Mbio za ubingwa wa Premier League: Mechi zilizosalia za Arsenal na Man City

Iliyochapishwa

Sare ya 2-2 ya vinara wa ligi Arsenal dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili imefungua milango kwa mabingwa watetezi Manchester City katika kinyang'anyiro cha kuwania taji.

Wakati The Gunners, ambao wanawinda taji lao la kwanza tangu 2004 sasa wana pengo la pointi sita dhidi ya City, vijana wa Pep Guardiola wana mchezo mkononi na watawakaribisha timu ya Mikel Arteta tarehe 26 Aprili katika mchezo ambao unaweza kuwa wa mwisho.

City pia wana tofauti ya mabao ya juu - kwa sasa 48 dhidi ya 43 ya Arsenal - ambayo inaweza kuwa sababu.

Wakati Arsenal wamebakiza mechi nane pekee, City bado wanawinda Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa, na wanaweza kuwa na ratiba iliyojaa kati ya sasa na mwisho wa msimu.

Kulingana na uigaji wa kampuni ya data ya Nielsen's Gracenote, City sasa wanapewa nafasi kubwa ya kunyakua kombe hilo kwa asilimia 56, huku nafasi ya Arsenal ikiwa ni 44%.

Arsenal haijaifunga City katika Ligi ya Premia tangu Desemba 2015 na ushindi wao wa mwisho wa ligi kuu huko Etihad ulikuwa Januari 2015.

Timu hizo tayari zimekutana mara mbili msimu huu, huku City ikishinda 1-0 kwenye Kombe la FA mnamo Januari na 3-1 kwenye ligi mnamo Februari.

Lakini Arsenal wanaweza kuwa na historia upande wao.

Kwa mujibu wa Opta, timu 13 kwenye ligi ya daraja la kwanza zimekuwa na pointi 73 au zaidi baada ya michezo 30 (kwa pointi 3 kwa ushindi) na ni mbili tu kati ya hizi ambazo hazijafanikiwa kutwaa ubingwa - Manchester United mwaka 2011- 12 na Liverpool mnamo 2018-19. Hata hivyo, jambo la kuvunja moyo kwa mashabiki wa Arsenal, ni City ambao hatimaye walimaliza mabingwa mara zote mbili.