Kobe Bryant: Vanessa azungumza kuhusu alivyoathiriwa na kifo cha mumewe

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mke wa Kobe Bryant Vanessa amefungua kimya chake kwa mara ya kwanza tangu ndege aina ya helikopta kumuua mumewe, na mwanawe mmoja na watu wengine saba Jumapili iliopita.

Katika chapisho moja katika mtandao wa instagram na picha ya familia, alisema kwamba ameharibikiwa kabisa na kwamba hakuna maneno ya kutosha kuelezea uchungu alionao.

Wawili hao walikuwa na watoto wanne wasichana akiwemo Gianna mwenye umri wa miaka 13 aliyefariki katika mkasa huo wa ndege pamoja na babake. Hakuna maelezo yoyote kuhusu mipango ya mazishi yake.

Sababu ya mkasa wa ajali hiyo iliotokea katika ukungu mkubwa magharibi mwa mji wa Los Angels bado inachunguzwa.

Bryant alikuwa akielekea kufunza timu ya mpira wa vikapu ya mwanawe katika mchuano wa vijana katika chuo cha mafunzo ya michezo cha Mamba Sports Academy.

Katika chapisho lake, Vanessa pia alisema: Tumeathiriwa na kifo cha ghafla cha baba ya watoto wangu na mwanangu mpenzi Giana, ambaye ni dadake Natalia , Bianka na Capri.

Aliongezea: Natamani ningekuwa nao hapa maisha yangu yote. Walikuwa baraka iliyochukuliwa kwetu haraka. Sijui maisha yetu yatakuwa vipi na hatuwezi kufikiria maisha bila wao.

Pia aliwashukuru watu kwa usaidizi wao na kutangaza mfuko wa fedha ambao utasaidia familia za wale wengine waliofariki katika mkasa huo.

Wengine waliofariki walikuwa rubani, wasichana wengine wawili wenye umri wa miaka 13 wazazi wao watatu na mkufunzi mwengine.

Bryant alikuwa bingwa mara tano wa taji la ligi ya NBA akiichezea timu yake ya Los Angeles Lakers na mshindi mara mbili wa medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki.

Baada ya kucheza mpira wa vikapu kwa takriban miaka 20 alistaafu mwezi Aprili 2016. Siku ya Jumatano timu ya Lakers iliweka kumbukumbu ikimtaja Bryant kuwa zaidi ya mchezaji wa mpira wa vikapu.

''Tumeshangazwa sana na kifo cha Kobe Bryant na mwanawe Gianna, Lakers ilisema katika taarifa iliochapishwa katika mtandao wa instagram.

''Maneno hayawezi kuelezea umuhimu wa Kobe kwa klabu yake ya zamani ya La lakers, mashabiki wetu na mji wetu. Alikuwa zaidi ya mchezaji wa mpira wa kikapu, alikuwa baba mpendwa na mchezaji mwenza. mapenzi yao yatasalia katika mioyo yetu milele''.