Ucheshi sio kwa binadamu tu,wanyama pia hufanyiana utani

Iliyochapishwa

Unapofikiria juu ya kile kinachotofautisha spishi zetu na wanyama wengine, basi ucheshi inaongoza kwenye orodha.

Tunapenda kucheka - sana, kiasi kwamba furaha inayotokana na vichekesho inaonekana usoni mwetu. Watoto walio na umri wa miezi mitatu pia hucheka, katika hali ambayo inafurahisha wazazi wao wanapovuta nyuso za kuchekesha. Kufikia miezi minane, watoto wachanga wamejifunza jinsi ya kutumia nyuso zao, miili na sauti zao kuwafanya watu wazima wacheke.

Muda baadaye, wazazi wanaweza kutambua kwamba mtoto wao amegeuka kuwa mcheshi wa wakati wote, akicheza kimakusudi na mambo ambayo wanajua kwamba hawapaswi kufanya kwa tabasamu la usoni.

Lalkini, utafiti mpya unaonyesha kuwa huenda sio wanadamu pekee walio na ucheshi. Wanyama wanaweza kutaniana pia. Pamoja na wenzake, Isabelle Laumer, mtafiti wa baada ya udaktari katika Chuo Kikuu cha California Los Angeles (UCLA), alitazama zaidi ya saa 75 za video za nyani wakubwa wakiwasiliana.

Nyani wakubwa ni jamaa zetu wa karibu wanaoishi, na ni pamoja na orangutan, sokwe, bonobos na nyani. Nyani katika utafiti wote waliishi katika mbuga za wanyama, na walirekodiwa wakihudhuria shughuli zao za kila siku.

Washiriki wa aina zote nne walionekana wakitaniana. Watafiti waligundua tabia 18 tofauti za kudhihaki, huku tano bora zikiwemo kuchokoza, kugonga, kuzuia harakati za nyani mwenzao, kupiga mwili kwa nguvu, na kuvuta sehemu ya mwili. Sokwe fulani walitikisa mara kwa mara sehemu za mwili au vitu mbele ya nyuso za nyani wenzao, au, kwa upande wa orangutan, walivutana nywele.

"Tulichoona mara kwa mara ni kwamba mtoto alikuwa akiingia kisiri nyuma ya mtu mzima ambaye alikuwa akijishughulisha na kumtunza nyani mwingine, na kuendelea kuwachokoza au kuwapiga mgongoni, wakati mwingine hata kuwashangaza," anasema Laumer, mwandishi wa kwanza wa utafiti huo.

"Basi walikuwa wakingoja na kuangalia majibu ya mtu mzima.

Kawaida, walengwa wangewapuuza tu, na hivyo wangeendelea kukejeli, na kufanya tabia hiyo kuwa ya kina na ngumu kupuuza, hadi wakati mwingine waliishia kupiga wakubwa na miili yao yote."

Kwa vile spishi zote nne za nyani zina uwezo wa kudhihaki kwa kucheza, inapendekeza kwamba hali ya ucheshi inaweza kuwa ilikuwepo katika babu yetu wa mwisho ambaye aliishi miaka milioni 13 iliyopita.

Walakini, wanasayansi wengi wanaamini kuwa ucheshi umeenea zaidi kati ya wanyama kuliko huu.

Kwa mfano, katika kitabu chake The Descent of Man, mwanabiolojia Charles Darwin anadokeza kwamba mbwa wanaweza kuwa na ucheshi.

"Ikiwa fimbo au kitu chochote kama hicho kitatupwa kwa mtu, mara nyingi atakichukua kwa umbali mfupi; na kisha kuchuchumaa nacho chini karibu na mbele yake, atasubiri mpaka bwana wake atakapokuja karibu kabisa kukichukua.

Kisha mbwa atamshika na kukimbilia kwa ushindi, akirudia ujanja ule ule, na ni dhahiri akifurahia mzaha huo wa vitendo."

Yeyote anayemiliki mbwa anaweza pia kuwa aligundua kuwa wakati wa kucheza, hutoa aina ya sauti ya kuvuta pumzi ambayo karibu inaonekana kama kicheko.

Katika utafiti wa 2005, mtaalamu wa tabia za wanyama Patricia Simonet aliwachezea mbwa sauti kwenye kituo cha uokoaji.

Aligundua kuwa kusikiliza "kicheko"cha mbwa kulifanya mbwa wa makazi wasiwe na mkazo.

Marc Bekoff, profesa mstaafu wa ikolojia na biolojia ya mageuzi katika Chuo Kikuu cha Colorado, Boulder, anasema amekusanya data ya miongo kadhaa inayoonyesha mbwa wakijihusisha na tabia ya kutania sawa na ile iliyoonyeshwa na Laumer na wenzake.

Kwa mfano, unapojaribu kupata mbwa ambaye hataki kucheza, mbwa mmoja anaweza kumkaribia mwingine kwa mwendo wa kucheza kamari kabla ya kukimbia.

"Nimeona hii kwa mbwa, mbweha na mbwa mwitu," anasema Bekoff.

Kuna hata ushahidi kwamba panya hufurahia kicheko kizuri. Kwa miaka kumi hivi iliyopita, Jeffrey Burgdorf, profesa wa utafiti katika Chuo Kikuu cha Northwestern nchini Marekani, amekuwa akichezesha panya ili kujipatia riziki.

Panya hao wanapochezewa, hupiga kelele kwa furaha kwa sauti ya juu inayofanana na kucheka.

Wanarudi tena na tena kwa zaidi, na wanaweza hata kufundishwa kucheza kujificha na kutafuta "malipo ya kufurahisha", kulingana na kazi iliyofanywa na kikundi tofauti katika Chuo Kikuu cha Humboldt cha Berlin. Sasa Burgdorf na timu yake wanatumia matokeo yao kufahamisha matibabu ya unyogovu.

"Tumekuwa tukijifunza ni kwamba wanyama wanakuwa wasikivu zaidi wakati wanafanya sauti hizi," anasema Burgdorf.

"Msimamizi wangu [mwanasayansi wa neva Jaak Panksepp] daima angesema kucheza ni mbolea ya ubongo, na ni kweli. Akili zao zinaunganishwa. Wanatengeneza sinepsi mpya na miunganisho mipya ya neva.

Na kwa hivyo nadhani hiyo inatuambia kwamba wakati sisi " tukiwa katika hali hizo za ucheshi, kwa kweli tunacheza kwa ubora wetu na tunakuwa bora zaidi," anasema Burgdorf.

Hata hivyo, ingawa panya hupenda kuchekeshwa, je, kucheka kwao kwa sauti ya juu ni ushahidi kwamba wana ucheshi?

Ushahidi mwingi wa wanyama kuwa na hisia za ucheshi ni wa hadithi, kwani tafiti chache kubwa zimefanywa. Pia ni vigumu kujua kwa nini mnyama anajihusisha na tabia fulani.

Je, nyani katika utafiti wa Laumer wanacheza tu mzaha wa vitendo, au wanajaribu kupunguza mvutano, kuanzisha mchezo, au hata kupata usikivu tu?

"Je, nadhani wanyama wana hisia ya ucheshi? Ndiyo, nadhani wanayo, lakini ni vigumu kuthibitisha, "anakubali Bekoff.

Pia kuna swali la nini ucheshi unaweza kutumika kwa wanyama. Kwa wanadamu, inadhaniwa kuwa kicheko kiliibuka kama njia ya kusaidia watu kupatana. Ni njia gani bora ya kupata marafiki, baada ya yote, kuliko kushiriki utani mzuri?

Je, inawezekana kwamba ucheshi huwa na jukumu sawa katika wanyama?

"Kwa wanadamu, ucheshi unaweza kutumika kama njia kuondoa vizuizi vya kijamii na kuimarisha uhusiano," anasema Laumer.

"Hatujui kama ni sawa kwa nyani au wanyama wengine, lakini inawezekana. Ili kujua kwa hakika tutahitaji kupima na kuchunguza makundi zaidi ya nyani na aina nyingine," anasema.

Imetafsiriwa na Jaison Nyakundi