Je, ni nani waliozimiwa simu Tanzania?

Usiku wa Januari 20 uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na machungu na wamiliki wa takribani laini milioni 20 za simu nchini Tanzania, ambao hawajasajili laini hizo kwa alama za vidole.
Saa nne ya usiku wa jana Jumatatu laini zote hizo ilitangazwa kuwa zitazimwa. Hata hivyo hali ni tofauti, na wengi ya wanaomiliki laini hizo bado wapo hewani.
Kampuni ya Vodacom imetangaza hii leo kuwa wateja wake 157,000 wamekatishiwa huduma za mawasiliano baada ya kushindwa kusajili laini zao kwa alama za vidole.
Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom Hisham Hendi amewataka wateja kuendelea na zoezi la usajili katika vituo vyao ili waendelee kupata huduma za mtandao huo wa simu.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) uzimwaji wa laini sasa utafanyika kwa awamu, na kwa kuanzia umewalenga watu zaidi ya 900,000.
"...Wapo watu tayari ambao wanazo namba za utambulisho wa taifa, wanafika 656,091 lakini hawajasajili laini zao. Kundi la pili ni watu 318,950 waliosajili laini zao kwa kitambulisho cha Taifa kabla ya kuanza mfumo wa kusajili kwa alama za kidole...Hawa wote hawana sababu ya kutozimiwa laini zao leo (jana usiku)," Mkurugenzi Mkuu wa TCRA James amelieleza Shirika la Habari la Taifa (TBC).

Chanzo cha picha, Eagan Salla
Kwa mujibu wa Kilaba, uzimaji huo unafanyika kwa awamu ili kuondoa usumbufu.
"...usajili wa laini hauna kikomo. Tunazima kidogo kwa sababu ya mambo ya kitaalamu, hauwezi ukazima laini milioni tano au 10 kwa mara moja."
Kilaba pia amesema uzimaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole unafanyika kwa awamu kuanzia jana Jumatatu Januari 20, 2020 ili kuondoa usumbufu."
Hata hivyo BBC imejiridhisha kuwa kuna baadhi ya watu ambao wana namba ama vitambulisho vya Taifa lakini hawajasajili laini zao na bado wapo hewani.
Pia TCRA haijafafanua kuwa mchakato huo wa kufungia laini utajumuisha awamu ngapi na lini utafikia tamati.
Mpaka tarehe 19 mwezi Januari mwaka 2020 waliojisajili walikuwa watu28,433,491 sawa na asilimia 58.2.
Watumiaji wa simu ambao hawajajisajili kwa alama za vidole ni watu 20,418,656 sawa na asilimia 41.8.
Idadi ya kadi za simu inaelezwa kuwa 48,852,147, kwa mujibu wa Afisa Mwandamizi Mkuu wa TCRA Semu Mwakyanjala.












