa Ataturk

Chanzo cha picha, EPA

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Idadi ya waliouawa katika shambulio lililotekelezwa na wanamgambo dhidi ya chumba cha kujifungua kina mama nchini Afghanistan imeongezeka na kufikia 24.

Kina mama, watoto wachanga waliozaliwa na wauguzi ni miongoni mwa waathirika. Karibia watu 16 walijeruhiwa, kwa mujibu wa wizara ya afya.

Shambulio lililotokea Jumanne katika mji wa Kabul limesababisha ukosoaji mkubwa. Hadi kufikia sasa hakuna kundi ambalo limedai kutekeleza shambulio hilo.

Katika shambulio la pili siku hiyo, mshambuliaji wa kujitoa muhanga alisababisha vifo vya watu 32 katika mazishi ya eneo la Nangarhar, mashariki mwa nchi hiyo.

Rais Ashraf Ghani ametoa agiza la operesheni ya kujilinda dhidi ya Taliban na makundi mengine.

Alishtumu wanamgambo kwa kupuuza wito wa mara kwa mara wa kupunguza vurugu.

Tahadhari: Baadhi ya wasomaji huenda wakaona taarifa hii ni yenye kukera

Kundi la Islamic State (IS) lilikiri kutekeleza shambulizi lililotokea kwenye mazishi ya kamanda wa polisi eneo la Nangarhar.

Bado haijafahamika aliyeshambulia hospitali ya Dasht-e-Barchi ya Kabul, baada ya kundi la Taliban kukanusha kuhusika.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Kipi kilichotokea hospitali?

Wenyeji wanaelezea kwamba walisikia milipuko miwili kisha ufyatuaji wa risasi ukaanza wakati shambulio hilo linatokea karibu saa 10:00 (05:30 GMT) Jumanne. Takriban watu 140 walikuwa kwenye hospitali wakati huo, daktari mmoja aliyenusurika amezungumza na BBC.

Chumba cha kuzalisha kina mama katika hospitali hiyo kinaendeshwa na shirika la kimatibabu la kimataifa la madaktari wasiokuwa na mipaka (MSF) na baadhi ya waliokuwa wakifanya kazi ni raia wa kigeni.

Hospitali hiyo ilishambuliwa mapema siku ya Jumanne

Chanzo cha picha, EPA

Watu waliingiwa na wasiwasi wakati tukio hilo linatokea, daktari mmoja ameliambia shirika la AFP.

Ramazan Ali, mchuuzi aliyeshuhudia shambulio hilo, ameliambia shirika la habari la Reuters: "Washambuliaji walimfyatulia risasi yeyote aliyekuwa kwenye hospitali hiyo bila sababu."

Mama mmoja amejifungua wakati wa shambulio hilo, shirika la MSF limenukuliwa na shirika la AFP.

Mama mwengine kwa jina la Zainabu alikuwa tu amejifungua kabla ya shambulio kutokea, Shirika la Reuters limesema. Alimpa mtoto wake jina la Omid linalomaanisha 'matumaini' kwa lugha ya Dari, kwasababu alichukua miaka kadhaa kabla ya kupata mtoto.

Vurugu zilipoanza kutokea alikuwa anaelekea chooni, mama huyo alirejea kwa haraka na kumpata mwanawe aliyemzaa saa nne zilizopita, wakati huo matumaini yake ya miaka saba yalikuwa yamefikia ukingoni.

"Nimemleta mkaza mwanangu katika hospitali hii ya Kabul ili asipoteze mtoto wake," amesema Zahra Muhammadi, mama vyaa wa Zainab, akiwa anaomboleza. "Leo hii tutaupeleka mwili wa mwanae Bamiyan."

Vikosi vya Afghan vilinusuru wanawake na watoto 100 pamoja na raia watatu wa kigeni, afisa mmoja amezungumza na BBC. Washambuliaji watatu ambao wanasemekana walikuwa wamevaa sare za maafisa wa polisi wote waliuawa na maafisa wa usalama.

Picha zinaonesha wanajeshi wakibeba watoto wachanga waliorukiwa na matone ya damu kwenye blanketi na kuwahamisha hadi eneo salama.

Je hospitali zimewahi kushambuliwa siku za nyuma?

Ndio, mashambulio kama hayo katika eneo hilo ambalo wengi ni Waislamu wa dhehebu la Kishia yamechangiwa na kundi la IS, ambalo kama Taliban ni la Waislamu wa dhehebu la Sunni.

Kiongozi wa IS Kusini mwa Asia na Mashariki ya Mbali alikamatwa mjini Kabul Jumatatu pamoja na watu wengine wa ngazi ya juu, kwa mujibu wa shirika la kijasusi la Afghan.

pamoja na watoto wawili wachanga takriban kina mama 12 na maafisa wa fya waliuawa

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, pamoja na watoto wawili wachanga takriban kina mama 12 na maafisa wa fya waliuawa

2017, mwanaume mmoja wa IS aliyekuwa amejihami kwa silaha alivalia kama mhudumu wa afya na kushambulia hospitali kuu ya jeshi ya Kabul na kusababisha mshutuko na hasira na kuibua maswali kuhusu usalama.

Baadae, mamlaka ilithibitisha kwamba watu karibia 50 wameuawa.

Lakini kundi la Taliban pia lilishambulia hospitali. Septemba mwaka jana watu 20 walikufa baada ya lori moja lililokuwa na vilipuzi kulipuliwa na wanamgambo wa kundi hilo nje ya hospitali moja kusini mwa mji wa Kabul.

Je mwitikio duniani umekuwaje?

Mashambulio ya Jumanne yameshtumiwa vikali na nchi mbalimbali duniani na makundi ya kutetea haki za binadamu, huku shirika la Amnesty International likisema: "Uhalifu wa kivita uliotekelezwa Afghanistan hii leo ni jambo lisilokubalika... linastahili kuamsha dunia kutokana na madhila wanayopita raia."

"Ni nani aliyeshambulia watoto waliozaliwa pamoja na kina mama zao? Nani hufanya hivi?" Debra Lyons ameandika kupitia Twitter, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema: "Shambulio lolote kwa watu wasiokuwa na hatia ni jambo lisilokubalika, lakini kushambulia watoto waliozaliwa tu na kina mama wanaosubiri kujifungua… ni kitendo cha uovu.

"Magaidi wanaoshambulia waomboleza waliojipanga mstari kufanya sala ya mwisho kwa mwenda zake wanatafuta njia za kutenga familia na jamii, lakini hawatafaulu."

Kulingana na manusura, maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika huko Nangarhar, na bomu likalipuliwa wakiwa nusu ya sala. Idadi ya raia waliofariki imeongezeka tangu kuripotiwa kwa kisa cha kwanza. Maafisa wanasema hadi kufikia sasa watu 133 wamejeruhiwa.

Mwanamke ambaye hakuweza kujizuia baada ya shambulio hilo

Chanzo cha picha, EPA

Wakati huohuo, kaskazini mwa Balkh karibia watu 10 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la anga lililotekelezwa na vikosi vya Marekani, ripoti zinasema.

Wakaazi na kundi la Taliban wanadai kwamba waathirika wote walikuwa raia wa kawaida, lakini Wizara ya Ulinzi ya Afghan imesema wote waliouawa walikuwa wanamgambo.

Kipi kinachoendelea katika mazungumzo ya amani ya Afghan?

Tangu makubaliano ya Februari ya kuondoa wanajeshi wa Marekani kutiwa saini kati ya Marekani na Taliban, mazungumzo kati ya serikali ya Afghan na Taliban yamegonga mwamba kwasababu ya suala la kubadilishana wafungwa na ghasia zimeendelea kushuhudiwa.

Makubaliano hayo yalilenga kumaliza vita vya miaka 18 tangu vikosi vya Marekani vilipoondoa kundi la Taliban madarakani kufuatia shambulio la kigaidi la 9/11 dhidi ya Marekani, lililoongozwa na Osama Bin Laden.

Maelfu ya watu, wengi wao wakiwa raia wameuawa kwasababu ya mapigano. Wengine wengi zaidi wamejeruhiwa au kulazimika kuhama makazi yao.