Mahakama ya kimataifa ya ICC yatoa hati ya kukamatwa kwa rais Vladmir Putin wa Urusi

Chanzo cha picha, bbcnews
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita (ICC) imetoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Mahakama ya ICC inadai kuwa anahusika na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kuwahamisha watoto kutoka Ukraine kwenda Urusi kinyume cha sheria.
Inasema uhalifu huo ulifanyika nchini Ukraine kuanzia tarehe 24 Februari 2022 - wakati Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili.
Moscow imekanusha madai ya uhalifu wa kivita wakati wa uvamizi huo.
Mahakama ya ICC imemshtaki Bw Putin kwa kuhusika katika kuwafukuza watoto, na inasema ina sababu za kuridhisha kuamini kuwa alifanya vitendo hivyo moja kwa moja, pamoja na kufanya kazi na wengine.
Mahakama pia ilisema kiongozi huyo wa Urusi alishindwa kutekeleza haki yake kuwazuia wengine waliowahamisha watoto.
Kamishna wa haki za watoto wa Urusi, Maria Alekseevna Lvova-Belova, pia anasakwa na mahakama hiyo
Licha ya kibali hicho cha kumkamata putin na Bi Lvova-Belova kutolewa, ICC haina mamlaka ya kuwakamata washukiwa, na inaweza tu kutumia mamlaka ndani ya nchi ambazo zimesaini makubaliano yaliyounda mahakama hiyo.
Urusi sio mwanachama wa makubaliano hayo - kwa hivyo hakuna uwezekano wa kiongozi huyo kuwasilishwa mbele ya mahakama hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
hata hivyo inaweza kuwaathiri kwa njia nyinginezo, kama vile kutoweza kusafiri.
Ujumbe huo ulikaririwa na Bi Zakharova ambaye alisema "Urusi si sehemu ya Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na haina wajibu wowote chini yake."
Viongozi wa upinzani wa Urusi walikaribisha tangazo hilo, huku mshirika wa karibu wa mkosoaji wa Kremlin Alexei Navalny Ivan Zhdanov akitweet "wow!".
"Hati ya kukamatwa kwa Putin! Ndiyo, ni hatua ya kiishara. Lakini ina umuhimu gani!" Bwana Zhdanov aliandika.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Ukraine Andriy Kostin alisema uamuzi huo ni "wa kihistoria kwa Ukraine na mfumo mzima wa sheria za kimataifa", huku mkuu wa wafanyikazi wa rais wa Ukraine Andriy Yermak akipongeza uamuzi huo kama "mwanzo tu".
Jonathan Leader Maynard, mhadhiri wa siasa za kimataifa katika Chuo cha King's College London alisema uamuzi wa kumfungulia mashtaka Bw Putin haukumshangaza.
Aliiambia BBC kuwa mahakama imekuwa na uchunguzi wa wazi kuhusu uhalifu wa kivita unaoweza kutokea tangu Machi 2022 na nguvu ya ushahidi ina maana "ni vigumu kuona jinsi gani ICC inaweza hatimaye kuepuka kutoa hati za kukamatwa."
Bw Maynard vile vile alikariri kwamba Putin hangeweza kusumbuliwa sana na mashtaka hayo, kwani ICC "inategemea ushirikiano kutoka kwa serikali ili kuwakamata watu, na serikali ya Urusi ni wazi haitatoa ushirikiano katika suala hili".
Lakini alisema inaweza kuathiri uhuru wa Bw Putin kusafiri kote ulimwenguni kwani mataifa mengine yaliyotia saini ICC yanaweza kusaidia katika kukamatwa kwake.












