Sudan kuwalipa waathiriwa wa mkasa wa bomu wa 1998 Kenya na Tanzania

Ndugu ya waathiriwa wa mkasa wa bomu wa 1998 jijini Nairobi akisoma majina ya walioathirika

Chanzo cha picha, SIMON MAINA

Maelezo ya picha, Ndugu ya waathiriwa wa mkasa wa bomu wa 1998 jijini Nairobi akisoma majina ya walioathirika
Iliyochapishwa

Waziri mkuu mpya wa Sudan Abdalla Hamdok, ameahidi kwamba taifa lake hivi karibuni litawafidia takriban dola bilioni 6 waathiriwa wa mkasa wa bomu nchini Kenya na Tanzania katika balozi za Marekani za 1998 mjini Nairobi na Dar es Salaam.

''Tulichukua jukumu la kuangazia madai hayo na kuafikia makubaliano'', alisema waziri mkuu Abdalla Hamdok akinukuliwa na gazeti moja nchini Marekani.

Hatahivyo mawikili wa waathiriwa hao wanatilia shaka ahadi hiyo wakisema kwamba huenda isilipwe.

Bwana Hamdok alikuwa akisema hayo wakati wa ziara yake ya kwanza nchini Marekani ambapo alitaka Sudan kuondolewa katika idadi ya mataifa yalioorodheshwa na Marekani kwamba yanaficha magaidi.

Familia zitakazofidiwa

Takriban familia 570 za wafanyakazi wa balozi za Marekani na wanakandarasi waliouawa katika mashambilio pacha yaliotekelezwa na kundi la al Qaeda mjini Nairobi na Dar es Salaam wanatarajiwa kufidiwa.

Hatahivyo fidia hiyo ilioagizwa na mahakama ya Marekani haitawafaidi maelfu ya Wakenya na Watanzania ambao waliathiriwa na mashambulio hayo aidha moja kwa moja au kwa njia nyengine lakini hawakuajiriwa na balozi ama kampuni za kibinafsi ambazo zilifanya biashara na balozi hizo.

Takriban watu 224 walifariki katika mashambulio hayo pacha- 214 mjini Nairobi na 10 Dar es Salaam.

Idadi hiyo inashirikisha Waafrika 212 na Wamarekani 12.

Je Sudan inahusika kivipi na mashambulizi hayo?

Mahakama za Marekani zimeiwajibisha Sudan kulipa fidia ya $5.9 bilioni kwa watu hao kwa kuwa ilihusika kumficha kiongozi wa kundi la al-Qaeda Osama bin Laden wakati alipokuwa akipanga njama za kutekeleza mashambulio hayo.

Manusura hao wanaweza kupokea nyongeza ya $4.3 bilioni iwapo mahakama ya kilele ya Marekani itabadilisha uamuzi wa mahakama ya chini wa kutowalipa fedha za muda waliotumia kuwasilisha kesi hiyo.

Baadhi ya waathiriwa wa mkasa huo wakitaka haki kufuatia mkasa huo

Chanzo cha picha, SIMON MAINA

Maelezo ya picha, Baadhi ya waathiriwa wa mkasa huo wakitaka haki kufuatia mkasa huo

''Fidia hiyo inatilia maanani hali ya kiuchumi ya Sudan pamoja na hali ya kiuchumi ya waathiriwa ambao maisha yao yameharibiwa na wengine wengi ambao wamekuwa masikini kwa takriban miaka 20 kufuatia kufariki kwa babao zao, mama zao ama hata mume ama mke wake'', aliandika wakili wa waathiriwa mwenye makao yake nchini Markani bwana Gavriel Mairone.

Mwanmke akisoma majina ya baadhi ya waathiriwa wa mkasa wa bomu wa ubalozi wa Kenya Jijini Nairobi 1998 katika eneo la kumbukumbu la iliokuwa ubalozi wa Markani jijini Nairobi

Chanzo cha picha, SIMON MAINA

Maelezo ya picha, Mwanmke akisoma majina ya baadhi ya waathiriwa wa mkasa wa bomu wa ubalozi wa Kenya Jijini Nairobi 1998 katika eneo la kumbukumbu la iliokuwa ubalozi wa Markani jijini Nairobi

Wakili huyo amesema kwamba tayari amewasiliana na mawakili wa serikali ya Sudan ili kuonyesha uwajibikaji wao na ameweka mapendekezo ya kutatua mgogoro huo.

'Tunasubiri mapendekezo muhimu kutoka kwa waziri mkuu huyo', aliongezea mwanasheria huyo mkuu ambaye anafuatilia sana kesi zinazohusika na maswala ya ugaidi.

Masharti ya Marekani kwa Sudan

Sudan iliorodheshwa miongoni mwa mataifa ya ugaidi 1993.

Muda mfupi baada ya shambulio la kigaidi la ubalozi wa Marekani jijini Nairobi 1998
Maelezo ya picha, Muda mfupi baada ya shambulio la kigaidi la ubalozi wa Marekani jijini Nairobi 1998

Vikwazo vinavyotokana na taifa lililoorodheshwa katika orodha hiyo ya ugaidi inazuia taifa hilo kutoshiriki kikamilifu katika maswala ya uchumi duniani.

Na ili kuondolewa kutoka katika orodha hiyo, Sudan ilihitajika kuafikia msururu wa masharti ya Marekani ikiwemo kuwalipa jamaa za wafanyakazi wake walioathiriwa katika mashambulio hayo ya bomu.

Bwana Hamdok aliateuliwa kuwa waziri mkuu mwezi Agosti kufuatia maandamano dhidi ya serikali ambayo yalimng'atua madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo Omar al- Bashir.

Kiongozi huyoo mpya ameahidi kufanya mabadiliko katika sera za ndani za taifa hilo pamoja na zile za kimataifa.

Maafisa wa Sudan awali wamekuwa wakilalamikia umasikini kama sababu kukwepa mauaji bila kukubali jukumu la madhara na uharibifu wa kiuchumi dhidi ya waathiriwa.