'Walifanya upasuaji wa kujifungua wakitumia mwanga wa simu, mkwe na mjukuu wangu wakafa'

Iliyochapishwa

Na Prashant Nanaware

BBC Marathi

Katika hospitali ya manispaa huko Bhandup, East Upnar, Mumbai, mwanamke mjamzito alifanyiwa upasuaji wa kujifungua (CS) kwa kutumia mwanga wa tochi ya simu baada ya umeme kukatika. Yeye na mtoto mchanga walipoteza maisha yao kutokana na upasuaji huo.

Familia ya Ansari, ambayo ilijiandaa kusherehekea mwaka mmoja wa ndoa na kuzaliwa kwa mtoto, ghafla imekumbwa na huzuni.

Katika hospitali ambako tukio hilo lilitokea, kumekuwa na matukio ya uzembe kwa upande wa wauguzi na madaktari huko nyuma, lakini utawala umeshutumiwa kuwa na uzembe.

"Nilipoonyeshwa uso wa mtoto wangu, alikuwa amekufa. Lakini walinihakikishia kwamba ana uchafu mdomoni mwake, tunamsafisha. Kuwa mvumilivu mtoto ni yuko vizuri. Kisha baada ya dakika 5-10 walikuja na kuniambia kuwa mtoto wangu amekufa."

Khusruddin Ansari, baba wa mtoto mchanga aliyekufa, alitazama kamera. Hakuwa na kingine cha kusema.

"Mtoto anapozaliwa, hushuka chini hadi tumboni chini , lakini mtoto wa mkwe wangu alikuwa kifuani na madaktari wawili walikuwa wakijaribu kumsukuma chini kutoka juu. Mtoto wetu alikufa tumboni wakati huo. Walimpeleka kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili upasuaji na kisha wakatoka ili kupata saini ya mwanangu kwenye hati kwani mambo yalienda vibaya.

"Wakati mkwe wangu alipochukuliwa, umeme ulikatika. Lakini waliendelea kumfanyia upasuaji wa kujifungua wakitumia mwangaza wa tochi ya simu . Binti yangu na mjukuu wangu walikuwa tayari wamekufa. Lakini tuliambiwa kwamba kila kitu kilikuwa sawa,"

Sahidun na Khusruddin Ansari walikuwa anatarajia kufanya sherehe ya maadhimisho ya kwanza ya harusi yao tarehe 15 Mei

Khusruddin ana mguu mmoja. Familia nzima ya Ansari ilikuwa na furaha kwani ndoa yao ilipangwa baada ya muda mrefu na habari njema ya kupata mtoto ingekuja ndani ya mwaka mmoja.

Katika kipindi cha miezi tisa, Sahidun na mtoto wake, ambao walikwenda kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara, walikuwa na afya nzuri. Daktari alisema kuwa angejifungua kwa njia ya asili. Baada ya kulazwa hospitalini Aprili 29, kila kitu kilikuwa sawa hadi jioni, mbali na dalili za kawaida za uchungu wa uzazi.

Tatizo lilikua ni nini hasa?

Sahidun Ansari, mwanamke mwenye umri wa miaka 26 anayeishi katika eneo la Hanuman Nagar katika vitongoji vya mashariki mwa Mumbai, alilazwa katika Hospitali ya Uzazi ya Sushma Swaraj ya Brihanmumbai Manispaa ya Bhandup saa 8 asubuhi Aprili 29 kwa ajili ya kujifungua.

Daktari alimchunguza Sahidun na kusema kuwa angejifungua kwa njia ya kawaida.

Hata baada ya saa 12 jioni, harakati hizo hazikusimama, hivyo ndugu walimuuliza daktari tena. Daktari alisema kuwa itachukua muda kwani ni mtoto wa kwanza.

Ndugu waliuliza tena baada ya muda kusonga mbele hadi saa mbili asubuhi. Lakini daktari huyo alisema kuwa mama na mtoto wako katika hali nzuri.

Walipoona Sahidun akizidiwa na maumivu, jamaa waliwaomba madaktari kufanya upasuaji wa kujifungua. Lakini hata hivyo, familia inasema kuwa daktari alisema kuwa uzazi wa asili utafanyika kwa saa moja hadi saa moja na nusu.

Lakini jamaa walisema kwamba ikiwa ana maumivu, mfanyie upasuaji wa kujifungua. Walidai kuwa daktari hakusema chochote kuhusu hilo.

Jioni, jamaa walimpatia chai na biskuti Sahidun kwa ushauri wa daktari. Wakati wa jioni, kiwango cha moyo wa mtoto kilikuwa 110. Daktari huyo alisema kuwa wanaweza kufanya upasuaji sasa na wakampeleka kwenye ukumbi wa upasuaji.

Rehmunnisa, ambaye ni shangazi wa Sahidun, aliarifu kuwa daktari huyo alimpasua kwa wembe Sahidun kwenye sehemu yake ya siri bila ruhusa ya jamaa zake na kumpasua kwa lazima. Damu nyingi ilitoka mwilini mwake.

Wakati huo huo, daktari alisema kuwa kiwango cha moyo wa mtoto kimefikia pointi 40 na kusema kuwa atalazimika kumfanyia upasuaji. Daktari alitoka nje ya ukumbi wa upasuaji na kuchukua saini ya Khusruddin kwenye nyaraka.

Mwili wake ulikuwa unavuja damu sana kiasi kwamba hatukujua cha kufanya, Rehmunnisa aliongeza. Baada ya hapo waliniambia kwamba wanataka kumpeleka kwenye chumba cha upasuaji. Hakuna hata mmoja wa mashangazi zake au wauguzi kutoka hospitali hiyo aliyekuwepo wakati wa kumpeleka huko. Nguo yake ilikuwa imejaa damu. Damu ilikuwa ikimwagika.

"Nilipoona haya yote nilikuwa na hofu na nilitokwa na machozi. Daktari aliniomba niondoe nguo yake. Alinipa mkasi wa kurarua nguo yake iliyokuwa imejaa damu.

Hawakuwa na kiti cha magurudumu au kitanda cha kumpeleka kwenye chumba cha upasuaji. Tukishikilia nguo nyuma yake, tulimbeba hadi kwenye chumba cha upasuaji. Wakati huo huo, umeme wa hospitali ulikatika."

Aliendelea kusema kuwa , "Sahidun alikuwa na maumivu makali na alikuwa akiniangalia usoni mwangu na nilikuwa nikimfariji. Baada ya upasuaji huo, wakati mtoto wa kiume alipotolewa, baba yake aliitwa na kuambiwa kuwa afya ya kijana huyo ilikuwa mbaya, kulikuwa na uchafu mdomoni mwake na alikuwa akimsafisha." Lakini kila kitu kitakuwa sawa. Mtoto alikuwa amekufa, lakini walimficha kwetu’’

"Baada ya muda walifika na kusema kuwa mtoto huyo amefariki. Baada ya hapo mama huyo alipelekwa hospitali nyingine.

Hawakuwa na hata wafanyakazi wa kumhamisha mgonjwa kwenye gari la wagonjwa. Ni watu wa familia yetu ambao walimhamisha kwenye gari la wagonjwa. Hawakuwa na hata hewa ya oksijeni. Alikuwa akijikuna mdomoni.

"Tulipowauliza, walisema alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Kwa kweli, alikufa hospitalini. Hata hivyo, binti yetu alipelekwa katika hospitali ya Sion. Alitangazwa kuwa amekufa huko."

Tulienda hospitali kusikia habari njema, lakini madaktari huko walituhuzunisha, anasema Rehmunnisa.

'Timu yetu ilishughulikia hali hiyo vizuri'

Kufuatia tukio hili , Shirika la Manispaa ya Mumbai limeunda kamati ya madaktari kumi wataalam kutoka hospitali tatu KEM, Shiv, na Nair. Kamati hii itawasilisha ripoti yake ndani ya wiki moja, baada ya hapo hatua zitachukuliwa dhidi ya wahalifu, alisema Afisa Mkuu wa Afya wa Idara ya Afya ya Manispaa,Daksha Shah akizungumza na BBC.

Hospitali ina jenereta, lakini siku hiyo kulikuwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara katika eneo lote. Hata hivyo, timu yetu ilishughulikia hali hiyo vizuri, Daksha Shah alisema.

Alipoulizwa kuhusu kutumiwa kwa mwanga wa tochi ya simu, katika upasuaji alisema, "Timu yetu ilishughulikia hali hiyo vizuri. Siku hiyo hiyo, wafanyakazi wetu walitengeneza mwingine wa asili. Tunajaribu kutoa vifaa mbadala wa umeme kwa ajili ya kutoa mwangaza."

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bhandup West 'S Division' Dr. Avinash Vydande ameiambia BBC Marathi kuwa suala zima linachunguzwa na baada ya ripoti kamili kupatikana, itawezekana kutoa maoni juu ya kile kilichotokea na kisha hatua zitachukuliwa dhidi ya wahalifu.

Ukosefu wa vifaa katika hospitali ya manispaa?

agruti Patil, aliyekuwa mkuu wa idara hii, amedai kuwa kumekuwa na matukio ya uzembe wa madaktari katika hospitali ya Sushma Swaraj Prasrutigriha.

Akizungumza na BBC Marathi, alisema, "Hospitali ya manispaa haina vifaa. Licha ya malalamiko ya mara kwa mara, hakuna hatua zinazochukuliwa. Nilifika huko saa 12.30 jioni siku ambayo tukio hilo lilitokea na nilikuwa hospitalini hadi saa 4.50 asubuhi. Baada ya simu za mara kwa mara, mkuu wa hospitali saa nane unusu asubuhi ndio alifika huko. Jenereta katika hospitali hiyo haijatumika tangu tarehe 27 Aprili. Pia tumelalamika kuhusu suala hilo kwa serikali."

Jagruti Patil alisema kuwa umeme ulikatika mara saba tangu asubuhi ya siku ya tukio hilo.

Mipango mbadala ya nishati inaweza kufanywa kwa urahisi katika miji kama Mumbai ikiwa jenereta haifanyi kazi. Taa zinazoendeshwa kwa betri zinaweza kuwekwa.

Mkuu wa hospitali hiyo Dkt. Chandrakala Kadam amekubali kuwa kulikuwa na makosa ya wafanyakazi wake na pia ametoa barua ya maandishi.

Hata hivyo, hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao. Kamati ya uchunguzi imeteuliwa na manispaa. Lakini Jagruti Patil pia aliibua swali kwamba licha ya kupoteza maisha ya mwanamke na mtoto mchanga, utawala unajaribu kuokoa nani na kwa nini.

Hatutakaa kimya juu ya suala hili. Kutokana na ukosefu wa vifaa katika manispaa hiyo, maandamano yatapelekwa hospitalini Jumatatu na mbunge wa zamani Kirit Somaiya pia atakuwepo katika hafla hii.

'Dada yangu aliuawa'

"Sahidun alikuwa mdogo zaidi kati ya ndugu zetu wote. Alikuwa ni mtu mchangamfu sana baada ya ndoa na wakati wa ujauzito. Nilikuwa nikizungumza naye kwenye simu kila siku.

Hakuwa na tatizo. Mtoto wake ambaye hajazaliwa pia alikuwa katika hali nzuri.

"Aliniomba nilete vitu kwa ajili ya mtoto kutoka kijijini. Nilileta vitu vyote kwa ajili yake. Mfuko wa vitu vilivyoletwa kwake sasa umelala hapo. Mtoto pia ametutoka. Dada yangu alishambuliwa na kuuawa. Baba yetu anashangazwa na kifo chake," Shahjahan alielezea hisia zake.

"Nilikuwa nimechoka kuwaomba waniruhusu nimwone mtoto, lakini hakuna mtu ambaye angenipa nafasi yoyote. Mtoto wetu alikuwa bado amezaliwa.Damu ilimwagika karibu na mdomo wake. Nzi walikuwa wakizunguka karibu naye. Mtoto wetu alikuwa ameachwa bila kushughulikiwa. Leseni ya muuguzi na daktari anayemtibu dada yangu inapaswa kufutwa, hapaswi kuajiriwa popote. Tunataka haki," alisema Shah Jahan.

Maafisa wasiojua wajibu wa umeme

Hakuna mtu anayejua ni nani hasa anayehusika na kukatika kwa umeme katika suala hili lote.

Akizungumza na BBC, Mayur Bhagwat, mhandisi wa umeme katika idara ya umeme, alisema,"Wizara yetu haihusiki na umeme wa hospitali. Hatujui ni nini hasa kilichosababisha kukatika kwa umeme katika eneo hilo na ikiwa jenereta ya hospitali imewashwa au imezimwa."

Mhandisi Mkuu wa MSCB, ambaye anhusika na nishati ya ziada ya umeme katika sehemu hiyo, hakupatikana kwa maoni.

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi