Juhudi za wakili wa Kenya Miguna Miguna kurejea nchini zatibuka

Iliyochapishwa

Wakili wa Kenya mwenye utata Miguna Miguna, emedai kuwa mamlaka nchini Ujerumani imemzuia kuabiri ndege ya kuja Kenya.

Bw. Miguna amesema kuwa tahadhari imetolewa kwamba asiondoke uwanja wa ndege wa Berlin kuelekea uwanja wa kimataifa wa JKIA au nchi yoyote ya Afrika.

Ndege ya shirika la Lufthansa aliyokuwa aabiri kuja Kenya ilikuwa imepangiwa kuondoka nchini Ujerumani saa tano na dakika ishirini na kuwasili Nairobi saa tatu na dakika ishirini na tano za usiku, majira ya Afrika mashariki.

Hatua hiyo inajiri saa kadhaa baada ya mahakama ya juu nchini Kenya kutoa agizo la kuitaka serikali ya Kenya kutomzuia wakili huyo aliyefurushwa kurejea nchini humo.

Pia unaweza kusoma

Serikali ya Kenya imesema kuwa itashughulikia suala hilo ili kumsaidia mwanasiasa huyo wa upinzani kurejea nchini siku ya Junanne, karibu miaka miwili baada ya kumfurusha kwenda Canada.

Wizara ya mambo ya ndani katika, taarifa yake imesema, itazingatia agizo la mahakama la mwaka 2018 ambalo liliagiza serikali impatie Bw. Miguna na stakabadhi za kumsaidia kurejea nchini humo.

Mahakama hiyo pia ili amuru maafisa wa kutetea haki za binadamu kuruhusiwa kuingia katika uwanja wa ndege kufuatilia mchakato huo.

Miguna Miguna ni nani?

Miguna alizaliwa katika kijiji cha Magina, katika jimbo la Kisumu, magharibi mwa Kenya.

Bw Miguna amekuwa kiongozi wa kundi linaloitwa National Resistance Movement (NRM, Vuguvugu la Taifa la Kupinga Serikali), ambalo liliundwa na muungano wa upinzani wa National Super Alliance siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao Bw Odinga alisusia mnamo 26 Oktoba mwaka 2017.

Bw Miguna baadaye alijitangaza kuwa Jenerali wa NRM.

Mnamo 30 Januari, siku ya kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi', muungano huo uliorodheshwa kuwa kundi haramu na waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Bw Miguna kujipata akikabiliana na serikali na nguvu zake.

Mwaka 1988, alikamatwa na serikali ya wakati huo ya Rais Daniel arap Moi.

Bw Miguna baadaye alitorokea Kenya ambapo alipata hifadhi kama mkimbizi wa kisiasa.