Guruneti ambalo halijalipuka latolewa kwenye kifua cha mwanajeshi wa Ukraine  

TH

Chanzo cha picha, FACEBOOK/UKRAINE MEDICAL FORCE COMMAND

Iliyochapishwa

Guruneti ambalo halikulipuka limetolewa kwenye kifua cha mwanajeshi wa Ukraine.

Picha za kabla na baada kwenye  ukurasa wa Facebook wa huduma ya matibabu ya jeshi la Ukraine zinaonyesha X-ray ya kilipuzi karibu na moyo wa askari, na nyingine ya  daktari wa upasuaji akiwa ameshikilia guruneti hilo lenye damu..

Chapisho hilo lilisema wanajeshi wawili walisaidia kusimamia operesheni hiyo ili kuhakikisha inafanyika kwa usalama.

Askari aliyejeruhiwa sasa anapata nafuu, kundi hilo lilisema.

Chapisho hilo la mtandao wa kijamii lilisema upasuaji huo ulifanyika bila kutumia umeme-njia ya kawaida ambapo mkondo wa umeme hutumiwa kusaidia kudhibiti kuvuja damu wakati wa upasuaji - kwa sababu "risasi hizo zinaweza kulipuka wakati wowote".

Iliongeza kuwa kifaa hicho kilikuwa ni bomu la VOG - kipande cha risasi cha urefu wa 4cm ambacho hurushwa na kinaweza kusafiri umbali wa mita 400, na kimeundwa kulipuka juu ya ardhi.

TH

Chanzo cha picha, FACEBOOK/UKRAINE MEDICAL FORCE COMMAND

 

Operesheni hiyo ilifanywa na Meja Jenerali Andrii Verba, anayetajwa kuwa "mmoja wa madaktari bingwa wa upasuaji" wa vikosi vya jeshi vya Ukraine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Haijulikani ni lini operesheni hiyo ilitekelezwa au ni wapi mwanajeshi huyo alijeruhiwa, ingawa chapisho hilo lilichapishwa Jumatatu.

 

Takriban miezi 11 baada ya Urusi kuanzisha uvamizi wake mbaya, mapigano mashariki mwa nchi yanaendelea huku wanajeshi wa Ukraine wakijaribu kuwarudisha nyuma wanajeshi waliotumwa na Moscow.

Siku ya Jumanne, kundi la mamluki la Wagner lilitangaza kuwa "limevamia" jiji la Soledar katika mkoa wa Donetsk na lilikuwa linaudhibiti kikamilifu, ingawa Kyiv ilisema wanajeshi wake wanashikilia, katika taarifa ya baadaye .

Soledar itakuwa faida ya kimkakati kwa Urusi, kwani jiji hilo linajivunia migodi ya chumvi ambayo ingewapa wanajeshi wavamizi mahali pa kuweka askari na vifaa, vilivyolindwa dhidi ya makombora ya Ukraine.

Pia iko karibu maili sita kusini-magharibi mwa Bakhmut ambapo wanajeshi wa Urusi kwa sasa wanalenga mashambulio yao.

Kunyakua udhibiti katika eneo lolote lile kutakuwa  ushindi wa propaganda unaohitajika sana kwa Moscow, kufuatia vikwazo kadhaa vikubwa nchini Ukraine tangu vita hivyo vilipoanza, ikiwa ni pamoja na kupoteza udhibiti wa Kherson, mji mkuu pekee wa kikanda kusini ilikoweza kuuteka.