Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran 'inatengeneza silaha zenye uwezo wa kinyuklia' mataifa ya Ulaya yaonya
Mataifa matatu ya Ulaya yenye uwezo mkubwa yameuonya Umoja wa mataifa kwamba Iran inatengeneza silaha za masafa marefu zenye uwezo wa kinyuklia hatua ambayo ni ukiukaji wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa.
Barua iliotumwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani inasema kwamba Iran ilifanyia majaribio silaha yake aina ya Shahab 3 ilioshikana na gari ambalo linaweza kusukuma silaha ya kinyuklia.
Kitendo kama hicho ni ukiukaji mkubwa wa azimio lililoidhinisha mpango wa kinyuklia wa mwaka 2015., Iran imekana madai hayo.
Waziri wa masuala ya kigeni Mohammed Javad Zarrif amesema kwamba barua hiyo ilikuwa ya uongo iliyoandikwa na mataifa hayo ya Ulaya ili kuziba uzembe wao wa kushindwa kuafikia makubaliano ya mpango wa kinyuklia wa Iran.
Azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa 2231 linatoa wito kwa Iran kutotengeneza silaza za masafa marefu zilizo na muundo wa kubeba nyuklia, ikiwemo kurusha makombora kupitia teknolojia hiyo ya makombora ya masafa marefu.
Iran imesisitiza kwamba mpango wake wa Kinyuklia ni wa amani na kukana madai kwamba mpango wake wa kutengeneza makombora ya masafa marefu unakiuka azimio hilo.
Lakini barua hiyo ya mataifa ya Ulaya inasema kwamba picha za video za jaribio katika mitandao ya kijamii tarehe 22 mwezi Aprili zinaonyesha utumizi wa kombora la Shabab 3.
Kutokana na hilo imebainika kwamba kombora hilo linauwezo wa kinyuklia.
Teknolojia ya kombora hilo ambayo ilianzishwa ili kuzuia kuenea kwa nyuklia, inasema kwamba mfumo wa kwanza wa kombora hilo una uwezo kubeba uzani wa kilo 500 hadi umbali wa takriban kilomita 300.
AP imesema kwamba barua hiyo ilitoa mifano mingine mitatu ya vitendo vya Iran ambavyo Uingereza , Ufaransa na Ujerumani zinasema vinakiuka azimio hilo la 2231:
- Kurushwa kwa kombora la masafa marefu kwa jina Shahab 3 tarehe 24 mwezi Julai
- Kurushwa kwa kombora la masafa ya wastani kwa jina Borkan 3 na waasi wa Houthi nchini Yemen ambao Iran imeshutumiwa kwa kuwahami
- Uzinduzi uliofeli wa gari la kurusha makombora kwa jina Safir tarehe 29 mwezi Agosti.
Waziri wa maswala ya kigeni nchini Israel Israel Katz aliunga mkono barua hiyo na kutoa wito kwa wanadiplomasia wa Israel kuwasilisha ripoti kamili ya Iran kuhusu ukiukaji huo wa makubaliano ya kinyuklia ya Iran katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 19 Disemba ambapo linatarajiwa kuzungumzia kuhusu Iran.
Iran imekiuka baadhi ya makubaliano yake chini ya mkataba huo katika miezi ya hivi karibuni ikijibu hatua ya rais wa Marekani Donald Trump kujiondoa katika makubaliano hayo mwaka uliopita kuiwekea vikwazo vya kiuchumi.
Bwana Trump anataka kuishinikiza Iran kurudi mezani na kujadiliana kuhusu makubaliano mapya ambayo yataweka vikwazo katika mipango yake ya kinyuklia na pia kusitisha utengenezaji wake wa silaha za masafa marefu .
Iran imekataa kurudi katika meza ya mazungumzo hadi pale Marekani itakapoondoa vikwazo vyake.
Mataifa mengine matano katika mkataba huo ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, China na Urusi - yamejaribu kuuheshimu mkataba huo . lakini vikwazo hivyo vimefanya biashara ya mafuta ya Iran kuporomoka , thamani ya sarafu yake kushuka huku mfumuko ukiongezeka.
Katika habari nyengine maafisa wa Marekani wanasema kwamba wanamaji wake waliopo katika eneo la Ghuba wamekamata vifaa vya silaha za kisasa vinavyoshukiwa kutoka Iran kuelekea Yemen.
Vifaa hivyo vinadaiwa kukamatwa katika boti dogo wiki iliopita.