Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bomu lalipuka karibu na wahandisi wa Uturuki na kuwajeruhi watu 6 Afgoye Somalia
Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari ambalo lilikuwa likiwalenga wajenzi kutoka Uturuki limelipuka katika eneo la Afgoye, kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Mogadishu, polisi wamesema.
Imeripotiwa kwamba gari hilo ambalo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi liligonga katika eneo ambapo wakandarasi hao wa Uturuki pamoja na maafisa wa polisi walikuwa wakila chakula chao cha mchana, kulingana na afisa wa polisi Nur Ali ambaye alizungumza na Reuters kutoka Afgoye.
Haijulikani ni nani aliyetekeleza shambulio hilo lakini wakaazi na maafisa wa polisi wanasema kwamba wapiganaji wa al Shabaab walijaribu kushambulia Afgoye, takriban kilomita 30 kutoka Mogadishu ,Ijumaa iliopita kabla ya kufurushwa.
Kundi hilo linalohusishwa na wapiganji wa al Qaeda limekiri kutekeleza mashambulio ya hapo awali katika kampeni zake za kuipindua serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
''Tulisikia mlipuko mkubwa na muda mfupi kukatokea moshi mkubwa hewani. Kabla ya mlipuko huo , wahandisi kadhaa wa Uturuki na msafara wa magari wa polisi wa Somalia waliojihami walionekana katika eneo hilo'', kulingana na mfanyabiashara mmoja wa duka aliyezungumza na Reuters kutoka Afgoye."
''Kufikia sasa tunajua kwamba wahandisi watatu wa Uturuki na wakalimani wao walijeruhiwa'' .
''Maafisa wawili wa polisi pia walijeruhiwa katika mlipuko huo'', Ali alisema baadaye alipoulizwa kuhusu majeruhi.
Kituo cha habari cha Uturuki kwa jina Anadolu kimesema kwamba raia wanne wa Uturuki , wakiwa wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi waliojeruhiwa katika shambulio hilo walikuwa wakitibiwa katika hospitali , kulingana na habari zilizotoka kwa ubalozi wa Uturuki mjini Mogadishu.
Wahandisi wa Uturuki wamekuwa wakisaidia katika ujenzi wa barabara.
Tangu ukame wa mwaka 2011 nchini Somalia, Uturuki imekuwa ikitoa usaidizi mkubwa kwa taifa hilo huku Ankara ikitafuta kuongeza ushawishi wake katika eneo la upembe wa Afrika.
Kundi moja la wahandisi ni miongoni mwa watu walioshambuliwa wakati wa mlipuko wa bomu wa mwezi Disemba uliosababisha vifo vya watu 90.