Kwanini bei ya Unga wa mahindi inaendelea kuzua gumzo Kenya
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC SWahili

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, taifa la Kenya na eneo la Upembe wa Afrika kwa ujumla limepata kiasi kidogo cha mvua na kusababisha ukame, mavuno duni na kuharibika kwa mazao katika baadhi ya maeneo ya nchi hizo.
Hali hii imechangiwa na majanga mengine yaliyotangulia, pamoja na uvamizi wa nzige wa jangwani mnamo 2019, athari za janga la Covid-19 mnamo 2020 na 2021, na usumbufu katika usambazaji wa chakula na pembejeo za kilimo, kufuatia vita vya Ukraine na Urusi. .
Ni kwasababu ya matatizo hayo ndiposa serikali iliyopita iliamua kuweka ruzuku katika bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta na Unga wa mahindi ili kumzuia mwananchi wa kipato cha chini kuathirika zaidi.
Vilevile suala hilo lilitumika kama kichocheo katika kampeni za uchaguzi uliopita ili kujaribu kuwavutia wananchi huku kila Mwanasiasa akijaribu kutumia tatizo hilo kuwarai wapiga kura kuwachagua.
Wengi akiwemo rais wa sasa William Ruto walisikika katika majukwaa ya kisiasa wakisema kwamba wangetibu tatizo la bei ya unga punde tu watakapochukua mamlaka.
Hatahivyo wiki kadhaa baada ya serikali mpya kuchaguliwa tatizo hilo limekuwa donda sugu, huku Wakenya wakiendelea kulipa zaidi ya shilingi 200 kwa pakiti ya kilo mbili ya bidhaa hiyo muhimu.
Kwanini Unga wa mahindi ni muhimu

Ugali, ni chakula maarufu nchini Kenya kinachopikwa kwa kutumia unga wa mahindi
Bei ya unga wa mahindi imekuwa ikipanda kwa kasi huku serikali ikihusisha hali hiyo na uhaba wa mahindi nchini Kenya.
Wanauchumi wanakadiria kuwa wakazi wa Kenya wanahitaji angalau magunia milioni 49 ya mahindi kila mwaka ili kutosheleza mahitaji ya ugali nchini, lakini ni magunia milioni 35 pekee nchini yalipatikana kabla ya dirisha la uagizaji bidhaa kufunguliwa Julai 1.
Mtangulizi wa Rais Ruto, Uhuru Kenyatta mnamo, Julai 20, alisema kupanda kwa bei kunatokana na uzalishaji uliokandamizwa na hali mbaya ya hewa, kupanda kwa gharama ya uzalishaji na kupanda kwa bei ya vyakula kote ulimwenguni.
Uhaba wa mahindi nchini Kenya ulisababisha ongezeko kubwa la bei ya unga wa mahindi - kutoka wastani wa kSh120 kwa pakiti ya kilo 2 ya unga wa mahindi hadi kSh230.
Je serikali mpya imechukua hatua gani?

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Kenya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Muda tu baada ya kuchaguliwa kwa serikali rais William Ruto Wakenya wengi hususan wale wa kipato cha chini walikuwa na matumaini sihaba kwamba , kiongozi mpya wa taifa angelitatua tatizo hilo kwa haraka iwezekanavyo .
Hii ni kutokana na wito wake wakati wa kampeni kwamba alipania kutatua matatizo yanayowakumba akina mama mboga, waendeshaji wa bodaboda na wale wasio na kazi kupitia kubuni ajira. Wito huu ulimfanya kiongozi huyo kuonekana kama mwokozi wa wanyonge.
Hatahivyo muda tu alipochukua mamlaka rais William Ruto aliondoa ruzuku katika Unga wa mahindi pamoja na mafuta, akidai kwamba ruzuku hizo zilikuwa hazimfaidi raia wa chini na kwamba badala yake zilikiuwa zikiwafaidi watu wachache serikalini.
"Kulikuwa na jaribio la kufadhili unga wa mahindi wakati wa maandalizi ya uchaguzi, mpango ambao ulipata dola milioni 58 kwa mwezi mmoja, bila athari yoyote. Mbali na kuwa ghali sana, uingiliaji kati wa ruzuku ya utumiaji huwa na matumizi mabaya, hupotosha soko na kuleta hali ya sintofahamu, ,” Ruto alinukuliwa akisema.
Hatua hiyo ilipongezwa na wengi waliodhani kwamba ingekuwa suluhu ya tatizo la kupanda kwa bei ya Unga na kwa zaidi mafuta. Kwa kuondoa ruzuku ya mahindi, William Ruto alidhania kwamba bei ya bidhaa hiyo hatimaye ingedhibitiwa na soko la bidhaa nchini Kenya na kushuka bila usaidizi wowote kutoka kwa serikali
Lakini wiki kadhaa baada ya uamuzi huo pakiti ya kilo mbili ya Unga imeendelea kuuzwa kwa zaidi ya shilingi 200 , huku tatizo hilo ambalo Wakenya walidhani limepata mtatuzi likiendelea kuwa kitendawili kisichoteguka.
Kuwasili kwa Mbolea
Kuwasili kwa mbolea ya bei nafuu ilikuwa mojawapo ya mipango ya serikali mpya katika kutatua tatizo la kupanda kwa bei za bidhaa nchini ikiwemo ile ya Unga wa mahindi.
Mbolea hiyo iliwasili muda mchache baada ya rais William Ruto kutawazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliopita ikiwa na lengo la kuwapunguzia mzigo wa uzalishaji wakulima ambao hatma yao imekuwa ikiamuliwa na mabroka, ili nao waweze kupunguza bei ya mazao yao wanapovuna.
Ni kutokana na sababu hiyo ndiposa serikali yenyewe ilichukua jukumu la kuisambaza mbolea hiyo kwa wakulima ili iafikie malengo yake.
Hatahivyo usambazaji wake umechukua muda na kukutana na msimu ambao wakulima wanapaswa kuvuna kabla ya kuanza kujiandaa kulima na kupanda mwaka ujao.
Hatahivyo Wakenya wengi wamekuwa wakijiuliza , je wakulima waliopokea mbolea hiyo wanategemea mvua au kilimo cha unyunyizaji maji.
Kutokana na uhaba wa mvua ambao umekuwa ukikumba maeneo mengi ya Afrika mashariki, ni wazi kwamba wakulima hao watalazimika kusubiri hadi msimu ujao wa upanzi ili kutumia mbolea hiyo.
Haya yote yatakuwa yakifanyika huku Mkenya wa pato la chini akizubiri miujiza ya bei ya mahindi na hatimaye Unga kushuka.

Chanzo cha picha, habarileo
Serikali kutatua bei ya Unga baada ya mwaka mmoja
“Niliwaambia lazima tushushe bei ya unga, nimeshaanza safari hiyo ya kushusha bei ya unga na kupunguza gharama za maisha, nipeni mwaka mmoja tu,” Rais William Ruto alinukuliwa akisema hivi karibuni.
Ruto alisema wakulima tayari wamehudumiwa kiasi fulani cha samadi kitakachosaidia kuwezesha kilimo na mengine yalikuwa yanakuja.
Aliongezea: “Tayari tumeshampa mkulima wetu gunia milioni moja na nusu na bado tutawapa gunia milioni sita za samadi ili kulima chakula na chakula kifike sokoni kwa bei nzuri,” alisema.
Hatua ya rais William Ruto kuomba Wakenya kumpatia muda wa mwaka mmoja kutatua tatizo la bei ya Unga ni thibitisho tosha kwamba bei ya bidhaa hiyo imezidi kuwa mwiba na kwamba serikali imeshindwa kutatua tatizo hilo kwa muda mfupi kinyume na ilivyowaahidi Wakenya wakati wa kampeni.
Lakini ni kwanini rais Ruto aliamua kuchukua uamuzi huo? Ukweli ni kwamba tupo katika kipindi cha mavuno na itachukua muda mwengine wa miezi minne hadi mitano kwa Wakulima kote nchini Kenya kuandaa ardhi zao na kuanza kupanda tena – hatua ambayo itachukua kipindi cha miezi mingine sita ili kuvuna.
Akitaja mwaka mmoja kuanzia sasa , rais Ruto ana maana kwamba atatatua fumbo hilo la bei ya Unga baada ya wakulima kuvuna mwezi Oktoba mwaka ujao.
Matamshi ya rais Ruto kuhusu kupewa muda zaidi ili kuangazia bei ya bidhaa hiyo muhimu , yaliungwa mkono na waziri mpya wa Kilimo Mithika Linturi aliyevunja matumaini ya Wakenya zaidi kwa kudai kwamba bei ya unga haiwezi kushuka kwasasa isipokuwa tu iwapo serikali ingependa kurudisha upya mfumo wa ruzuku uliotumika na serikali iliopita.
Je hali hiyo inawawacha wapi Wakenya ambao tayari wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa hali ngumu ya maisha?.Ukweli ni kwamba licha ya Wakenya kupiga kura kikabila miaka nenda miaka rudi suala la njaa halina kabila na huenda likawaunganisha iwapo hali ngumu ya maisha itaendelea kuwakodolea macho katika siku za usoni.
Jinsi Wakenya walivyopokea tangazo la Ruto
Wakenya wengi hatahivyo hawakufurahia uamuzi uliotolewa na Rais Ruto baada ya kuahidi kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu wakati wa kampeni.
Baadhi yao walisema kwamba muda alioomba ili kutatau tatizo hilo ni mrefu sana kwa mwananchi wa kipato cha chini kuvumulia.
Hatahivyo wengine walisema kwamba ijapokuwa hawakuwa na tatizo na muda ulioahidiwa na Ruto, ahadi yake wakati wa kampeni ndio inayowakera.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 1
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe, 2












