Maonyesho ya sanaa ya mikono yamewaleta watu kutoka nje ya Tanzania

Visiwani Zanzibar yanaendelea maonesho ya aina yake ya Sanaa mbalimbali ikiwemo uchoraji na picha. Ni tamasha la kwanza la aina yake likiwa na lengo la kulinda Sanaa hii kwa miaka ijayo. wasanii kutoka Tanzania Bara, Zanzibar, Ghana na Senegal wameshiriki.
Ni wiki muhimu kwa wasanii wa kuchora, kuchonga, na picha ndani na nje ya zanzibar wanaokutana hapa kuonesha kazi zao za sanaa
"Ni nafasi nzuri sana kwa sisi watu wa Sanaa, hasa wachanga, wanahitaji kusaidiwa na wasanii wakubwa na tamasha kama hili ni mwanzo wa mafanikio kwetu" anasema Mwandali Mwanyekwa mchongaji wa vinyago.
Unaweza pia kusoma:
Kwa miaka mingi Zanzibar imekua kivutio Cha watalii kutoka nchi mbalimbali, lakini wasanii wa hapa na nje ya Zanzibar wanaona ni fursa nzuri ya kuendeleza shughuli za utalii na kuhifadhi kazi za Sanaa kwa vizazi vijavyo.

Waziri wa habari, utamaduni na masuala ya kale Mohamoud Thabiti Kombo anasema kuwa tamasha hili ni mwanzo wa kulinda kazi za sanaa na kuhifadhi historia .
"Zanzibar tangu miaka ya sabini tulikua na sanaa , lakini kadri muda ulivyokwenda ikaanza kufa , si kwa sababu ya serikali bali kwa sababu ya wasanii wenyewe, sasa utaliii umeongezeka sana na hatua hii itaanza kuinua tena Sanaa ya hapa na nje ya eneo hili".
Wakazi wa hapa zanzibar na Watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani wameonesha kuvutiwa sana na tamasha hili lakini hasa umuhimu wake katika kutunza sanaa za wazanzibari na wasanii kutoka nje ya zanzibar .
"Nimefurahi sana kuja hapa na naona Zanzibar itatangazwa zaidi kupitia sanaa, na sisi tutafaidika mana watalii pia wataongezeka sana" Amesema Juma Rajab mmoja wa washiriki wa tamasha hili.

Kwanini tamasha hili limeanzishwa sasa?
Wazo la kuanzisha onesho hili la kila mwaka limetoka kwa baadhi ya waandaji wakiwemo wasanii wenyewe.
Hamad Mbaruku Hamad mmoja wa waanzilishi anasema kuwa , "Sanaa hizi ni muhimu sana hapa visiwani zanzibar kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani katika vipindi vyote vya mwaka".












