Nywele bandia si salama kwa wanawake wa Kinshasa, kulikoni?

Iliyochapishwa

Katika mji mkuu wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo(DRC) wanawake wamekua na hofu baada ya wizi wa nywele zao za bandia al maarufu wigi pamoja na za kushonelewa zinazofahamika kama weave kuibiwa.

Wizi huu umeshamiri katika mitaa ya mji huo jambo ambalo linalowafanya wanawake kuwa na wasiwasi mkubwa wanapotembea njiani au barabarani huku wakiwa wamejipamba kwa nywele hizo bandia.

Mwandishi wa BBC mjini Kinshasa Mbelechi Msochi anasema kuwa wizi huu umetokana na kuibuka kwa biashara ya nywele bandia zilizotumiwa. "Tunatembea barabarani kwa hofu, lazima kuangalia kichwa kila wakati kama sivyo mwizi atakuja kung'oa nywele zako ambazo umevaa kichwani'', anasema mmoja wa akinadada aliyevalia wigi.

Eneo la Matonge mjini Kinshasa ni moja ya maeneo yenye shughuli nyingi za burudani na anasa, ambako visa vya kunyofolewa kwa wigi na nywele nyingine za kushonelewa kichwani vimekua vikishamiri.

Katika Saluni moja mjini Kinshasa makumi kadhaa ya wanawake waliokua wakipandikwa nywele za bandia waliiambia BBC kuwa japo wanabandika nywele hizo ili kuwa warembo zaidi, maisha yao yamekua ya hofu kutokana na wizi wa nywele hizo.

'' Karibu wiki mbili zilizopita wezi waliongoa nyele zangu ambazo nilikua nimenunua nunua dola mia moja na hasmni za Marekani sasa hatujuwi kama tusiwe tunajipamba tena au vipi". Alisema mmoja wao :''Mimi niliona msichana ambae alikuwa juu ya pikipiki, wezi wakaja na kumuong'oa nyele zake bandia, msichana akaanguka na gari likaja kumgonga; alifariki, niliona pia mwigine ambae alikuwa ndani ya gari, wezi wakaingiza mkono dirishani na kumuong'oa nyele zake...sasa sijui kama katika hali hiyo tutatuishi vipi, usalama wetu umekuwa hatarini kwa ajili ya nywele ambazo sisi wenyewe tumejinunulia", anasema Bi Jeanine.

''Nimelazimika kutembea na upala''

Berte anafanya kazi katika ofisi moja, kwa kumuona kweli hana nywele , kichwa chake ni kipara kabisa, lakini nywele hizo za kubandika au za kuvaa kama kofia maarufu kama wigi ndizo zinamusaidia kupendeza, lakini yeye ameamua kuvaa wigi mara afikapo kazini ili kuepuka kuibiwa. "Mimi baada ya kuibiwa nyele zangu, nimekuwa makini, nikialikwa kwenye sherehe fulani, nachukuwa nyele zangu naweka ndani ya begi, nikifika mlangoni ndo nazivaa tena, sherehe ikimalizika, wakati wakurejea nyumbani, basi naondoa na kuzirejesha tena ndani ya begi"

Si kila mtu anaweza kununua nywele bandia mjini Kinshasa

Mamuu Lukebuka ni muuzaji wa nywele bandia na mmiliki wa Saluni anasema wanawake waliovaa wigi au kushona nywele bandia wanapaswa kuwa waangalifu kwasababu zinahatarisha maisha yao: ''Unaona hapa ninauza nywele ndefu dola mia tatu, na siwezi kupenda kusikia wateja wetu wawe wanaibiwa nywele zao kila mara, mimi binafsi na hisi ni vema, wakivaa hiyo kofia ya nywele ni vema waishonelee kichwani badala ya kuacha hivo'', Anasema Mamuu na kuongeza kuwa...kama unataka urembo wa nywele za kubadika, basi wakati unapotembea hapa kinshasa tazama upande wako wa kushoto, kulia , mbele na nyuma kwani wezi pia wanahitaji hizo nywele zako'', anasema.

Unaweza pia kusoma: