Wanajeshi wa Kenya wadaiwa 'kutoroka' shambulio la al-Shabab Lamu

Iliyochapishwa

Majeshi ya Kenya yamepinga vikali madai yaliochapishwa katika gazeti la New York Times kwamba maafisa wake "walijificha kwenye nyasi"wakati wanamgambo wa kiislam wa al-Shabab waliposhambulia kambi ya kijeshi ya Manda Bay.

Wanajeshi watatu wa Marekani waliuawa nkatika shambulio la Januari 5.

Kambi inayofahamika kama, Camp Simba, ipo katika eneo la Hindi Magogoni pembezoni mwa kisiwa hicho cha kitalii Lamu hutumiwa na vikosi vya Kenya na Marekani.

Taarifa ya New York Times ilidai kuwa utenda kazi wa wanajeshi wa Kenya uliwatia hofu wenzao wa Marekani.

Pia ilisema kuwa wanamgambo wa Al-Shabab walinufaika na taarifa waliyopewa na Wakenya waliokuwa katika kambi hiyo.

Lakini msemaji wa majeshi ya Kenya kanali Paul Njuguna ameiambia BBC kuwa taarifa hiyo haikuegemea msingi wawote wa kweli.

Aliongeza kuwa maelezo kuhusu shambulio hilo yatakjulikana pale bodi iliyopewa jukumu la kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo itakapotoa ripoti yake.

"Taarifa hiyo haina msingi wowote. Uchunguzi unaendelea kwa mujibu wa wachunguzi, sio rasmi,"alisema kanali Njuguna.

Gazeti la Kenya la Daily Nation pia limemnukuu afisa wa jeshu wa ngazi ya juu wa jeshi ambaye hakutajwa ambaye alisema; "Kambi ya Simba ni kituo cha kijeshi kinachotumiwa na Marekani kuendesha oparesheni ya kiusalama. Kinasimamiwa na kupewa ulinzi na Wamarekani."

Vyanzo hivyo pia viongeza kuwa: "Kilichofanyika katika kambi hiyo mpaka sasa hakijafichuliwa hadi wa leo, Marekani haijatoa taarifa kamili ni wanajeshi wangapi walikuwa katika kambi hiyo wakati wa shambulio hilo ''Ni wao ndio wanaondesha mabo katika kambi hiyo."