Rais wa Uganda Yoweri Museveni aanza matembezi ya siku sita jangwani

Yoweri Museveni

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Yoweri Mueseveni, akiongoza matembezi tofauti mwezi uliopita
Iliyochapishwa

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameanza matembezi ya siku sita jangwani, kama sehemu ya kumbukumbu ya jinsi vikosi vyake vilivyopambamba mwaka 1986 kunyakua madaraka mikononi mwa Idi Amin na Milton Obote.

Wapinzani wake wamekosoa matembezi hayo wakidai kuwa na mpango wa kujipatia umaarufu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao, ambapo Bw. Museveni anatarajiwa kugombea uraisi kwa muhula wa sita.

Anakabiliwa na upinzani kutoka kwa msanii wa zamani wa muziki na mwanasiasa Bobi Wine, ambaye anajinadi kama mkombozi wa masikini.

Bwana Museveni atakamilisha matembezi hayo katika mji wa magharibi wa Birembo, eneo ambalo mapigano makali yalizuka kati ya vikosi vya waasi vikiongozwa na yeye (Museveni) na wanajeshi wa aliyekuwa rais wa Uganda wakati huo Milton Obote, Junuari 10 .

Katibu mkuu wa mawasiliano ya rais, Don Wanyama, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa: "Safari hii inayoongozwa na rais, ni hatua ya kukumbuka yaliyopita ili kujivunia hali ilivyo sasa.

"Safari hii itadumu kwa wiki moja jangwani, kupitia njia iliyopitiwa na wakombozi wa nchi wakiongozwa na Museveni."

Bw. Museveni, 75, ni mmoja wa viongozi wa Afrika waliohudumu madarakani kwa muda mrefu.

Map

Bw. Wine -ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi -ameliambia shirika la habari la AFP kwamba matembezi hayo ya rais ni ya "kupoteza muda".

"Ushauri wangu kwake, badala ya kuharibu fedha za walipa kodi kwa safari kama hizo, Museveni anatakiwa kufahamu kuwa muda wake madarakani umeisha," Wine alisema. "Muda wa kuwahadaa masikini umepita."

Mbunge wa upinzani MP Asuman Basalirwa pia ametaja matembezi hayo kama "kigezo cha kampeini".

"Waganda wanataka uongozi bora na wala sio rais anayetembea jangwani,"alisema.

"Muda huo ungelitumiwa kuangazia masuala muhimu kwa taifa , hususan jinsi anavyopanga kupokezana uongozi."