Virusi vya corona: Mfungwa aliyeachiliwa huru ameshindwa kurejea nyumbani

zaidi ya wafungwa 20,000 wameachiliwa huru ili kupunguza idadi yao

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, zaidi ya wafungwa 20,000 wameachiliwa huru ili kupunguza idadi yao
Iliyochapishwa

Arif (ambaye sio jina lake halisi) alipoachiliwa huru kutoka gerezani magharibi mwa India machi 31, alikuwa na hamu sana ya kurejea nyumbani.

Lakini kwa kipindi cha majuma mawili, amefukuzwa mara tatu katika miji miwili kutoka mji wao na ule wa mfungwa mwenzake - kabla ya kuishia kwenye makazi ya muda.

Alitoroka na kujaribu kurejea kwao tena na kwa sasa hivi yupo kwenye karantini katika nyumba ya rafiki yake.

Anayopitia Arif yanajikita kwenye unyanyapaa na kudhalilishwa ni jambo linalowakabili wafungwa wengi nchini India ambao wameachiliwa huru wakati nchi hiyo ikiwa inatekeleza hatua za kusalia ndani kusitisha maambukizi ya virusi vya corona.

Mwanaume huyo mrefu mwenye umri wa miaka 32, aliyekuwa akifanya kazi ya kuendesha taxi alishikiliwa katika gereza la Taloja magharibi mwa jimbo la Maharashtra kwa miezi sita bila kufikishwa mahakamani kwa madai ya kuiba simu ya mkononi.

Aliruhusiwa kuachiliwa kwa dhamana lakini familia yake haikuweza kulipa rupee 15,000 zilizohitajika sawa na ($198; £160). Hivyo basi akawa hana la kufanya zaidi ya kusalia jela.

Arif ni miongoni mwa wafungwa 22,000 ambao wameachiliwa huru hadi kufikia sasa kwa dhamana binafsi au kwa msamaha kulingana na data ya Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Jumuia ya Madola.

Simulizi yake iliarifiwa BBC na mashirika yanayojaribu kumsaidia kuanza maisha mapya. Ingawa juhudi za kuwasiliana na Arifa hazikufua dafu. Ni miongoni mwa maelfu ya watu wanaopitia hali kama yake kote nchini humo.

Kuachiliwa huru kwa wanaume na wanawake kama Arif kunawadia wakati ambapo mahakama ya juu zaidi ilitaka serikali za majimbo kuwaachilia huru wafungwa katika magereza yenye msongamano wa wafungwa kote nchini India kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid-19.

Mahakimu wanasema kwamba wafungwa waliohukumiwa ambao wanahudumu kifungo cha hadi miaka saba au chini wanaweza kuachiliwa huru.

Pia wale ambao kesi zao bado zinasikilizwa zinaweza kupitiwa tena ikiwa inawezekana wakaachiliwa huru.

Lakini siku ambayo Arif aliachiliwa huru, hakuna aliyekuja kumchukua.

Jela hiyo yenye zaidi ya miaka 1400 inawahifadhi wafungwa 450,000

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jela hiyo yenye zaidi ya miaka 1400 inawahifadhi wafungwa 450,000

Nyumbani ni Mahad, mji wenye vilima vidogo, kilomita 150 kutoka gerezani. Baba yake aliaga dunia. Mke wake alimuacha mwaka jana, akilalamikia uraibu wake wa kunywa pombe uliokuwa umepitiliza. Kaka yake ambaye ni mlemavu, anayefanyakazi ya mkono katika kampuni moja ya kibinafsi, siku hiyo alikuwa kazini na pia hakuwa na pesa za nauli. Na mama yake mzee ambaye ni mgonjwa, hakuwa amelipa kodi ya chumba kimoja anachoishi kwa miezi sita na anatunzwa na majirani.

Akiwa hana hata shilingi na mwenye njaa ajabu, Arif alitembea na kuomba msaada na kuruhusiwa kupanda malori akiwa kwenye barabara kuu kabla ya kufika numbani jioni siku ya pili. Lakini punde tu baada ya kuwasili, majirani wakaandamana.

"Ametoka Mumbai. Hatuwezi kumruhusu kukaa na sisi," walisema. Mji huo wa magharibi, eneo ambalo kitovu cha masuala ya kifedha na burudani umekuwa na waathirika wengi wa ugonjwa wa covid-19 nchini India, huku zaidi ya watu 13, 500 wakisemekana kuambukizwa na vifo 500 vikithibitishwa.

Arif aliyekuwa na msongo wa mawazo alirejea. Aliomba simu ya mkononi na rupee 400 kutoka kwa mama yake.

Akapungia mkono gari la kubeba bidhaa za msingi na kumlipa dereva rupee 200 ambaye alimbeba na kumrejesha Mumbai, ambapo mfungwa mwenzake alikuwa amemuahidi makazi.

Asijue kwamba jirani mwengine katika eneo alilokuwa amekaribishwa na rafikie huko Mumbai amepigia simu maafisa wa polisi, na wenyeji wakamfukuza. "Wakati huu alikuwa eneo la Mumbai. Mama yake alinipigia simu na kuniomba ni msaidie kijana wake," Manohar Fansekar, mfanyakazi wa jamii anasema.

Mapema Aprili, Arif alipatikana akiwa mitaani na kupelekwa katika makao ya watu wasiokuwa na makazi viungani mwa mji wa Mumbai.

Aliishi hapo kwa zaidi ya wiki tatu. Usiku wa Aprili 30, alitoroka makazi hayo na kujaribu tena kurejea nyumbani.

Mamlaka inajaribu kuandaa usafiri kwa wafungwa walioachiliwa huru

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mamlaka inajaribu kuandaa usafiri kwa wafungwa walioachiliwa huru

"Ninataka kurejea nyumbani. Kila mmoja anaenda nyumbani. Naomba munipe pesa na muniachilie niende nyumbani. Mama yangu amekuwa akiniita," alikuwa akimuambia hivyo mfanyakazi wa jamii kabla ya kutoroka.

Lakini kwa mara nyengine tena, majirani waliokuwa na hasira hawakumruhusu kuingia.

Akaondoka ten a na kuelekea kwenye nyumba ya rafiki yake iliyoko mjini.

Wiki iliyopita, wafanyakazi wa jamii wanasema, Arif alilewa na kumuomba msukuma riksho ampeleke hadi kwa mama yake. Lakini kabla ya kuingia alipo mama yake, aligombana na mwendeshaji riksho hiyo na kuiharibu.

Kwa sasa hivi familia inajaribu kutafuta rupee 4,000 kumlipa mmiliki wa riksho. Arif amerejea kwa nyumba ya rafiki yake ambako yuko kwenye karantini na amerejelelea tena kunywa pombe, kulingana na wafanyakazi wa jamii.

Kuachilia wafungwa wakati wa kanuni ya kutotoka nje halijakuwa jambo rahisi. Wengi wao wameshindwa kurejea nyumbani. Siku ambayo Arif aliachiliwa huru, mfungwa mwengine wa kike - mama maskini wa watoto wawili aliachiliwa kutoka gereza moja lililokuwa Mumbai na kupewa makazi na mfungwa mwenzake katika nyumba yake iliyoko kwenye kitongoji duni.

Wawili hao hawakuwa wanafahamiana hadi pale walipoachiliwa huru kutoka gerezani pamoja. Katika eneo la Latur, Maharashtra, wafanyakazi wa jamii wamefanikiwa kuwapa makazi wafungwa 24 walioachiliwa huru.

Ndani ya gereza, wasiwasi na hali ya kujitenga ndio inaotawala miongoni mwa wafungwa. Wengi wamezua vurugu wakitaka kuachiliwa huru.

Machi, mtu mmoja aliuawa na wengine 28 kujeruhiwa katika gereza moja magharibi mwa mji wa Kolkata ambao awali ulifahamika kama Calcutta.

Moja ya sababu ni kwamba jamaa zao hawawezi tena kuwatembelea kwasababu ya kanuni zilizowekwa kukabiliana na mlipuko wa virusi vua corona.

"Kutembelewa ni miongoni mwa yale ambayo yalikuwa yakiwapa matumaini. Kukatisha mawasiliano na wanafamilia kunaathiri wafungwa kisaikolojia," Madhurima Dhanuka, kutoka Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Jumuiya ya madola, amesema.

takriban wafungwa 70 wameambukizwa virusi vya corona katika jela ya mjini Mumbai Arthur road

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, takriban wafungwa 70 wameambukizwa virusi vya corona katika jela ya mjini Mumbai Arthur road

Mashirika yasio ya serikali yanatoa wito kwa serikali kuachilia huru wafungwa ambao ni wagonjwa. Aidha makundi ya kujitolea yanasaidia wafungwa na familia zao kwa kuwapa makazi, chakula na pesa kidogo za matumizi.

Ingawa mahakama ya juu zaidi inataka idadi ya wafungwa kupunguzwa, watu bado wanakamatwa na kuwekwa magerezani kwa kukiuka kanuni za kusalia ndani pamoja na makosa mengine.

"Naweza kukadiria kwamba tumefanikiwa kupunguza msongomano wa wafungwa kwa asilimia 10 pekee baada ya wafungwa kuachiliwa huru. Magereza yetu bado yamesongamana kiasi kwamba ni muda tu ndio unaosubiriwa kwa janga baya zaidi kutokea," Vijay Raghavan, mkurugenzi wa shirika moja la kusaidia walioachiliwa huru anasema. Hilo tayari ni kama limeanza kutokea.

Kote duniani, magereza yamekuwa vitovu vya maambukizi. Hadi kufikia wiki hii, wafungwa 77 katika ya 2,600 wameachiliwa huru katika gereza la Mumbai Arthur Road prison - lililokuwa la wafungwa wa ngazi ya juu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Pia maafisa 26 wa magereza walipata maambukizi. Mfungwa mmoja zaidi aliambukizwa katika gereza la Satara. "Tunafanya maandalizi ya kuwapeleka wafungwa hospitali," afisa mmoja mwandamizi, Deepak Pandey, amesema.

Wakati huohuo, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tagu alipoachiliwa huru, Arif bado anajaribu kurejea nyumbani.