Bernadette Lukoki: Mwalimu ajuza ataka serikali kumpatia nyumba badala ya fedha DRC

Iliyochapishwa

Mwalimu ajuza aliyefunza shule moja nchini DRC kwa kipindi cha miaka 66 Bernadette Lukoki sasa ameiomba serikali kumkumbuka kwa kumpatia nyumba badala ya fedha zake za kustaafu kama kumbukumbu ya kazi yake.

Kikongwe huyo ambaye amegonga vichwa vya habari Afrika mashariki kwa kuendelea kufunza licha ya kuwa na umri mkubwa ameiomba serikali kumstaafisha kwa kuwa hana tena nguvu za kuendelea na kazi hiyo.

Akizungumza na waziri huyo wa elimu ajuza huyo amemtaka afisa huyo wa serikali Didier Mudimbu kumtafutia mahala ambapo anaweza kuishi maisha yake yaliosalia.

''Kulingana na jinsi nilitumikia muda mrefu na kupita umri wa kuustaafu, nimepambana na ugojwa, kujikimu kimaisha, baba waziri, mimi kweli sina tena haja ya kupewa hizo pesa, waziri, wewe ndo ulinitafuta, unitafutie mahala nitaweza kukaa hadi mwenyezi mungu atakaponichukuwa''. Alinukuliwa akisema.

Alisema kwamba hatofundisha tena baada ya kukutana na waziri huyo huku akimtaka kufuatilia maswala yake ya kustaafu.

Kwa upande wake waziri huyo alisema malalamishi ya kikongwe huyo yatasaiia kutatua kesi nyingi za wakongwe ambao wanaedelea kuchapa kazi licha ya muda wao wa kustaafu kutimu.

Alisema kwamba licha ya kuwa serikali haina mapato mengi inapaswa kuangazia matatizo yanayowakumba watu kama hao.

Bernadette lukoki , ameendelea kufanya kazi akiwa na umri wa miaka 83, licha ya kwamba umri wa mwisho wa kufanya kazi kisheria nchini humo ni miaka 65.

Kila siku , bibi huyu amekuwa akiiomba serikali kumkumbuka ili apumzike hivi sasa, kwa kuwa afya yake imeanza kudhoofu.

Mzee huyu anafundisha darasa la kwanza, na kwamba wanafunzi wake humuita Bibi, kwani wengi wao ni kama wajukuu.

''Kulingana na miaka mingi niliyofundisha ninajua namna ya kufanya ili wakae kimya na waelewe ninachowafundisha kwasababu ninapenda watoto wawe na ujuzi''.

Mwalimu huyu mwenye miaka 83 amekuwa kwenye kazi ya ualimu kwa miaka 66 .Lakini kwa sasa si kazi rahisi kwake.

Bibi Bernadette anaendelea kufundisha huku akisubiri malipo yake ya mwisho kutoka serikalini.

'' Kwa kusema kweli,siwezi tena kuendelea kufundisha watoto kwa kuwa wazazi hawalipi tena ada ya shule ya msingi, hivyo kufanya idadi ya watoto kuongezeka, na kazi zimekuwa nyingi zaidi, inanibidi kumfuatilia kila mmoja'' alieleza.

''Siwezi kubaki nyumbani, nilianza kazi hii tangu 1953 , na pesa ndogo nimepata hapa zimenisaidia.''

''Nimeshaitumia serikali jina la mama huyu kila mara kuomba astaafu lakini sipati jibu, mama huyu ameanza kutumika kabla ya mimi kuzaliwa, na ameendelea kutumika na mimi, ni ma mbo ya kusikitisha sana, kweli anafundisha vizuri, kulingana na umri wake anapaswa kupumuzishwa. Nimeomba viongozi wetu waangalie namna ya kumstaafisha mama huyu''.

Bi bernadette , amesema, hadi sasa hajapata matunda ya kazi yake, anaendelea kuishi katika hali ya umasikini kama kila mwalimu, mshahara wake ulifikia zaidi ya dola mia mwezi jana wakati rais rais alihaidi kurebisha maisha ya walimu.

Baada ya miezi nne baada ya kuapishwa kwake ; Raisi Felix Tshisekedi aliahidi kushughulikia wafanya kazi wa serikali ambao wamefikisha umri wa kustaafu.BBC Ilijaribu kumuuliza Mkurugenzi wa shule ili kufahamu kwa nini mama huyu bado hajapumzika, Kongwaka Litela Yvone ni mkurugenzi wa shule ya msingi EP Mushi.